Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatano, 20 Agosti 2014 13:21

Sura ya Al Furqan, aya ya 35-40 (Darsa ya 627)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 627 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 25 ya Al Furqan. Tunaianza darsa yetu hii kwa aya za 35 na 36 ambazo zinasema:

وَلَقَدْ آتَيْنَا مُوسَى الْكِتَابَ وَجَعَلْنَا مَعَهُ أَخَاهُ هَارُونَ وَزِيرًا

Na hakika tulimpa Musa Kitabu na tukamweka pamoja naye nduguye, Harun, kuwa waziri.

فَقُلْنَا اذْهَبَا إِلَى الْقَوْمِ الَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا فَدَمَّرْنَاهُمْ تَدْمِيرًا

Tukawaambia: Nendeni kwa watu waliokanusha Ishara zetu. Basi tukawateketeza kabisa.

Katika darsa iliyopita tulivitaja baadhi ya visingizio vilivyokuwa vikitolewa na wapinzani wa Bwana Mtume SAW ili kuukataa wito wa haki aliowatangazia. Aya hizi zinamuelekea na kumhutubu Bwana Mtume na waumini kwa kusema: migongano na mivutano baina ya haki na batili imekuwako katika zama zote za historia na kuashiria baadhi ya mifano ya mivutano hiyo. Kwanza zinaelezea jukumu alilopewa Nabii Musa pamoja na ndugu yake Haroun AS la kwenda kumfikishia wito wa uongofu Firauni na wafuasi wake, ambapo kundi na tabaka hilo la madhalimu liliukataa na kuupinga wito wa Mitume hao wa Allah. Kwani badala ya kusikiliza maneno ya haki na kuyaamini waliamua kuyakadhibisha na kudai kwamba miujiza ya wazi kabisa waliyoonyeshwa na Nabii Musa ni uongo mtupu. Na kwa kuwa Firauni na kaumu yake waliamua kuipa mgongo haki na kuzidi kufanya dhulma na uonevu hatimaye waligharikishwa na kuangamizwa. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba Manabii wa Allah walikuwa walezi wenye uchungu ambao walikuwa wakitoka na kuwafuata watu ili kuwafikishia uongofu na kuwaonesha njia ya uokovu, na si kujikalia tu na kuwasubiri watu wawafuate wao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa katika suala la kufanya tablighi ya dini na katika kutekeleza majukumu makubwa kwa ujumla, badala ya kujifanyia mambo kila mtu peke yake tujitahidi kuwa na ushirikiano na kusaidiana, pamoja na kufanya kazi kwa fikra na mawazo ya pamoja. Kadhalika aya hizi zinatutaka tupate ibra na mazingatio kutokana na historia ya waliotangulia na wala tusiipinge haki, kwani matokeo ya kuipinga na kuikadhibisha haki ni kuhilikishwa na kuangamizwa.

Zifuatazo sasa ni aya za 37, 38 na 39 ambazo zinasema:

وَقَوْمَ نُوحٍ لَّمَّا كَذَّبُوا الرُّسُلَ أَغْرَقْنَاهُمْ وَجَعَلْنَاهُمْ لِلنَّاسِ آيَةً وَأَعْتَدْنَا لِلظَّالِمِينَ عَذَابًا أَلِيمًا

Na watu wa Nuhu, walipowakanusha Mitume, tuliwagharikisha, na tukawafanya ni Ishara kwa watu. Na tumewaandalia wenye kudhulumu adhabu yenye kuumiza.

وَعَادًا وَثَمُودَ وَأَصْحَابَ الرَّسِّ وَقُرُونًا بَيْنَ ذَلِكَ كَثِيرًا

Na (tuliwaangamiza) kina A'di na Thamudi na watu wa Rass na vizazi vingi vilivyokuwa baina yao.

وَكُلا ضَرَبْنَا لَهُ الأَمْثَالَ وَكُلا تَبَّرْنَا تَتْبِيرًا

Na wote tuliwapigia mifano, na wote tuliwaangamiza kabisa kabisa.

Kaumu nyingi katika zama zote za historia ziliwakadhibisha Mitume wa Allah ambapo baadhi ya kaumu hizo zimetajwa majina yao katika aya hizi tulizosoma. Kaumu ya Nabii Nuh (AS) ni miongoni mwa kaumu hizo ambapo Mtume huyo wa Allah alitumia muda wa miaka 950 kufanya kazi ya tablighi ya kuwafikishia watu wa kaumu yake ujumbe wa uongofu, lakini ni wachache tu miongoni mwao waliomwamini na kumfuata. Na kutokana na kuikadhibisha na kuipinga haki, kaumu ya Nuh (AS) iliangamizwa kwa tufani na gharika kubwa.

Nabii Hud (AS) alikuwa Mtume wa kaumu ya Aaad, na kwa watu wa kaumu ya Thamud alitumwa Nabii Saleh (AS). Kaumu mbili hizo zilikuwa zikiishi Bara Arabu ambapo athari zao zingali zimebakia hadi sasa. Nao As-habur rass ni kaumu nyengine pia ya watu waliomkadhibisha Mtume wao. Kwa mujibu wa baadhi ya hadithi watu hao walimuua shahidi Mtume wao. Amma kuhusu mahali walipokuwa wakiishi watu hao wa Rass, kuna rai tofauti baina ya maulamaa. Lakini nukta muhimu ni kwamba Allah SW anasema: Sisi tuliwatolea na kuwabainishia mifano watu wa kaumu zote hizo ya watu wa kaumu zilizopita. Lakini hawakupata ibra wala mazingatio, wakaamua kuendelea kuipinga haki na kuendelea kufanya maovu, dhulma na ufisadi hadi mwishowe wakaangamia. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba Qur'ani ni kitabu cha kupata ibra na mazingatio, si kitabu cha visa na simulizi. Ni kitabu cha kuaidhisha na kunasihisha, na si cha kuchangamsha na kuburudisha. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kuwakadhibisha Mitume na mafundisho yao ni dhulma kubwa inayomfanya mtu awe na hatima na mwisho mbaya. Wa aidha aya hizi zinatuelimisha kwamba Mwenyezi Mungu huwa kwanza anatimiza dhima kwa makafiri na madhalimu kwa kuwaonyesha hoja kamili za haki, wasipokubali wakaendelea kuikadhibisha haki na kufanya maasi ndipo anapowapa jaza ya ikabu na adhabu.

Tunaihatimisha darsa yetu hii kwa aya ya 40 ambayo inasema:

وَلَقَدْ أَتَوْا عَلَى الْقَرْيَةِ الَّتِي أُمْطِرَتْ مَطَرَ السَّوْءِ أَفَلَمْ يَكُونُوا يَرَوْنَهَا بَلْ كَانُوا لا يَرْجُونَ نُشُورًا

Na kwa hakika wao wamefika kwenye mji ulionyeshewa mvua mbaya. Basi, je, hawakuwa wakiuona? Bali walikuwa hawataraji kufufuliwa.

Aya hii inaashiria magofu na mabaki ya miji iliyoangamizwa ya kaumu ya Nabii Luti (AS). Kutokana na kukitihiri madhambi na maovu waliyokuwa wakifanya, watu wa kaumu hiyo waliteremshiwa adhabu ya mvua ya mawe kutoka mbinguni iliyowamiminikia na kuwaangamiza. Athari za mabaki hayo ziko katika njia itokayo Hijaz kuelekea Sham ya zama hizo ambapo washirikina wa Makka walikuwa wakipita njia hiyo wakati wa safari zao za kibiashara. Hata hivyo hawakuwa wakiziangalia athari hizo kwa jicho la kupata ibra na mazingatio na kupata funzo kutokana na jinsi hatima na mwisho wa watu hao ulivyokuwa. Na sababu ni kwamba kimsingi hasa hawakuwa wakiamini kuwa kuna Kiyama na malipo ya Pepo au Moto hata wafikirie nini yatakuwa malipo ya amali na matendo yao. Katika aya tulizozungumzia kwenye darsa yetu ya leo yametajwa makundi sita ambayo kila moja kati yao lilikuwa na upotofu wa kifikra au wa kimwenendo. Na licha ya watu wote hao kumakinika na kuwa na ukwasi wa mali, nguvu na mamlaka lakini walipatwa na ghadhabu za Allah na kuangamizwa kwa anuai za adhabu zikiwemo za tufani, umeme, gharika na zilzala. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba athari za kale zinaweza kuwa wenzo kwa watu kupata ibra na mazingatio. Kwa hivyo kuna ulazima wa kuzitunza na kuhifadhi athari zilizobaki za kaumu zilizotangulia ili ziweze kutoa ibra na mazingatio kwa wanaofuatia. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kuwa kusimulia historia na kubainisha hatima ya watu waliopotoka kwa kuipa mgongo njia ya haki kunaweza kuwa na athari nzuri katika malezi na uongozaji watu kuelekea kwenye uongofu. Na aidha aya hii inatuelimisha kuwa kuipuuza Siku ya Kiyama huwa sababu ya kuporomoka na kuangamia mtu hapa duniani. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 627 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa wenye kupata ibra na mazingatio kutokana na yaliyozisibu umma zilizopita. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)