Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatano, 25 Juni 2014 13:06

Sura ya Al Furqan, aya ya 27-30 (Darsa ya 625)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 625 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 25 ya Al Furqan. Tunaianza darsa yetu kwa aya za 27, 28 na 29 ambazo zinasema:

وَيَوْمَ يَعَضُّ الظَّالِمُ عَلَى يَدَيْهِ يَقُولُ يَا لَيْتَنِي اتَّخَذْتُ مَعَ الرَّسُولِ سَبِيلا

Na siku ambayo mwenye kudhulumu atajiuma mikono yake, na huku anasema: Laiti ningelishika njia pamoja na Mtume!

يَا وَيْلَتَى لَيْتَنِي لَمْ أَتَّخِذْ فُلانًا خَلِيلا

Ee Ole wangu! Laiti nisingelimfanya fulani kuwa rafiki!

لَقَدْ أَضَلَّنِي عَنِ الذِّكْرِ بَعْدَ إِذْ جَاءَنِي وَكَانَ الشَّيْطَانُ لِلإِنسَانِ خَذُولا

Kwa hakika amenipoteza, nikaacha Ukumbusho, baada ya kwisha nijia, na kweli Shet'ani ni khaini kwa mwanaadamu.

Katika darsa iliyopita tuliona jinsi Allah SW alivyotubainishia hali za waja wema na wabaya zitakavyokuwa Siku ya Kiyama. Aya hizi tulizosoma zinaendeleza maudhui hiyo na kueleza kwamba wale watu ambao hapa duniani waliyasikia maneno ya wajumbe wa Mwenyezi Mungu lakini waliyapuuza na wala hawakuyajali watajuta majuto makubwa Siku ya Kiyama kutokana na dhulma waliyozifanyia nafsi zao. Kwani watauma mikono yao kwa majuto makubwa yatakayowafika. Mtu ambaye aliikengeuka njia ya haki atasema siku hiyo mimi niliyapuuza aliyoyaleta Mtume kwa ajili ya kuwaamsha na kuwaelimisha watu na badala yake nikaenda kuwafuata marafiki waovu ambao walinipotosha. Ya laiti badala ya kufanya urafiki na watu wale lau kama ningeliifuata njia ya Mtume nisingaliishia kwenye upotofu. Hapo Allah SW atasema: Hayo yote ni matokeo ya hila za shetani ambaye humvuta na kumtoa mtu nje ya njia ya Mitume na kisha kumwacha kama alivyo, na kumfanya mtu huyo adhalilike na kuishia kwenye hali ya kutangatanga. Kwa hakika chanzo cha masaibu yote ya mwanadamu ni shetani; lakini yeye hutumia mbinu na nyenzo tofauti kwa ajili ya kumpoteza kiumbe huyo ambapo aya hizi tulizosoma zimeashiria moja ya mbinu iliyo muhimu zaidi yaani sahibu na rafiki mbaya.
Kitajiriba pia imethibitika kwamba marafiki wazuri au wabaya wanachangia sana hatima na majaaliwa ya mtu. Mtu atake asitake huwa anaathiriwa na mazingira yanayomzunguka; na kwa kuwa rafiki ni mtu aliyemchagua yeye mwenyewe na ana mapenzi naye huwa na taathira kubwa juu yake kuliko watu wengine wakiwemo hata wazazi wake wawili pamoja na mwalimu wake. Masahaba walimuuliza Bwana Mtume: Ni nani rafiki bora? Mtukufu huyo akasema:"Yule ambaye unapomwona hukukumbusha Mwenyezi Mungu, maneno yake huzidisha elimu yako na mwenendo wake unahuisha ukumbuko wako juu ya Kiyama". Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba ikiwa hatutojihadhari na kujichunga hapa duniani tutakwenda kujuta majuto makubwa Siku ya Kiyama huko akhera. Lakini majuto hayo hayatokuwa na tija wala faida yoyote kwa sababu haitokuwepo tena fursa yoyote ile. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kuiacha njia ya mitume ni dhulma; na kinyume chake kushikamana na njia ya wajumbe hao wa Allah ndiko kunakomdhaminia mja saada na uokovu. Aidha aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba mapenzi mawili hayawezi kukaa ndani ya moyo mmoja. Kumpenda Mtume na waja wema na kuwapenda marafiki waovu na wapotoshaji hakuwezi kuchanganyika pamoja. Kadhalika aya hizi zinatuelimisha kuwa marafiki wabaya wana matokeo mabaya na hatari kwa mtu. Marafiki wabaya na wapotofu ni mawakala wa shetani wafanyao kazi ya kumpotosha na kumpoteza mtu.
Darsa ya 625 inahitimishwa na aya ya 30 ambayo inasema:

وَقَالَ الرَّسُولُ يَا رَبِّ إِنَّ قَوْمِي اتَّخَذُوا هَذَا الْقُرْآنَ مَهْجُورًا

Na Mtume atasema (siku hiyo): Ee Mola wangu Mlezi! Hakika watu wangu waliifanya hii Qur'ani ni kihame.

Aya hii inaendelea kuzungumzia hali ya Siku ya Kiyama iliyoashiriwa katika aya zilizotangulia kwa kunukuu maneno ya Bwana Mtume Muhammad SAW atakayosema mbele ya Allah na kueleza kwamba, nabii huyo wa rehma ambaye alifanya kazi kubwa isiyo na mfano hapa duniani kwa ajili ya kuwaelekeza watu kwenye uongofu na kuwafikishia wahyi utokao kwa Mola wao, Siku ya Kiyama atashtakia kwa Mwenyezi Mungu kutokana na jinsi watu walivyokuwa wameipuuza Qur'ani.
Kushtakia huko hakutoishia kwa makafiri na washirikina wa zama za mtukufu huyo tu ambao hawakuwa tayari hata kuzisikiliza aya za Qur'ani; bali kutawajumuisha pia Waislamu ambao leo hii wanaisoma Qur'ani na kusikiliza qiraa na visomo vya maqarii wa kitabu hicho cha Allah, lakini katika maisha yao hawayatekelezi na wala hawayafanyii kazi maamrisho yaliyomo ndani ya kitabu hicho kitukufu. Kwa masikitiko, leo hii Waislamu wanashughulishwa zaidi na kuiandika Qur'ani kwa maandishi ya kuvutia zaidi na kuisoma kwa sauti za kupendeza zaidi kuliko kuzingatia na kuyafanyia kazi mafundisho yale aali na matukufu. Wanaiweka na kuihifadhi Qur'ani ndani ya majalada yenye marembo ya kuvutia na kuitunza kwa heshima na taadhima huku wakighafilika kwamba wanachotakiwa kufanya ni kukifungua kitabu hicho ili kiweze kuponya magonjwa na maradhi yanayozitesa roho na nafsi zao na kutatua mazonge na matatizo yanayozihangaisha jamii zao. Katika jamii mbalimbali, Qur'ani hupewa heshima na kutangulizwa mbele wakati wa hafla za aqdi na ufungaji ndoa, wakati wa watu kuhamia nyumba mpya, katika ufunguzi wa kiwanda na hata wakati watu wanapomwaga msafiri au kuwalaki mahujaji na mazuwari watokao kuzuru maeneo matakatifu ya kidini. Aidha mabango mbalimbali ya sanaa na kuta za majengo matukufu ya kidini ikiwemo misikiti hunakishiwa kwa aya tukufu za Qur'ani. Lakini si wale maarusi ambao baada ya kufunga ndoa yao huishi maisha yao kwa kufuata mafundisho ya Qur'ani, si kiwanda kinachofunguliwa ambacho kinapofanya kazi zake hufuata maamrisho na miongozo ya kiuchumi ya Uislamu na wala si wale wasanii wa nakshi na uchoraji wanaoshikamana na mafundisho ya dini hiyo. Naam, hivi ndivyo tulivyo. Leo hii Qur'ani imehamwa zaidi kuliko wakati mwengine wowote ule. Licha ya Waislamu kuwa na kanuni na sheria za maisha zilizo aali na tukufu zaidi na zilizokamilika zaidi, lakini wanaishi maisha yao katika hali ya kuendeshwa na kuburuzwa na madola ya kibeberu huku nchi zao zikiongozwa na kuendeshwa kwa kufuata sheria zinazokinzana na Uislamu. Na baya zaidi huku wakidhani kwamba kadiri watakavyofuata Umagharibi zaidi ndivyo watakavyoweza kupata maendeleo zaidi na kufikia kwenye saada zaidi. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba Bwana Mtume SAW atakuwa mmoja wa walalamikaji Siku ya Kiyama. Yeye ambaye tuna matumaini ya kupata shufaa na uombezi wake siku hiyo atalalamika dhidi yetu kwa sababu ya kuihama Qur'ani na kuacha kuyatekeleza na kuyafanyia kazi mafundisho yake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kuipuuza Qur'ani katika maisha yetu ya kila siku kutakwenda kutufanya tuulizwe na kuwajibishwa Siku ya Kiyama. Aidha aya hii inatutaka tuelewe kwamba kuisoma tu Qur'ani hakutoshi bali kuna ulazima wa kutadabari na kuzingatia aya zake na kuzifanyia kazi kwa kadiri ya uwezo wetu ili katiba na mwongozo huo wa maisha yetu usije ukawa kitu kilichohamwa. Kwa haya machache wapenzi wasikilizaji tunaifunga darsa yetu hii. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa miongoni mwa wabebaji wa kweli wa Qur'ani, wanaoisoma, wakaitafakari na kuifuata kivitendo katika maisha yao yote, amin.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)