Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 22 Juni 2014 21:44

Sura ya Al Furqan, aya ya 10-16 (Darsa ya 622)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 622 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 25 ya Al Furqan. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 10 ambayo inasema:

تَبَارَكَ الَّذِي إِن شَاء جَعَلَ لَكَ خَيْرًا مِّن ذَلِكَ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الأَنْهَارُ وَيَجْعَل لَّكَ قُصُورًا

Ametukuka Yule ambaye akitaka atakujaalia yaliyo bora kuliko hayo, nayo ni mabustani yapitayo mito chini yake, na atakujaalia makasri.

Katika darsa iliyopita tulisema kuwa wapinzani wa Bwana Mtume walikuwa kila mara wakitafuta visingizio vikiwemo vya kumwambia mtukufu huyo kwamba kama wewe ni Mtume mbona huna kasri wala bustani yoyote? Kwa nini huna mtumwa na mtumishi wa kushughulika kukutafutia chakula mpaka unalazimika wewe mwenyewe kwenda sokoni? Hivyo aya hii tuliyosoma inatoa jibu kwa matarajio hayo hewa kwa kusema: Lau kama Mwenyezi Mungu angalitaka angaliweza kumpa Mtume wake yaliyo bora zaidi ya hayo mnayoyatasawari nyinyi. Na si bustani moja tu bali mabustani kadha wa kadha ya kijani kibichi yaliyonawiri na makasri ya fahari na yenye kuvutia, lakini Mitume hawakupangiwa kuishi maisha kama ya wafalme na kuwaweka watu chini ya t'aa na amri zao. Madhumuni ya kuja Mitume ni kuwaelimisha na kuwaonyesha watu uongofu; na wao watu kuamua kwa irada na hiyari yao wenyewe kufuata mafundisho yao. Isitoshe ni kwamba kuwa na mali na utajiri mkubwa kutawafanya baadhi ya watu wawafuate Mitume kwa sababu ya kupata manufaa yao ya kidunia tu. Hali ya kuwa lengo la kutumwa Mitume ni kuwakomboa na kuwatoa watu kwenye utumwa wa kuikumbatia na kuipaparikia dunia. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba Mitume wa Allah kama walivyokuwa watu wengine wa kawaida walikuwa wakiishi maisha yasiyo na makuu wala mambo yoyote ya kifahari. Na hiyo ni moja ya sifa zao maalumu ambayo wafanya tablighi wote wa dini wanatakiwa kuifanya kuwa mwenendo wa kuiga na kufuata katika maisha yao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa suala muhimu kwa mja ni kutii amri za Allah SW, awe mtu ni fakiri asiye na chochote au tajiri aliyejaaliwa kuwa na mali chungu nzima.
Tunaendelea na darsa yetu kwa kuitegea sikio aya ya 11 na 12 ambazo zinasema:

بَلْ كَذَّبُوا بِالسَّاعَةِ وَأَعْتَدْنَا لِمَن كَذَّبَ بِالسَّاعَةِ سَعِيرًا

Bali wameikanusha Saa (ya Kiyama). Na (Sisi) tumemuandalia Moto mkali kabisa (huyo) mwenye kuikanusha Saa.

إِذَا رَأَتْهُم مِّن مَّكَانٍ بَعِيدٍ سَمِعُوا لَهَا تَغَيُّظًا وَزَفِيرًا

Ule Moto utakapowaona tangu mahali pa mbali watasikia hasira yake na mngurumo wake.

Aya zilizopita ziliashiria itikadi potofu za washirikina juu ya Mwenyezi Mungu na matarajio yasiyo na msingi waliyokuwa nayo kwa Bwana Mtume. Aya hizi zinaashiria upotofu wa washirikina hao katika itikadi na imani yao kuhusu maadi na kufufuliwa viumbe na kueleza kwamba wao, si wakadhibishaji wa Tauhidi na Utume tu, bali wanakikana Kiyama pia na wala hawauamini wowote ule katika usuli na misingi ya dini za mbinguni. Na kimsingi hasa ni kwamba chimbuko la visingizio vyao vyote ni kukadhibisha Kiyama. Lakini hakuna shaka yoyote kwamba ukanushaji na ukadhibishaji wao huo hautokuwa wa milele bali siku itafika ambapo ukweli wa hilo utawathibitikia kwa uwazi kabisa. Ni siku ambayo macheche yanayorindima na kuchemka kwa ghadhabu ya moto wa Jahanamu yatakayopowaandama, yakawazunguka na kuwafunika kutokea kila upande. Siku hiyo hakutakuwapo tena ufanyaji kejeli, stihzai wala utoaji visingizio hivi na vile. Wale ambao hawakutaka kutumia mantiki na akili waliyopewa na kwa sababu ya ghururi na kiburi wakawa hawako tayari kuikubali haki hatima na maskani yao yatakuwa kwenye moto wa Jahanamu, na hiyo ni adhabu ya kiadilifu kabisa ya Mola kwa watu wa aina hiyo. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kukadhibisha maadi humfungulia njia mtu ya kufanya kila mambo maovu na machafu na kumulekeza kwenye hilaki ya adhabu ya moto. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa hapa duniani, makafiri wanawatolea vitisho, kuwadhalilisha na kuwafanyia stihzai waumini; lakini Siku Kiyama watajibiwa nao kwa vitisho na udhalilishaji wakati watakapokuwa wanaingizwa kwenye moto wa Jahanamu.
Zifuatazo sasa ni aya za 13 na 14 ambazo zinasema:

وَإِذَا أُلْقُوا مِنْهَا مَكَانًا ضَيِّقًا مُقَرَّنِينَ دَعَوْا هُنَالِكَ ثُبُورًا

Na watakapotupwa humo mahali palipo finyu, hali wamefungwa, ndipo hapo wataomba mauti.

لا تَدْعُوا الْيَوْمَ ثُبُورًا وَاحِدًا وَادْعُوا ثُبُورًا كَثِيرًا

(Waambiwe) Msiyaombe mauti mara moja tu, bali ombeni mauti mara nyingi!

Aya hizi wapenzi wasikilizaji zinatoa picha na taswira ya jinsi watu wa motoni watakavyokuwa wanahiliki na kuteseka na adhabu ya moto kiasi cha kumfanya kila mtu muumini akae ataamali na kutafakari kwamba asije akafikwa na hatima kama hiyo, ambapo badala ya kufaidika na rehma zisizo na mpaka za Allah Mwingi wa rehma akaja akapatwa na ghadhabu zake Mola; Mola ambaye huwaangalia muda wote waja wake kwa jicho la rehma na hata kutoa fursa kwa waliomwasi ya kutubia na kufanya mema kufidia mabaya waliyoyatanguliza. Walifanya nini waja hao hata wakastahiki adhabu kama hiyo? Kuna jegine ghairi ya kwamba kutokana na amali na matendo yao maovu, wamejiandalia kwa mikono yao wenyewe moto huo mkali wenye kuhilikisha kwa namna isiyomithilika? Kwa mujibu wa aya na hadithi, motoni ni mahali penye uenevu mkubwa mno, lakini watu wa motoni watakuwa muda wote wanahisi wamebanwa na wako kwenye hali ya tabu na dhiki. Mfano wake ni kama ulivyo ukuta mkubwa ambao mtu anapigilia msumari juu yake; kwani japokuwa ukuta huo ni mkubwa lakini sehemu ulipopigiliwa msumari pana mbano unaouweka muda wote msumari huo katika hali ya mbinyo na mgandamizo. Hali ya watu wa motoni ni nzito mno, ya mateso na isiyoweza kuvumilika kiasi cha kuwafanya muda wote watamani kufikwa na mauti. Lakini kutamani huko kutakuwa na faida na tija gani wakati huko akhera hakuna mauti! Na kadiri mtu atakavyoungua hatokufa, bali badala yake atatiwa ngozi, nyama na mifupa upya ili aweze kuendelea muda wote kuyahisi machungu na mateso ya adhabu. Baadhi ya mafunzo ya kuzingatiwa katika aya hizi ni kwamba maadi yatakuwa ya sura ya kiwiliwili na si kiroho tu. Funzo jengine la kuzingatiwa katika aya hizi ni kuwa watu wa motoni hawatoingia motoni kwa miguu yao, bali watarembewa na kuvurumizwa humo kwa namna ya udhalilishaji. Kadhalika aya hizi zinatuelimisha kwamba watu wa motoni watafungwa kwenye makongomeo na minyororo na watakuwa katika hali ya mbano na mbinyo. Watapiga makelele na mayowe na kulia kwa sauti ya juu, lakini hakuna wa kuwaitikia kilio chao na hakutokuwa na lolote watakaloweza kufanya.
Tunaihatimisha darsa yetu hii kwa aya za 15 na 16 ambazo zinasema:

قُلْ أَذَلِكَ خَيْرٌ أَمْ جَنَّةُ الْخُلْدِ الَّتِي وُعِدَ الْمُتَّقُونَ كَانَتْ لَهُمْ جَزَاء وَمَصِيرًا

Sema: Je! Hayo ni bora au Pepo ya milele, ambayo wameahidiwa wachamngu, iwe kwao malipo na marejeo?

لَهُمْ فِيهَا مَا يَشَاؤُونَ خَالِدِينَ كَانَ عَلَى رَبِّكَ وَعْدًا مَسْؤُولا

Watayapata humo wayatakayo wakae humo milele. Hii ni ahadi juu ya Mola wako Mlezi, inayoombwa.

Ulinganishaji wa hatima ya waumini na ile ya makafiri ni miongoni mwa njia ambazo Allah SW amezitumia katika aya nyingi za Qur'ani na kumwambia Mtume wake awatake watu watafakari wao wenyewe na kuchagua njia ya kufuata kwa kulinganisha hatima ya watu wa motoni na ya wale watakaoingia peponi. Kama wanachotafuta ni neema na maisha ya raha ya kweli basi upeo wa uoni wao usiishie katika kuikodolea macho dunia tu na kujipinda kwa ajili ya dunia hii ya kupita; bali wafikirie pia akhera na wajitahidi na kujipinda kwa ajili ya maisha yao ya milele ili watakapofumba jicho badala ya nyumba ya raha na neema wasije wakahamishiwa kwenye nyumba ya mateso na hilaki na kuishia kwenye majuto ya milele. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba tunapochagua kukufuru au kuamini na kufanya jambo jema au baya tufikiri hatima na mwisho wake; nao ni je tunaitaka Pepo au tunaridhia kwenda kuishi motoni?! Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa mwanadamu ataweza kupata yale yote anayoyatamani atakapokuweko peponi, kwani akila akitakacho kitakuweko humo. Amma wale watakaokuweko motoni hawatoweza kupata chochote watakachokitarajia. Na Aidha aya hizi zinatutaka tufahamu kwamba Mwenyezi Mungu amedhamini kutekeleza yale aliyoyaahidi. Ahadi za Allah SW ni za hakika, hazina shaka na utekelezaji wake ni wa kudumu. Wapenzi wasikilizaji darsa ya 622 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Mola aturehemu kwa kutuingiza katika Pepo yake ya milele na atulinde na adhabu ya moto. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)