Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatano, 25 Juni 2014 13:02

Sura ya Al Furqan, aya ya 21-26 (Darsa ya 624)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 624 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 25 ya Al Furqan. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 21 ambayo inasema:

وَقَالَ الَّذِينَ لا يَرْجُونَ لِقَاءَنَا لَوْلا أُنزِلَ عَلَيْنَا الْمَلائِكَةُ أَوْ نَرَى رَبَّنَا لَقَدِ اسْتَكْبَرُوا فِي أَنفُسِهِمْ وَعَتَوْ عُتُوًّا كَبِيرًا

Na walisema wale wasiotarajia kukutana Nasi: Mbona sisi hatuteremshiwi Malaika au hatumwoni Mola wetu Mlezi? Hakika wametakabari katika nafsi zao, na wamepanda kichwa vikubwa mno!

Katika darsa zilizopita tumewahi kueleza kwamba washirikina hawakuwa na burhani wala hoja yoyote ya maana ya kutoa kukabiliana na hoja za mantiki na za wazi kabisa za Mitume kuhusu tauhidi na maadi, yaani kufufuliwa viumbe, na badala yake wakawa wanatoa visingizio tu hivi na vile. Aya hii tuliyosoma inataja visingizio vyao viwili na kueleza kwamba watu hao walikuwa wakisema: kwa nini malaika wanawashukia Mitume tu? Kwa nini hawatushukii na sisi na kutufikishia kwa njia ya moja kwa moja ujumbe wa Mwenyezi Mungu? Na kwa nini hasa hatuwezi kumwona Mwenyezi Mungu ili tuweze kumwamini? Qur'ani tukufu inaujibu utoaji visingizio hivyo visivyo na msingi kwa kueleza kwamba watu hao wameathiriwa na kibri na kujikweza, na ndiyo maana wanakaidi na hawako tayari kuyakubali maneno ya haki. Ikiwa wanatoa visingizio hivyo, kwani yeye Mtume mwenyewe amemwona Mwenyezi Mungu kwa macho yake? Lakini ana imani thabiti juu ya Allah na anawalingania watu kumwabudu na kumtii Yeye Mola. Na kwani sharti la kuyaamini maneno ya Mwenyezi Mungu ni kuwaona malaika na kusikia maneno yao? Inatosha nyinyi kutumia akili zenu kwa kuona miujiza ya Mtume na kusikiliza maneno yake ili kuweza kutambua ukweli wa risala na utume wake. Ni kwa nini mnajitukuza na kujiona bora zaidi kushinda Mitume na kushikilia muwe na mawasiliano ya moja kwa moja na Mwenyezi Mungu na malaika wake? Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba kiburi na kujikweza humfanya mtu akanushe Kiyama na kufufuliwa. Aidha aya hii inatutaka tuelewe kuwa si vitu vyote vya kimaada vinaweza kutambulika kwa njia tano za hisi tulizonazo. Kwa kutoa mfano tu kuna aina kadhaa za nuru na miali kama miali ya urujuani kwa kimombo ultraviolet ambayo hatuwezi kuiona kwa macho yetu. Au hata kanuni kuu ya fizikia ya kani ya mvutano yaani force of gravity ni kitu ambacho hatuwezi kukitambua kwa njia ya hisi. Kama ni hivyo vipi baadhi ya watu wanataka kumwona Mwenyezi Mungu kwa macho yao ili uwe ndio uthibitisho wa kuweko kwake?
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya za 22, 23 na 24 ambazo zinasema:

يَوْمَ يَرَوْنَ الْمَلائِكَةَ لا بُشْرَى يَوْمَئِذٍ لِّلْمُجْرِمِينَ وَيَقُولُونَ حِجْرًا مَّحْجُورًا

Siku watakayowaona Malaika haitakuwa furaha siku hiyo kwa wakosefu. Na watasema: Kuwe na kizuizi kizuiacho!

وَقَدِمْنَا إِلَى مَا عَمِلُوا مِنْ عَمَلٍ فَجَعَلْنَاهُ هَبَاءً مَّنثُورًا

Na tutayaendea yale waliyoyatenda katika matendo, tuyafanye mavumbi yaliyotawanyika.

أَصْحَابُ الْجَنَّةِ يَوْمَئِذٍ خَيْرٌ مُّسْتَقَرًّا وَأَحْسَنُ مَقِيلا

Watu wa Peponi siku hiyo watakuwa katika makaazi bora na mahali penye starehe nzuri.

Kama tulivyoeleza, wapinzani wa Bwana Mtume walikuwa wakitarajia washuke malaika na kuwaona kwa macho yao ndipo waamini. Mwenyezi Mungu anasema: watu hao watawaona malaika Siku ya Kiyama, lakini hawatofurahia kuwaona kwao. Kwa sababu badala ya ahadi ya pepo malaika hao watawapa hakikisho watu hao la kupata adhabu ya moto. Matendo yao machafu na maovu waliyofanya hayatostahili malipo mengine ghairi ya adhabu ya moto, na mema yao yote waliyofanya yaliishia papa hapa duniani na wala hayatokuwa na faida na wao huko akhera. Kimsingi hasa ni kwamba amali itakayofika huko akhera na kuwa na faida ni ile aliyoifanya mtu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu tu. Amma amali ambayo haikufanywa kwa ikhlasi kamili au bila ya kuwa na nia yoyote kwa ajili ya Allah, hiyo itapotea na wala haitofika huko kwenye ulimwengu wa milele. Kisha aya zinaendelea kwa kulinganisha hali ya watu wa peponi na ile ya watu wa motoni na kueleza kwamba: watu wa peponi watakuwa katika hali bora kabisa na ya utulivu na kwenye amani kamili. Miongoni mwa yale tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kwamba ni jambo linaloyumkinika mwanadamu kuwaona malaika. Na kwa hivyo Siku ya Kiyama makundi yote mawili, yaani watu wa peponi na wale wa motoni, watawaona viumbe hao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa wale wanaofikiria juu ya dunia tu na kujipinda kwa ajili ya ulimwengu huu wa kupita, kama ambavyo viwiliwili vyao vitageuka udongo baada ya kufa, amali zao njema pia zitakuwa mithili ya vumbi ambalo kwa kupeperushwa na upepo hutoweka pasina kubakia athari yake yoyote. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba katika majuto ya Siku ya Kiyama ni kutoweka amali ambazo hazikufanywa kwa ikhlasi. Ni amali ambazo tuna matumaini nazo lakini kiuhakika ni mabua na makapi matupu.
Aya za 25 na 26 ndizo zinazotuhatimishia darsa yetu hii. Aya hizo zinasema:

وَيَوْمَ تَشَقَّقُ السَّمَاء بِالْغَمَامِ وَنُزِّلَ الْمَلائِكَةُ تَنزِيلا

Na siku zitakapopasuka mbingu kwa mawingu, na wateremshwe Malaika kwa wingi,

الْمُلْكُ يَوْمَئِذٍ الْحَقُّ لِلرَّحْمَنِ وَكَانَ يَوْمًا عَلَى الْكَافِرِينَ عَسِيرًا

Ufalme wa haki siku hiyo utakuwa wa Arrahman, Mwingi wa Rehema, na itakuwa siku ngumu kwa makafiri.

Aya hizi zinatilia mkazo kwa mara nyegine tena juu ya kuteremka malaika na kueleza kwamba wakati wa kukaribia Kiyama ambapo mfumo wa maumbile utasambaratika na kutokea miripuko mikubwa kila mahala ikiwemo katika sayari hii ya dunia na katika mwezi na jua, wingu zito kabisa litatanda mbinguni ambapo mbingu hizo zitapasuka na malaika kushuka kwa sura ya mtawalia. Wakati watu wote watakaposimamishwa katika uwanja wa kufufuliwa, watautambua barabaraba utawala na mamlaka mutlaki ya Allah jalla jalaluh juu ya kila kitu. Ni mamlaka na utawala thabiti na uliosimama juu ya msingi wa haki. Ni wazi kuwa katika mazingira kama hayo, makafiri na waovu watakuwa katika hali ngumu kabisa. Kwa sababu watasimamishwa mbele ya Mola wao ambaye walimkana katika umri na uhai wao wote na hawakuwa tayari kumkubali kuwa ni Mola wa haki; kwa hivyo siku hiyo watabaki mikono mitupu. Si wao wenyewe watakuwa na amali yoyote ya kuwafanya waokoke na si mahala ambapo watakuwa napo pa kukimbilia ili kusalimika na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba sayari na maumbo ya angani ambayo leo hii yanatembea kwa nidhamu kupitia njia maalumu yalizoainishiwa, wakati wa kukaribia Kiyama yatasambaratika kwa kuripuka na kupasukapasuka kwa irada ya Allah. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa mamlaka na utawala wa Mwenyezi Mungu juu ya ulimwengu ni wa hakika na wa kweli, si wa kujipangia tu na wala si wa kidhalimu. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba Siku ya Kiyama ni siku ya kudhihirikiwa waja na rehma za Allah isipokuwa wale ambao waliamua kwa hiyari yao kujinyima rehma hizo zisizo na ukomo kutokana na amali zao mbaya na ovu. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 624 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Mola atupe katika dunia hii mema, na akatupe huko akhera mema na atulinde na adhabu ya moto.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)