Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 30 Septemba 2014 10:33

Sura ya Al Furqan, aya ya 53-55 (Darsa ya 631)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 631 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 25 ya Al Furqan. Tunaianza darsa yetu hii kwa aya ya 53 ambayo inasema:


وَهُوَ الَّذِي مَرَجَ الْبَحْرَيْنِ هَذَا عَذْبٌ فُرَاتٌ وَهَذَا مِلْحٌ أُجَاجٌ وَجَعَلَ بَيْنَهُمَا بَرْزَخًا وَحِجْرًا مَّحْجُورًا


Naye ndiye aliye ziunganisha bahari mbili, hii ni tamu mno, na hii ya chumvi chungu. Na akaweka baina yao kinga na kizuizi kizuiacho.

Aya hii inaendelea na maudhui iliyowahi kuzungumziwa katika baadhi ya aya zilizopita zilizotaja neema kadhaa za Allah SW, ambapo kwa upande wake inaashiria moja ya ishara za qudra na uwezo wa Mola katika uumbaji kwa kueleza kwamba: mbali na maji ya mvua yanayozitosheleza na kuzishibisha ardhi zenye kiu pamoja na wakaazi wake, kuna na bahari mbalimbali pia ambazo sehemu moja ya maji yake ni matamu na yenye kuburudisha, na sehemu yake nyengine ni yenye chumvi na machungu. Pamoja na kwamba aina mbili hizo za maji ziko mahala pamoja na zimeungana, lakini huchukua muda mrefu sana bila ya kuchanganyika maji matamu na yale ya chumvi, huku kila moja kati yao yakibaki katika hali yake ile ile. Kwa maneno mengine, kuna kizuizi kisichoonekana baina ya maji ya chumvi yenye uchungu na maji baridi na matamu ambacho kinazuia kuchanganyika pamoja maji hayo. Leo hii imedhihirika kwamba tofauti iliyopo ya uzito baina ya maji ya chumvi na maji baridi na matamu ndiyo inayoyafanya maji ya aina mbili hizi yabaki kwa muda mrefu sana bila ya kuchanganyika. Katika baadhi ya bahari kuu aina mbili hizi za maji, yaani matamu na ya chumvi, zinaonekana pamoja. Mfano mwengine hai wa hali hii ni maji ya mito. Mito mikubwa humwaga baharini kiwango kikubwa cha maji baridi na matamu. Katika eneo kubwa la mahali yanapoingilia baharini maji hayo ya mito, maji yanayokuwepo kandokando ya pwani ya bahari huwa matamu na baridi, na huchukua muda mrefu bila ya kuchanganyika na maji ya chumvi ya baharini. Maji haya matamu huwa ni yenye faida kwa watu waishio maeneo hayo ya pwani ambao huyatumia kwa ajili ya shughuli zao za kilimo na umwagiliaji maji wa konde na mashamba yao. Katika ulimwengu wa maisha ya watu pia, japokuwa inayumkinika muumini na kafiri wakawa wanaishi pamoja katika mji na mahali fulani lakini kitakuwepo kizuizi cha kuufanya ukafiri wa kafiri usiweze kupenya ukaathiri na kuchafua imani ya muumini. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba ulimwengu wote wa maumbile uko kwenye mamlaka ya Allah SW, Muumba wa kila kitu, na ni Yeye aliyepanga na kuweka sheria na kanuni zinazotawala katika ulimwengu huo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kwa ajili ya kuendelea maisha ya viumbe kuna ulazima wa kuwepo maji baridi na matamu na pia maji machungu ya chumvi. Viumbe waishio nchi kavu wanahitaji maji matamu, na viumbe wa baharini, wao wanahitaji maji ya chumvi; na Yeye Allah Muumba wa viumbe hao amemtengea kila mmoja wao fungu lake.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 54 ambayo inasema:


وَهُوَ الَّذِي خَلَقَ مِنَ الْمَاء بَشَرًا فَجَعَلَهُ نَسَبًا وَصِهْرًا وَكَانَ رَبُّكَ قَدِيرًا


Naye ndiye aliye muumba mwanaadamu kutokana na maji, akamjaalia kuwa na (mafungamano) ya nasaba na sababu. Na Mola wako Mlezi ni Muweza.

Baada ya aya iliyotangulia iliyoashiria nafasi na mchango wa maji ya mvua na maji ya baharini katika kuendeleza maisha ya viumbe, aya hii inasema Mwenyezi Mungu amekuumbeni nyinyi wanadamu kutokana na maji pia. Na hilo ni kwa mwanadamu wa mwanzo, ambaye kwa irada yake Allah jalla fii ulaah aliumbwa kutokana na mchanganyiko wa maji na udongo, na pia kwa wanadamu waliofuatia baada yake ambao wametokana na tone la manii, huku maisha yao pia yakiwa yanategemea maji. Ghairi ya Mwenyezi Mungu aliyetukuka, ni nani mwengine awezaye, kutokana na tone la maji, kupamba na kutia sura kwa namna ya kupendeza na kuvutia kama hii; na ambaye katika muda wa miezi tisa hulibadilisha tone la maji kuwa kiumbe kamili chenye macho, masikio, ulimi, mikono, miguu, moyo, ubongo na viungo vinginevyo!? Hii yenyewe ni ishara na alama ya wazi kabisa ya qudra na uwezo usio na mpaka wa Muumba wa mwanadamu.
Kisha baada ya kuzungumzia uumbwaji wa mwanadamu aya imeashiria kuongezeka kwa vizazi vya kiumbe huyo. Katika kubainisha hilo inataja nafasi ya kuzaliana wanadamu kwa njia ya ndoa na kupatikana mafungamano na mahusiano baina yao ya ujamaa wa nasaba na wa sababu, ambapo kati ya viumbe wote mafungamano na mahusiano ya aina hii yako baina ya wanadamu tu peke yao. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu akayafanya mafungamano hayo yawe na heshima na staha maalumu pamoja na hukumu zake makshsusi. Mfungamano na uhusiano wa nasaba ni uhusiano unaokuwepo baina ya watu kwa njia ya uzawa. Baba na mama pamoja na watoto, au dada na kaka, shangazi na mama mdogo, au mjomba na ami n.k, hao wote wanahisabika kuwa maharimu wa mtu kwa nasaba. Baada ya mtu kuoa, baina ya mtu na jamaa wa mkewe hupatikana ujamaa wa sababu. Kwa mfano baba na mama wa mke au kama mke mwenyewe atakuwa na watoto, wote hao huwa maharimu wa mume kwa sababu. Miongoni mwa mafunzo ya kuzingatiwa katika aya hii ni kwamba wanadamu wote wametokana na chimbuko moja. Kwa hivyo ni upuuzi usio na msingi kwa watu kujikweza, kujitukuza na kujiona bora kuliko wenzao kwa sababu ya kabila, rangi au asili zao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kwa upande wa kimwili mwanadamu hana ubora wowote kuliko mnyama kwa sababu wote wawili, yaani mwanadamu na mnyama wameumbwa kutokana na maji. Kadhalika aya hii inatuelimisha kwamba kuutalii uumbwaji wa mwanadamu akiwa katika hali ya kiinitete ni njia bora ya kuthibitisha qudra, uwezo na adhama ya Muumba wa ulimwengu na vilivyomo ndani yake.
Darsa yetu ya leo inahatimishwa na aya ya 55 ambayo inasema:


وَيَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّهِ مَا لا يَنفَعُهُمْ وَلا يَضُرُّهُمْ وَكَانَ الْكَافِرُ عَلَى رَبِّهِ ظَهِيرًا


Na wanayaabudu badala ya Mwenyezi Mungu yasiyo wafaa wala yasiyo wadhuru. Na kafiri daima ni msaidizi wa (wapotofu na makafiri) wa kumpinga Mola wake Mlezi.

Washirikina, ambao walikuwa wakimkubali Mwenyezi Mungu kuwa ni Muumba, walikuwa wakitegemea pia vitu na viumbe vingine katika maisha yao na wakawa wanaviabudu vitu na viumbe hivyo kwa sura na namna tofauti. Katika aya hii tuliyosoma Mwenyezi Mungu anasema: maabudu na miungu hao bandia na wa kubuni hawakufaidisheni wala kukudhuruni kwa chochote. Ikiwa Mwenyezi Mungu atataka ikupateni dhara yoyote wao hawana uwezo wa kuizuia. Kama ni hivyo kwa nini badala ya kumwabudu kwa ikhlasi Muumba wenu na kudhihirisha uja wenu kwake mnawaendea wengine na kujiingiza kwenye shirki? Hao wengine mnaowaabudu, wawe ni kitu au mtu yeyote yule wameumbwa na Mwenyezi Mungu, na bila ya irada na kutaka Yeye Mola hawawezi kuwa na taathira yoyote kwa maisha yenu. Lakini kama mtakuwa waja wa kweli wa Allah, Yeye Mola wenu amekuruhusuni kutumia nyenzo na njia alizozijuzisha kutumia kwa ajili ya kupata matilaba yenu na kukidhi mahitaji yenu.
Kisha aya inaendelea kwa kusema: washirikina na makafiri wanasaidiana katika kufanya mambo yao ya batili na upotofu na kila mara hufanya propaganda kwa madhumuni ya kuipa nguvu zaidi fikra yao batili. Kwa hivyo na nyinyi Waislamu pia simameni imara katika njia yenu ya haki na muwe mnasaidiana wenyewe kwa wenyewe. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba ikiwa tunataka kupata manufaa na kuepukana na madhara katika maisha haya ya dunia, basi tumwombe Mungu ambaye upataji wa manufaa yote na uepukaji wa madhara yoyote yale uko mikononi mwake, na si kuwaendea na kuwapigia magoti watu na vitu ambavyo vyenyewe havina lolote vililonalo. Aidha aya hii inatuelimisha kuwa makafiri huwa wanasaidiana na kupeana msukumo katika ukafiri wao. Kwa hivyo waumini nao wanapaswa wawe na umoja na mshikamano baina yao ili wasije wakashindwa na maadui hao wa Allah. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 631 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atulinde na kila aina ya shirki, ya siri na ya dhahiri. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)