Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatano, 25 Juni 2014 12:58

Sura ya Al Furqan, aya ya 17-20 (Darsa ya 623)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 623 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 25 ya Al Furqan. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 17 na 18 ambazo zinasema:

وَيَوْمَ يَحْشُرُهُمْ وَمَا يَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّهِ فَيَقُولُ أَأَنتُمْ أَضْلَلْتُمْ عِبَادِي هَؤُلاء أَمْ هُمْ ضَلُّوا السَّبِيلَ

Na siku atakapowakusanya wao na wale wanaowaabudu badala ya Mwenyezi Mungu, na akasema: Je! Ni nyinyi mliowapoteza waja wangu hawa, au wao wenyewe walipotea njia?

قَالُوا سُبْحَانَكَ مَا كَانَ يَنبَغِي لَنَا أَن نَّتَّخِذَ مِن دُونِكَ مِنْ أَوْلِيَاء وَلَكِن مَّتَّعْتَهُمْ وَآبَاءَهُمْ حَتَّى نَسُوا الذِّكْرَ وَكَانُوا قَوْمًا بُورًا

Watasema: Subhanak, Umetakasika na upungufu! Haikutupasa sisi kuwafanya wasimamizi badala yako, lakini Wewe uliwastarehesha wao na baba zao hata wakasahau kukumbuka, na wakawa watu walioangamia.

Aya tulizosoma katika darsa iliyopita zilihusu adhabu na iqabu itakayowapata makafiri na malipo ya thawabu watakayolipwa waumini Siku ya Kiyama. Aya hizi tulizosoma zinasema: Katika kutoa hukumu kwa makafiri na washirikina, Mwenyezi Mungu atawaleta mbele ya mahakama yake ya uadilifu wale, wao na waliokuwa wakiabudiwa na watu hao wakiwemo majini, malaika na hata baadhi ya Mitume kama Nabii Issa (AS), na wakati pande mbili hizo zitakapokutanishwa pamoja atawauliza wale waliokuwa wakiabudiwa, je nyinyi mliwataka watu hawa wakuabuduni, au walijiamulia wao wenyewe kukuabuduni nyinyi?
Suali linalofanana na hili limeletwa katika aya ya 116 ya Suratul Maidah kuhusu Nabii Issa bin Maryam (AS) ambapo Allah SW anamuuliza Mtume wake huyo:"Je wewe uliwaambia watu nifanyeni mimi na mama yangu waola badala ya Mwenyezi Mungu?" Lakini jibu watakalotoa kwa Mwenyezi Mungu Siku ya Kiyama wale waliokuwa wakiabudiwa hapa duniani, ni jibu lenye kutoa mguso. Kwani waabudiwa hao watasema: Ewe Mola, sisi hatukumfanya mwengine kuwa msimamizi wetu ghairi yako wewe, sasa vipi tutake kutafuta watu wa kuwa wasaidizi wetu na kusimama dhidi yako? Kisha aya zinaendelea kwa kuashiria moja ya mambo yanayosababisha watu kupotoka na kueleza kuwa, kujaaliwa neema na atiya za kidunia, kama hakutoandamana na ushukurivu humfanya mtu aghafilike na asahau kumdhukuru na kumtaja Mwenyezi Mungu na kutumbukia kwenye lindi la madhambi. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba maabudu wote bandia Siku ya Kiyama, badala ya kuwaunga mkono washirikina, watawakana na kujiweka mbali nao. Funzo jengine tunalopata katika aya hizi ni kuwa Siku ya Kiyama vitu vyote yakiwemo masanamu yatakuwa na hisi za uelewa na yatasemezwa. Kadhalika aya hizi zinatuelimisha kwamba kujaaliwa kwetu kuwa na neema si kipimo cha kuonyesha kuwa sisi ni watu wazuri na tuyafanyayo ni ya sawa. Kwa sababu Mwenyezi Mungu hawanyimi neema zake hata makafiri na washirikina pia.
Ifuatayo sasa ni aya ya 19 ambayo inasema:

فَقَدْ كَذَّبُوكُم بِمَا تَقُولُونَ فَمَا تَسْتَطِيعُونَ صَرْفًا وَلا نَصْرًا وَمَن يَظْلِم مِّنكُمْ نُذِقْهُ عَذَابًا كَبِيرًا

Basi hakika wamekukadhibisheni kwa mliyoyasema. Kwa hiyo hamuwezi kujiondolea (adhabu) wala (kupata) wa kukusaidieni. Na atakayedhulumu miongoni mwenu tutamwonjesha adhabu kubwa.

Baada ya washirikina na wale waliokuwa wakiwaabudu kuhudhurishwa mbele ya mahakama ya Mwenyezi Mungu na kubainika kwamba sababu ya upotofu wa washirikina hao ni wao wenyewe na hao waliokuwa wakiwafanya maabudu na waola wao hawakuhusika kwa namna yoyote katika jambo hilo Allah SW atawaambia:"Nyinyi, ambao kule duniani mliwafanya hawa kuwa maabudu wenu kwa matumaini ya kukingwa na madhara na kupata manufaa kupitia wao leo mnajionea wenyewe kwamba wao hawana uwezo wa kukufanyieni chochote. Si adhabu ambayo wanaweza kukulindeni nayo, na wala si manufaa yoyote wanayoweza kukunufaisheni. Nyinyi mmefanya dhulma kubwa kabisa, ambayo ni shirki. Mmezidhulumu nafsi zenu na vilevile mmewafanyia dhulma mitume waliokuja kukuonyesheni uongofu pamoja na vitabu vya mbinguni walivyokuja navyo; na malipo ya dhulma ni adhabu kali ya moto. Miongoni mwa mafunzo ya kuzingatiwa katika aya hii ni kwamba wale ambao hapa duniani walighariki kwenye dimbwi la shirki na dhulma Siku ya Kiyama hawatoweza kupata msaada wa aina yoyote na wala hawatoweza kufanya lolote ili kuziokoa nafsi zao. Funzo jengine la kuzingatiwa katika aya hii ni kuwa katika utamaduni wa dini, maana ya dhulma ni pana zaidi ya dhulma ya mtu mmoja kumfanyia mwengine; ambapo katika hatua yake ya kwanza dhulma hiyo inajumuisha mtu kujidhulumu nafsi yake mwenyewe. Isitoshe shirki ni miongoni mwa vielelezo vya wazi kabisa vya dhulma; na mushrik ni mtu dhaalimu.
Tunaihatimisha darsa yetu hii kwa aya ya 20 ambayo inasema:

وَمَا أَرْسَلْنَا قَبْلَكَ مِنَ الْمُرْسَلِينَ إِلاَّ إِنَّهُمْ لَيَأْكُلُونَ الطَّعَامَ وَيَمْشُونَ فِي الأَسْوَاقِ وَجَعَلْنَا بَعْضَكُمْ لِبَعْضٍ فِتْنَةً أَتَصْبِرُونَ وَكَانَ رَبُّكَ بَصِيرًا

Na hatukuwatuma kabla yako Mitume wowote ila kwa hakika na yakini walikuwa wakila chakula, na wakitembea masokoni. Na tumewajaalia baadhi yenu wawe mtihani kwa wengine; Je! Mtakuwa na subira? Na Mola wako Mlezi ni Mwenye kuona.

Moja ya visingizio vilivyokuwa vikitolewa na makafiri, na ambacho kiliashiriwa katika aya ya saba ya sura hii kilikuwa ni hali ya Bwana Mtume kuwa kiumbe wa kawaida na kuishi maisha kama ya watu wa kawaida; ambapo watu hao walikuwa wakimwambia mtukufu huyo:"Wewe ni Mtume gani ambaye kama tulivyo sisi unahitajia chakula na maji, na kama walivyo watu wengine unaamua wewe mwenyewe kwenda sokoni, na wala huna mtumwa na mtumishi wa kukutumikia!?" Ni kwamba wao walitarajia kuwa mtume wa Allah anapasa awe malaika aliye tofauti na watu, ambaye hahitajii maji wala chakula; na au kama atakuwa mtu basi lazima awe mithili ya wafalme na watawala, ambao chini yao kuna wanaume na wanawake wanaowatumikia na kuwafanyia kazi zao za binafsi. Kwa hakika kile ambacho kwa mtazamo wao wao ni nukta ya ila na udhaifu kwa Bwana Mtume, ilikuwa ndiyo nukta ya ukamilifu kwa mtukufu huyo; kwa sababu katika zama zote za historia, Mitume wote walikuwa wakiishi pamoja na watu; na wakichanganyika na kulahikiana nao; na kazi ya kufikisha na kubainisha maamrisho ya Mwenyezi Mungu kwa watu waliifanya ndani ya jamii zao. Mitume walikuwa walimu na walezi wenye kuwaonea uchungu na huruma watu, ambao walikuwa wakitoka wao wenyewe kuwafuata wanafunzi wao, na si kutawa majumbani na misikitini ili kuwasubiri watu wawafuate wao; au waamue kuteua kikundi fulani tu cha watu wateule na wenye vipawa na kuwafanya wanafunzi wao na kutowajali watu walio wengi katika jamii. Tab'an huko kuwa kwao Mitume waja wasio na makuu na kuishi kwao maisha kama ya watu wa kawaida, wenyewe ulikuwa mtihani wa kujaribiwa watu. Kwa sababu kwa kutumia kisingizio hicho hicho, baadhi ya watu hawakuwa tayari kuwaamini na kuukubali wito wa haki na uongofu waliowafikishia. Na hasa pale ilipotokea Mtume kuwa na uwezo wa chini kwa mali na utajiri kulinganisha na wao. Kisha aya inaendelea kwa kuashiria ugumu wa jambo hilo na kuuliza:"Je mko tayari kuyakubali maneno ya haki na kushikamana nayo? Je mko tayari kudhibiti hawaa na matamanio yenu na kuyasikiliza maneno ya mtu ambaye kiuwezo ana hali ya chini kulinganisha na nyinyi, lakini anayoyasema ni ya haki? Na kwa kumalizia aya inawatanabahisha watu kuwa yote muyasemayo na muyatendayo Allah SW anayajua na hakuna chochote kinachoweza kufichika kwake. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba Mitume wote wa Mwenyezi Mungu walikuwa na lengo moja katika kufikisha na kueneza wito wa dini ya tauhidi. Hakuna shaka kuwa waumini wanaliwazika na kufarajika kwa kusoma na kutalii historia na yaliyojiri katika maisha yao. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kuwa lengo la mitihani ya Allah ni kumlea na kumjenga mja; na subira na uvumilivu ndio siri ya kufaulu na kufuzu mithani hiyo. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 623 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Mola azifanye thabiti imani zetu, atutakabalie amali zetu na aufanye mwema mwisho wetu.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)