Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatano, 25 Juni 2014 13:10

Sura ya Al Furqan, aya ya 31-34 (Darsa ya 626)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 626 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 25 ya Al Furqan. Tunaianza darsa yetu hii kwa aya ya 31 ambayo inasema:

وَكَذَلِكَ جَعَلْنَا لِكُلِّ نَبِيٍّ عَدُوًّا مِّنَ الْمُجْرِمِينَ وَكَفَى بِرَبِّكَ هَادِيًا وَنَصِيرًا

Na kama hivi tumemfanyia kila Nabii adui miongoni mwa wakosefu, na Mola wako Mlezi anatosha kuwa Mwenye kuongoza na Mwenye kunusuru.

Katika aya hii Allah SW anamfariji na kumliwaza Mtume wake wa mwisho Nabii Muhammad SAW kwa kumwambia: usidhani ni wewe tu umekabiliwa na watu wakaidi na wenye inadi kama hawa; mitume wote, katika zama zote za historia walikuwa na hali kama hiyo ya kukabiliwa na upinzani wa watu waovu na wabaya katika njia yao ya kufikisha wito wa tauhidi. Hata hivyo jua kwamba wewe huko peke yako bali Mwenyezi Mungu yuko pamoja nawe na ndiye mlinzi na msaidizi wako. Atakuongoza katika kukabiliana na hila zao na atakusaidia ili kuziviza njama zao na Uislamu uzidi kuenea siku baada ya siku.
Kimsingi hasa ni kwamba chaguo la kufuata njia ya haki au batili analifanya mtu kwa hiyari ambayo Mwenyezi Mungu amemjaalia kuwa nayo mja wake; na Yeye Mola amemwachia kila mtu achague njia anayotaka kufuata. Na kwa kuwa wanadamu wamejaaliwa uhuru na mamlaka hayo ya kuchagua, baadhi yao wanaamua kufuata njia ya batili, wanasimama kukabiliana na Mitume na hawako tayari kuyakubali maneno ya haki. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba mgongano baina ya haki na batili umekuwepo katika zama zote za historia ya wanadamu, na utaendelea kuwepo hadi mwisho wa historia yao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa dhambi na maovu humtenganisha mtu na njia ya haki. Na kuendelea kufanya maovu na madhambi huanza taratibu kumfanya mwanadamu awapinge Mitume na kuwa na uadui na wajumbe hao wa Allah. Vilevile tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba katika kuwakabili wapinzani, tutegemee qudra na nguvu zisizo na kikomo za Allah ambaye anatosha kuwa msaidizi na mwongozaji wetu.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya za 32 na 33 ambazo zinasema:

وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لَوْلا نُزِّلَ عَلَيْهِ الْقُرْآنُ جُمْلَةً وَاحِدَةً كَذَلِكَ لِنُثَبِّتَ بِهِ فُؤَادَكَ وَرَتَّلْنَاهُ تَرْتِيلا

Na wakasema wale waliokufuru: Kwa nini hakuteremshiwa Qur'ani yote mara moja? Hayo ni hivyo ili tuuthibitishe kwayo moyo wako, na ndio tumeisoma kwa mafungu.

وَلا يَأْتُونَكَ بِمَثَلٍ إِلاَّ جِئْنَاكَ بِالْحَقِّ وَأَحْسَنَ تَفْسِيرًا

Wala hawatakuletea mfano wowote, ila Nasi tutakuletea (jawabu) kwa haki, na tafsiri iliyo bora.

Makafiri na washirikina ambao hawakuwa tayari kuyakubali maneno ya Bwana Mtume walikuwa wakitoa visingizio mbalimbali ili kuyapinga maneno hayo ya haki. Mara walikuwa wakisema: kwa nini na sisi pia hatuteremshiwi wahyi? Na mara nyengine wakisema: kwa nini hatuwezi kumwona malaika wa wahyi? Katika aya hizi tulizosoma walikuwa wakisema: kwa nini Qur'ani haiteremshwi kwa Muhammad yote kwa pamoja ili tuweze kuielewa yote kwa ujumla na kujua maneno na maamrisho ya mungu wa Muhammad? Mwenyezi Mungu SW akawajibu wapinzani hao kwa maneno yao hayo kwa kusema: Sisi tumeziteremsha aya za Qur'ani kidogo kidogo ili Mtume awasomee watu kulingana na hali, mazingira, mambo na matukio yanayojiri na kuwabainishia kwa uwazi kabisa wanayopaswa kufanya kila pale inapohitajika. Kwa sababu yeye ana jukumu la kulea na kuwafunza watu, jambo ambalo linachukua muda na hufanyika hatua kwa hatua. Mtume ni mithili ya mlezi mwenye uchungu na huruma aliyeko pamoja na watu, ili kila wakati na katika kila hali aweze kuwaongoza kwenye njia sahihi. Yeye si kama mwandishi wa kitabu ambaye amealifu kitabu na kukichapisha kwa ajili ya watu wote lakini hana jukumu tena katika suala la kutoa mafunzo kwao au kuufanyia kazi muhtawa na yaliyomo ndani ya kitabu chake hicho. Yeye Mtume ni mwalimu ambaye kwa wanafunzi wa darsa la kwanza huwafundisha kwanza alifabeti tu na katika miaka inayofuata ndipo huanza kidogo kidogo na hatua kwa hatua kuinua viwango vya uwezo wao.
Akiwa Makka alipambana na shirki na kuabudu masanamu, na baada ya kuhajiri kuelekea Madina na kupatikana mazingira ya watu kuubali wito wa Laa ilaha illa Allah ndipo alipofikisha kwa watu maamrisho na mafundisho kama Sala, Funga na Zaka. Kimsingi katika suala la kujifunza na utoaji mafunzo, kitu kinachoyafanya mafunzo hayo yawe yathibiti na kukita ndani ya nyoyo na akili za wanafunzi ni kufanyika jambo hilo kidogo kidogo na hatua kwa hatua kulingana na ratiba iliyopangwa. Hakuna shaka yoyote kuwa ratiba ya kumwongoza mwanadamu imeshaainishwa na Allah kwa sura kamili, lakini katika hatua na marhala ya utekelezaji inabidi ifanyiwe kazi hatua kwa hatua, na wala hakuna haja mathalani lile linalopasa kufanywa katika mwaka wa kumi lifanyike katika mwaka ule ule wa kwanza. Kwani si hasha hilo likaifanya kazi iwe ngumu pia na kuwavunja moyo watu au hata kuwafanya wakimbie. Isitoshe ni kuwa kuteremshwa kidogo kidogo Qur'ani kunamfanya Bwana Mtume aendelee kuwa na mawasiliano na chemchemi ya wahyi, na hilo linazidi kuimarisha azma na irada yake ya kutekeleza jukumu lake la Utume. Lakini pia maneno yoyote ya tuhuma na yasiyo na msingi yanayotamkwa na maadui katika kila zama yanapatiwa jibu mwafaka na Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa njia ya aya za Qur'ani na kuwathibitishia watu hao ukweli wa Utume wa Nabii Muhammad SAW. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba mafunzo ya Qur'ani na hukumu za dini yanapasa yafanyike kidogo kidogo na kulingana na uwezo na utayarifu wa wanaokusudiwa kufunzwa. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa dini hai na iliyokamilika ni ile yenye mawasiliano ya karibu na matukio na minasaba. Aidha aya hizi zinatuelimisha kwamba usomaji Qur'ani unapasa uwe wa polepole na wa kutaamali na kutafakari. Kadhalika tunajifunza kutokana na aya hizi kuwa kusoma Qur'ani huufanya moyo wa muumini uwe imara na kuupa utulivu katika hali ya shida, tabu na misukosuko. Na vilevile aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba maneno ya wapinzani ni batili, na Qur'ani inakabiliana nayo kwa kubainisha haki kwa uwazi kabisa. Na hata kama utakuwemo ukweli katika baadhi ya wanayosema wapinzani hao lakini yasemwayo na Qur'ani ni bora zaidi na yaliyokamilika zaidi.
Darsa ya 626 ya Qur'ani inahatimishwa na aya ya 34 ambayo inasema:

الَّذِينَ يُحْشَرُونَ عَلَى وُجُوهِهِمْ إِلَى جَهَنَّمَ أُوْلَئِكَ شَرٌّ مَّكَانًا وَأَضَلُّ سَبِيلا

Wale watakaokusanywa na kubururwa kifudifudi mpaka kwenye Jahannamu, hao watakuwa mahali pabaya, ndio wenye kuipotea njia sana.

Wanadamu watafufuliwa Siku ya Kiyama kulingana na mwenendo na matendo yao ya hapa duniani. Mtu ambaye alijitia upofu wa kutoiona haki hapa duniani, Siku ya Kiyama atafufuliwa akiwa kipofu. Yule ambaye alikuwa mithili ya mnyama na hayawani na akawa ameelekeza fikira zake zote katika kujaza tumbo tu na kukidhi shahawa na matamanio yake ya kijinsia, siku hiyo atakuwa anatembea kama mnyama hoa wa miguu minne. Amma yule ambaye anaipa mgongo haki katika ulimwengu huu na kutakabari, Siku ya Kiyama atalazwa uso wake kifudifudi, abururwe na kukokotezwa chini huku akisukumizwa kuelekea motoni. Na amma wale ambao walikuwa wakijiona wajuzi na watambuzi zaidi kuliko watu wote na kujihisi bora kuliko wenzao na wakawa wanawaona waumini kuwa watu wajinga na wasiojua kitu, Siku ya Kiyama watabainikiwa kwamba wao walikuwa ndio watu waliopotoka zaidi. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba kuwadunisha wafuasi wa njia ya haki kutamfanya mtu awe duni na dhalili Siku ya Kiyama. Funzo jengine tunalopata katika aya hii ni kuwa pasina kuitambua njia ya haki tutajuaje kama tuko kwenye haki au upotofu au tuko karibu na tunakokusudia kwenda au tuko mbali nako? Wapenzi wasikilizaji darsa ya 626 imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuonyeshe haki na atuwafikishe kuifuata, na atuonyeshe batili na atuwezeshe kuiepuka.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)