Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 30 Septemba 2014 10:41

Sura ya Al Furqan, aya ya 56-59 (Darsa ya 632)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 632 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 25 ya Al Furqan. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 56 na 57 ambazo zinasema:


وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلاَّ مُبَشِّرًا وَنَذِيرًا


Nasi hatukukutuma ila uwe ni Mbashiri na Mwonyaji.


قُلْ مَا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ مِنْ أَجْرٍ إِلاَّ مَن شَاء أَن يَتَّخِذَ إِلَى رَبِّهِ سَبِيلا


Sema: Sikukuombeni ujira juu yake; isipokuwa atakaye ashike njia iendayo kwa Mola wake Mlezi.

Katika darsa iliyopita tulizungumzia upinzani usio na hoja wa makafiri na washirikina wa kuipinga haki na kushikilia imani yao ya kuabudu masanamu na vitu ambavyo havikuwa vikiwapa faida wala kuwaletea madhara yoyote. Aya hizi tulizosoma zinamhutubu Bwana Mtume kwa kusema: jukumu lako wewe kwa watu hawa ni kuwaonya na kuwapa indhari, ikiwa hawatokubali si kwamba kazi unayoifanya ina ila au kasoro. Bali ni kwa sababu wao wenyewe hawataki kuacha upotofu na kufuata uongofu.
Ewe Mtume! Wewe hujawaomba wao pesa au malipo yoyote, hata kwa sababu ya kukwepa kutoa malipo hayo waamue kuyapa mgongo yale unayowaeleza. Malipo ya kazi yako wanayalipa wale watu wanaoitafuta njia ya kuwafikisha kwa Mwenyezi Mungu na wanaomfikia Mola wao kwa kufuata uongofu na mwongozo wako. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kazi ya Mitume ni kuwaelekeza watu kwenye uongofu, si kuwalazimisha waikubali dini ya Allah wanayowalingania. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa utoaji miongozo na ufanyaji tablighi, na uonyaji na utoaji bishara njema huwa na faida na taathira yanapofanywa kwa pamoja. Kadhalika aya hizi zinatuelimisha kwamba Mitume wanawalingania watu wito wa kumtii Mwenyezi Mungu na si kuwatii wao; na wanatarajia kupata malipo ya kazi yao kwa Yeye Allah SW na si kwa wanadamu.
Ifuatayo sasa ni aya ya 58 ambayo inasema:


وَتَوَكَّلْ عَلَى الْحَيِّ الَّذِي لا يَمُوتُ وَسَبِّحْ بِحَمْدِهِ وَكَفَى بِهِ بِذُنُوبِ عِبَادِهِ خَبِيرًا


Na mtegemee Aliye Hai, ambaye hafi. Na umtukuze kwa sifa zake. Na yatosha kuwa Yeye ni Mwenye khabari za dhambi za waja wake.

Aya hii inaendeleza maudhui ya aya iliyotangulia kuhusu kutohitaji Mtume malipo ya mali kwa watu na kueleza kwamba egemeo na tegemeo lake Bwana Mtume ni Allah SW peke yake; mambo yake yote amemwachia Yeye na ametawakali na kumtegemea Yeye Mola. Ghairi ya Mwenyezi Mungu ambaye ni wa mwanzo na wa mwisho, vingine vyote ni vyenye kumalizika na kutoweka na kwa hivyo havina thamani ya kuvifanya vitegemewe. Ni Allah SW tu aliye hai milele na kwa hivyo mwanadamu anaweza kumtegemea na kutawakali kwake. Kwa kutawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu mwanadamu hawi na hofu wala woga wa mtu au kitu chochote, na wala hahisi kupoteza wala kupata madhara kwa amali anazotenda. Mtu kama huyo huwa mithili ya tone la mchirizi wa maji ulioungana na bahari pana isiyo na mpaka; bahari yenye adhama ambayo ndiyo chemchemi na chanzo cha uhai, inayostahiki kutukuzwa na kuhimidiwa na ndiyo anayopasa mtu kutawakali kwayo na kuitegemea. Kisha aya inaendelea kwa kumhutubu Bwana Mtume SAW kuwa: wewe huna dhima yoyote kutokana na uasi na kuipa mgongo haki kunakofanywa na wapinzani; hayo wayafanyayo mwachie Mola wako, kwani Yeye ni mjuzi zaidi wa hali zao na uafriti waufanyao, Naye ataamiliana nao kwa namna atakayoona inafaa kulingana na uadilifu wake na hikma yake. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba wafanya tablighi ya dini hawatakiwi kuwa na tamaa ya mali na utajiri wa watu bali wanapaswa wazisabilie nafsi zao kwa Allah aliye hai na mwenye kubaki milele daima dawamu, na kumfanya kuwa ndiye mlinzi wao katika masuala yote ya maisha yao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa waja wa kweli wa Mwenyezi Mungu huwa washukurivu kwa Mola wao katika hali zao zote na wala hawamnasibishii Yeye ila, kasoro wala upungufu wowote. Wa aidha aya hii inatutaka tujiepushe na kuchunguza na kutaka kujua madhambi waliyonayo watu. Allah SW ni mjuzi wa kila kinachofanywa na waja wake na hilo pekee linatosha.
Darsa ya 632 ya Qur'ani inahatimishwa na aya ya 59 ambayo inasema:


الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَى عَلَى الْعَرْشِ الرَّحْمَنُ فَاسْأَلْ بِهِ خَبِيرًا


Ambaye ameumba mbingu na ardhi, na vilivyomo ndani yake kwa siku sita. Kisha akatawala juu ya A'rshi, Arrahman, Mwingi wa Rehema! Basi muombeni Yeye Mwenye habari (ya mambo yote).


Aya hii inaendeleza maudhui iliyozungumziwa katika aya iliyopita kwa kuashiria qudra na uwezo wa Allah SW katika uumbaji na uendeshaji ulimwengu na kueleza kwamba Yeye Mola Muumba aliziumba mbingu na ardhi katika nyakati sita kisha akashughulika na tadbiri na uendeshaji wa masuala ya viumbe wake. Yeye Allah ametamalaki na kutawala juu ya kila kitu; tadbiri na uendeshaji wa ulimwengu uko mikononi mwake, na hakuna chochote kinachoweza kutoka nje ya mamlaka ya utawala wake. Bila ya shaka mfumo wa uumbaji wa ulimwengu umesimama juu ya msingi wa rehma za Allah SW, na viumbe wote wakiwemo wanadamu daima wananeemeka na rehma, uraufu na fadhila zake Mola. Awe ni muumini au kafiri, wote hao wanafaidika na neema, rehema na riziki wanazoruzukiwa na Allah.
Kwa hivyo ewe Mtume, na enyi waumini ikiwa mnataka kujua hakika ya ulimwengu, jinsi ulivyoumbwa na namna unavyoendeshwa, yatafuteni hayo kwa Mungu na Mola aliye Mjuzi zaidi na mwenye habari zaidi za kila kitu, na si kuwaendea watu wanaojisemea mambo kwa dhana na makisio tu na kujibunia nadharia hizi na zile; hali ya kuwa wao si waumbaji wa ulimwengu na wala hawakusimamia uumbwaji wake! Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba uumbaji wa ulimwengu ulifanyika hatua kwa hatua na katika nyakati tofauti, na si katika wakati mmoja na kwa mpigo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa tadbiri na uendeshaji ulimwengu unafanyika kwa rehma za Allah, kama ambavyo uumbaji wake pia ulifanyika kutokana na rehma zake Mola Muumba. Aidha aya hii inatuelimisha kwamba ulimwengu umeumbwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu na uko chini ya udhibiti wake kamili Yeye Mola. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kuwa kama tunataka kuijua hakika na haki na kupata majibu ya masuali yetu ya dini tuwaendee kuwauliza watu weledi na wajuzi wa dini. Kwa haya machache wapenzi wasikilizaji tunaifunga darsa yetu hii. Tunamwomba Allah atuonyeshe haki na kutuwafikisha kuifuata na atuonyeshe batili na kutuwezesha kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)