Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 30 Septemba 2014 10:11

Sura ya Al Furqan, aya ya 45-49 (Darsa ya 629)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 629 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 25 ya Al Furqan. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 45 na 46 ambazo zinasema:


أَلَمْ تَرَ إِلَى رَبِّكَ كَيْفَ مَدَّ الظِّلَّ وَلَوْ شَاء لَجَعَلَهُ سَاكِنًا ثُمَّ جَعَلْنَا الشَّمْسَ عَلَيْهِ دَلِيلا


Je! Huoni jinsi Mola wako Mlezi anavyo kitandaza kivuli. Na angeli taka angeli kifanya kitulie tu. Kisha tumelifanya jua kuwa ni dalili yake.


ثُمَّ قَبَضْنَاهُ إِلَيْنَا قَبْضًا يَسِيرًا


Kisha tunakivutia kwetu kidogo kidogo.

Katika darsa iliyopita yalielezewa na kupatiwa majibu baadhi ya matarajio hewa na muamala muovu wa washirikina kwa Bwana Mtume Muhammad SAW. Aya hizi na nyengine zitakazofuatia zimeashiria alama na ishara za Mwenyezi Mungu mbinguni na ardhini na kueleza kwamba moja ya neema za Allah ni kivuli ambacho huwa sababu ya kuingia usiku na kupatikana fursa ya kupumzika watu na viumbe wengine wote walioko katika sayari ya dunia. Katika mzunguko wa sayari ya dunia kulizunguka jua, kila mara nusu ya sayari hiyo huwa katika mwanga na nusu nyengine huwa katika kiza. Kwa hakika kiza hicho ni kivuli cha ule upande wa sayari ya dunia unaolielekea jua. Na ifikapo mwisho wa kutwa ya siku kivuli hicho huanza kuchomoza kidogo kidogo kikaenea na kuufanya usiku uingie. Kivuli hiki huwa kinaendelea hadi kabla ya kuchomoza jua la siku ya pili. Kwa maneno mengine, hicho ni kivuli kilichokuwepo kabla ya kuchomoza jua, na wakati jua linapochomoza hujikusanya kidogo kidogo na hatimaye kutoweka!
Ni wazi kwamba mfumo wa kuingia na kupishana usiku na mchana una nafasi na mchango muhimu katika maisha ya watu na viumbe wengine na huzuia kupanda kwa joto au kushuka kupita kiasi. Na ndio maana Qur'ani tukufu inasema katika aya za 71 na 72 za Suratul Qasas ya kwamba : Sema: Mwaonaje, Mwenyezi Mungu angeli ufanya usiku umekukalieni moja kwa moja mpaka Siku ya Kiyama, mungu gani asiye kuwa Mwenyezi Mungu atakaye kuleteeni mwangaza? Basi je, hamsikii? Sema: Mwaonaje, Mwenyezi Mungu angeli ufanya mchana umekukalieni moja kwa moja mpaka Siku ya Kiyama, mungu gani asiye kuwa Mwenyezi Mungu ataye kuleteeni usiku mkapumzika humo? Basi je, hamwoni? Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kutafakari juu ya vitu vya ulimwengu wa maumbile ni moja ya njia bora kabisa ya kumtambua Mwenyezi Mungu. Kwa sababu vitu vyote hivyo vimeumbwa kwa qudra na hekima yake ya Mola Mwenyezi. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa mzunguko wa sayari ya dunia kulizunguka jua si jambo linalotokea kwa sadfa na kwa bahati tu bali linafanyika kwa tadbiri ya Allah SW.
Ifuatayo sasa ni aya ya 47 ambayo inasema:


وَهُوَ الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ اللَّيْلَ لِبَاسًا وَالنَّوْمَ سُبَاتًا وَجَعَلَ النَّهَارَ نُشُورًا


Naye ndiye aliye kufanyieni usiku kuwa ni vazi, na usingizi kuwa mapumziko, na akaufanya mchana kuwa ni wa mtawanyiko.

Aya iliyotangulia imeashiria kutandawaa na kujikusanya kwa kivuli mwishoni na mwanzoni mwa kuanza kila siku. Baada ya hayo aya tuliyosoma inazungumzia moja ya matokeo ya hali hiyo ambayo ni kupatikana usiku na mchana na kueleza kwamba: giza la usiku ni mithili la nguo anayojifunika na kujigubika nayo mtu wakati wa kulala, ambalo huwafunika viumbe wote na kuwaandalia mazingira ya kuweza kulala na kupumzika ili hadi jua litakapochomoza waweze kujiandaa kwa ajili ya harakati na kushughulika na kazi zao katika siku nyengine. Kwa kawaida na kimaumbile, giza la usiku huwafanya watu waache na wasimamishe kufanya kazi na shughuli zao nyingi za kutwa. Na wakati mtu anapolala, harakati zake za kimwili pia hupungua na kufikia kiwango cha chini kabisa, kwa sababu wakati mtu anapolala, sehemu kubwa ya viungo vinavyofanya kazi mwilini hupumzishwa na sehemu nyenginezo kama moyo na mapafu hufanya kazi polepole na kwa utulivu zaidi. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba mzunguko wa usiku na mchana una malengo na mipango ya kihekima. Usiku na mchana ni miongoni mwa neema za Allah kwa wanadamu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa mwanadamu anahitaji utulivu; na usiku ndio wakati bora wa kulala na kupata utulivu huo. Wa aidha aya hii inatutaka tuelewe kwamba mchana ni wakati wa kufanya kazi, na usiku ni wakati wa kupumzika. Kuzibadilisha nyakati hizi kuna madhara kwa mtu na ni ufanyaji mambo kinyume na mkondo wa kimaumbile.
Aya za 48 na 49 ndizo zinazotuhatimishia darsa yetu hii. Aya hizo zinasema:


وَهُوَ الَّذِي أَرْسَلَ الرِّيَاحَ بُشْرًا بَيْنَ يَدَيْ رَحْمَتِهِ وَأَنزَلْنَا مِنَ السَّمَاء مَاء طَهُورًا


Naye ndiye anaye zituma pepo kuwa bishara njema kabla ya rehema yake, na tunayateremsha kutoka mbinguni maji safi.


لِنُحْيِيَ بِهِ بَلْدَةً مَّيْتًا وَنُسْقِيَهُ مِمَّا خَلَقْنَا أَنْعَامًا وَأَنَاسِيَّ كَثِيرًا


Ili kwayo tuihuishe nchi iliyo kufa, na tuwanyweshe wanyama na watu wengi tulio waumba.

Baada ya kutajwa neema ya usiku na mchana ambazo hutoa fursa kwa watu kufanya kazi na shughuli zao na kupumzika na kupata utulivu, aya hizi zinaashiria neema nyengine ya upepo na kueleza kwamba: mwendo na harakati ya mawingu yapitayo juu ya mito na bahari hadi kwenye maeneo yenye ardhi kavu vinafanyika kwa upepo na kutoa bishara ya kunyesha mvua kwa ardhi hiyo iliyoyabisika na yenye kiu ya maji.
Mwanadamu huchimba mitaro, akatandika mabomba na njia za chini kwa chini kwa ajili ya kufikisha maji kwenye maeneo ya ardhi kame, lakini Mwenyezi Mungu Mtukufu anayafikisha maji hayo kupitia angani. Kutokana na kushtadi nuru ya jua, maji ya bahari hugeuka mvuke na kupanda juu. Mkusanyiko na mrundiko wa mvuke wa maji katika hewa baridi ya angani husababisha kufanyika mawingu. Lakini baada ya hapo ni pepo ndizo zinazofanya kazi kuu ya kufanikisha unyeshaji wa mvua. Kwani pepo hizo huyasukuma mawingu yaliyokusanyika na kuyafikisha kila pembe ya dunia, na kila pale panapohitajika huyasitisha ili yadondoke kwa sura ya mvua ya kukidhi kiu ya maji iliyonayo ardhi ya mahala hapo.
Katika aya hizi Allah SW ameyaelezea maji ya mvua kuwa na sifa mbili maalumu. Moja ni ya kusafisha na kutoharisha na nyengine ni ya kuondoa kiu; ambapo katika hali zote hizo mbili maji hayo yana nafasi muhimu sana katika maisha ya mwanadamu. Ya kwanza ni katika afya na uzima wake na ya pili katika suala la chakula na ukuaji wake. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kuvuma kwa pepo na kunyesha kwa mvua si mambo yanayotokea kibahati tu, bali yanafanyika kwa msingi wa tadbiri na hekima ya Mola Mlezi. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa katika masuala yanayohusiana na kiwiliwili, mwanadamu huwa katika daraja moja na wanyama na wala hawi na ubora wowote wa kuwapita wao. Ikiwa anataka kufikia kwenye utukukaji na ukamilifu wa kiutu inampasa aupe umuhimu upande wake wa kiroho na kimaanawi. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba maji ni kitu safi kwa nafsi yake, na pia ni yenye uwezo wa kusafisha. Kwa haya machache wapenzi wasikilizaji tunaifunga darsa yetu hii. Tunamwomba Allah atuwezeshe kuwa washukurivu wa neema zake; tunazozijua na tusizozijua. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)