Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 30 Septemba 2014 10:23

Sura ya Al Furqan, aya ya 50-52 (Darsa ya 630)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 630 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 25 ya Al Furqan. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 50 ambayo inasema:


وَلَقَدْ صَرَّفْنَاهُ بَيْنَهُمْ لِيَذَّكَّرُوا فَأَبَى أَكْثَرُ النَّاسِ إِلاَّ كُفُورًا


Na kwa hakika tumeisarifu kati yao wapate kukumbuka. Lakini akthari ya watu hawakuchagua njia nyengine ila kukufuru.

Mwenyezi Mungu Mtukufu ameteremsha aya za kitabu chake cha Qur'ani kwa sura na namna tofauti kwa ajili ya kuwahidi na kuwaonyesha watu uongofu. Baadhi ya aya zimekuja kwa sura ya kutoa bishara na baadhi ya nyengine kwa namna ya kuonya na kutoa indhari. Kuna aya zilizo na sura ya kuamrisha na kuna zile zilizokuja kwa sura ya kukataza. Aya nyengine za kitabu hicho cha mbinguni zinasimulia visa, habari na hatima za kaumu zilizotangulia, na kuna aya zinazoelezea habari na matukio yatakayojiri Siku ya Kiyama. Kuna baadhi ya aya za Qur'ani zinazobainisha huruma, upole na uraufu wa Allah SW na kuna zile zinazoonyesha ukali wa ghadhabu na adhabu ya Mola. Sura na hali zote hizi tofauti za aya za Qur'ani zimekuja ili kumfanya mwanadamu akumbuke na azinduke kwa kutosahau yaliyopita nyuma yake na vile vile awe na dukuduku na wahasha juu ya hatima na mustakabali wake. Pamoja na hayo historia inaonyesha kuwa kutokana na kufuata hawaa na matamanio ya nafsi zao, kila mara akthari ya watu badala ya kukumbuka hayo na kuyazingatia na hivyo kufuata njia iliyonyooka ya Allah huamua kuikengeuka na kuipa mgongo haki. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba hatari ya mwanadamu kughafilika na nafsi yake pamoja na Muumba wake ni hatari kubwa inayomkabili kiumbe huyo. Kwa hivyo kuna ulazima wa kila mara na kwa mbinu na njia tofauti kumzindua, kumkumbusha na kumtanabahisha mwanadamu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kuyaweka kando maamrisho ya Mola katika maisha ya mtu binafsi na ya kijamii ni kufuru na ukanushaji mkubwa zaidi wa neema za Mwenyezi Mungu.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 51 ambayo inasema:


وَلَوْ شِئْنَا لَبَعَثْنَا فِي كُلِّ قَرْيَةٍ نَذِيرًا


Na kama tungetaka tungepeleka katika kila mji Mwonyaji.

Katika suala la Utume, kwamba mtu gani na katika zama na mahala gani abaathiwe na kupewa Utume, hilo liko kwenye mamlaka ya Allah SW, na wanadamu hawana nafasi yoyote katika jambo hilo. Na Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwa elimu na hikma yake humchagua mtu anayefaa kwa ajili ya kubeba jukumu hilo adhimu. Kwa hivyo katika kujibu matakwa hewa na yasiyo na msingi ya Washirikina wa Kikureishi, ambao kwa kutaka kudhoofisha hadhi na nafasi ya Bwana Mtume walikuwa wakisema: hivi isingekuwa bora kama Mwenyezi Mungu angemtuma Mtume katika kila mji na mahali, aya hii inasema: kama Mwenyezi Mungu angetaka angefanya hivyo. Lakini kwa elimu na hikma yake, Yeye Mola amemtuma Nabii Muhammad SAW na kumtaka atangaze na kuilingania dini yake kwa walimwengu wote. Na jambo hili linaonyesha hadhi na nafasi ya mtukufu huyo mbele ya Allah SW. Hakika aya hii inabainisha kwa namna fulani ujumuishi na ukamilifu wa dini tukufu ya Uislamu na kuhitimishwa Utume na Nabii Muhammad SAW. Kwa sababu kwa kuletwa mtukufu huyo hakuna haja tena ya kuja Mtume mwengine; na dini aliyokuja nayo inao uwezo wa kuendesha jamii zote za wanadamu za kila zama na mahali. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba kulinda na kudumisha umoja katika uongozaji wa jamii ni miongoni mwa usuli na misingi ya Uislamu. Aidha aya hii inatuelimisha kuwa Utume si suala la uchaguzi bali ni suala la uteuzi unaofanywa na Allah SW mwenyewe, kwa hivyo wanadamu hawana mchango wala sauti yoyote katika jambo hilo.
Darsa yetu ya 630 inahatimishwa na aya ya 52 ambayo inasema:


فَلا تُطِعِ الْكَافِرِينَ وَجَاهِدْهُم بِهِ جِهَادًا كَبِيرًا


Basi usiwat'ii makafiri. Na pambana nao kwayo (Qur'ani) kwa Jihadi kubwa.

Baada ya aya iliyotangulia kubainisha hadhi na nafasi aali na tukufu ya Bwana Mtume SAW aya hii inamhutubu mtukufu huyo kuwa: katika suala la kuwalingania na kuwaita makafiri kwenye dini ya Allah ya Uislamu usikubali katu kufanya maridhiano nao, bali jadiliana nao na kabiliana na upotofu wao kwa kutumia Qur'ani, na wala usiwe tayari abadani kusalimu amri mbele ya matakwa yao. Kwa hakika kinyume na propaganda zinazofanywa na kuenezwa na maadui wa Uislamu, za kudai kwamba dini hiyo tukufu imeenea katika pembe mbali mbali za dunia kwa vita na upanga, aya hii tuliyosoma inaonyesha kuwa kwa mujibu wa aya za Qur'ani, jihadi ya kifikra na kiutamaduni inatangulizwa na kupewa kipaumbele cha kwanza kuliko aina nyengine yoyote ile ya jihadi na inaeleza kwamba: katika kupambana na makafiri, kwanza kabiliana nao kwa jihadi ya kifikra. Kwa sababu hakuna shaka kwamba silaha ya hoja na mantiki, na tena basi inayotokana na maneno ya wahyi inafanya kazi zaidi kuliko silaha ya upanga. Tunapoitupia jicho ramani ya jiografia ya nchi za Kiislamu inatubainikia kuwa leo hii nchi ya Kiislamu yenye idadi kubwa zaidi ya Waisalmu yaani Indonesia, ambayo ina idadi ya Waislamu wapatao milioni 200 iliupokea na kuukubali Uislamu pasina jeshi la Waislamu kutumwa katika ardhi ya nchi hiyo. Kimsingi hasa ni kwamba Waislamu wa mashariki ya Asia kuanzia China hadi Malaysia, Indonesia na Ufilipino, nchi ambazo kiujumla zina idadi kubwa ya Waislamu, hawakushambuliwa kijeshi kwa ajili ya kulinganiwa Uislamu. Watu wa nchi hizi walisilimu na kuifuata dini ya haki ya Allah kupitia mabadilishano ya kibiashara na kiutamaduni tu na Waislamu wa maeneo mengine ya dunia. Aidha kusambaa kwa wimbi la watu wenye kiu, hamu na shauku ya Uislamu barani Ulaya na Marekani ambalo limewafadhaisha na kuwatia wahka wanasiasa wa Magharibi na viongozi wa Kanisa, hiyo pia sababu yake ni kwamba kuna Wamagharibi ambao baada ya kuitalii na kuihakiki Qur'ani na Uislamu wameweza kuyaelewa mafundisho aali ya dini hii tukufu. Na ni wazi kwamba hakuna ulazimishaji wala utezaji nguvu wa aina yoyote uliowafanya watu hao wavutiwe na kuukubali Uislamu. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba mtu muumini hawi tayari asilani kusalimu amri mbele ya matakwa potofu na yasiyo sahihi ya makafiri na huwa hayuko tayari kufikia maridhiano nao juu ya jambo hilo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kuwaita na kuwalingania watu Uislamu kunapasa kufanyike kwa msingi wa mafundisho ya Qur'ani, na huu ni wajibu wa watu wote. Kwa maneno mengine, Qur'ani ni wenzo bora zaidi na madhubuti zaidi kwa ajili ya kukabiliana na makafiri kwa jihadi ya kifikra na kiutamaduni. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba jihadi kubwa zaidi ni jihadi ya kifikra na kielimu ya kupambana na upotofu unaoenezwa kila siku na makafiri kwa kutumia njia na mbinu mpya. Kwa haya machache wapenzi wasikilizaji tunaifunga darsa yetu hii. Tunamwomba Allah awape Waislamu uelewa wa kuijua thamani ya neema waliyojaaliwa ya Uislamu na awafanye wasio Waislamu waifahamu na kuifuata nuru hiyo ya uongofu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)