Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatano, 28 Mei 2014 12:32

Sura ya Al Furqan, aya ya 4-9 (Darsa ya 621)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 621 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 25 ya Al Furqan. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya nne ambayo inasema:

وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا إِنْ هَذَا إِلاَّ إِفْكٌ افْتَرَاهُ وَأَعَانَهُ عَلَيْهِ قَوْمٌ آخَرُونَ فَقَدْ جَاؤُوا ظُلْمًا وَزُورًا

Na wamesema waliokufuru: Haya si chochote ila ni uzushi aliouzua, na wamemsaidia kwa haya watu wengine! Hakika hawa wamekuja na dhulma na uzushi.

Katika zama zote za historia, moja ya mbinu ambazo zimekuwa zikitumiwa na makafiri ni kuzusha tuhuma dhidi ya Mitume na kuzitia doa shakhsia za waja hao wateule. Watu hao walikuwa wakidai kwamba Mitume ni watu wazushi na waongo ambao wanadai wametumwa na Mwenyezi Mungu ili kuweza kujipatia hadhi na utukufu wa kidunia, na kwamba yale wanayodai kuwa ni vitabu vya mbinguni walivyokuja navyo kwa ajili ya watu wameviandika wao wenyewe kwa msaada wa vikundi vya watu. Na kwamba eti watu hao wamewasaidia wao katika jambo hilo ili waweze kuwa na nguvu za madaraka na mamlaka na kushirikiana nao ili na wao pia waweze kufanikisha matakwa, malengo na tamaa zao.

Hakika ya maneno yao hayo ni uongo mkubwa na tuhuma nzito dhidi ya watu safi zaidi na wakweli zaidi kati ya watu wote wa zama zao. Na ukweli ni kwamba wapinzani wa haki hawana jibu la maana la kutoa kukabiliana na hoja wadhiha na za wazi kabisa za Mitume na vitabu vya mbinguni walivyokuja navyo. Katika zama za Bwana Mtume Muhammad SAW, badala ya watu hao kujenga hoja na kujadiliana kielimu, walichokuwa wakifanya ni kuchafua shakhsia ya mtukufu huyo, na pasina kuwa na hoja na ushahidi wowote wakawa wanamtuhumu kuwa kitabu cha Qur'ani amekitunga yeye mwenyewe kwa msaada wa rafiki zake na kumnasibishia Mwenyezi Mungu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba ili kuhalalisha ukafiri wao, makafiri walikuwa wakimzushia tuhuma Bwana Mtume kuwa ni muongo, na kushindwa kutoa hoja na burhani yoyote ya kuzipinga aya za Qur'ani. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa udhalilishaji, uzushaji tuhuma na kuhadaa watu ndizo mbinu za kila siku ambazo wapinzani huzitumia kwa lengo la kutaka kuzuia wito wa haki wa Mitume usienee.

Ifuatayo sasa ni aya ya tano na ya sita ambazo zinasema:

وَقَالُوا أَسَاطِيرُ الأَوَّلِينَ اكْتَتَبَهَا فَهِيَ تُمْلَى عَلَيْهِ بُكْرَةً وَأَصِيلا

Na wakasema: Hizi ni ngano za watu wa kale alizoziandikisha, anazosomewa asubuhi na jioni.

قُلْ أَنزَلَهُ الَّذِي يَعْلَمُ السِّرَّ فِي السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ إِنَّهُ كَانَ غَفُورًا رَّحِيمًا

Sema: Ameiteremsha (hii) ajuaye siri za mbinguni na ardhini. Hakika Yeye ni Mwenye kughufiria, Mwenye kurehemu.

Aya ya tano ya sura hii inaendelea na maudhui iliyozungumziwa na aya iliyotangulia kwa kutaja tuhuma nyengine ya wapinzani wa haki na kueleza kwamba watu hao ambao hawana hoja yoyote ya kutoa kukabiliana na mantiki imara ya Qur'ani, wakati mwengine huwa wanasema: visa vilivyosimuliwa ndani ya Qur'ani ni zile zile ngano zilizotajwa katika vitabu vilivyopita, na yeye Muhammad amenukuu kutoka kwenye vitabu hivyo na kuwasomea watu kwamba ni aya za Mwenyezi Mungu. Ukweli ni kuwa yeye mwenyewe hana alichonacho, bali kila asemalo ni maandiko ya watu wengine, anayoyasoma kwa ajili ya kudaia Utume.

Kwa tuhuma zao hicho chafu, wapinzani wa haki walikuwa wakidai na kutaka kuonyesha kwamba Bwana Mtume Muhammad SAW ni mtu aliyekuwa akijua kusoma na kuandika na kwamba si kweli kama inavyoelezwa ndani ya Qur'ani kuwa yeye ni mtu ummiyyi ambaye hakujifunza mahala kusoma na kuandika. Bali yeye amevisoma vitabu vya waliotangulia, na watu wanaomsaidia katika kazi hiyo wamekuwa wakimsomea yaliyomo ndani ya vitabu hivyo kisha yeye anayaandika na kuwapatia watu kwa jina la Qur'ani! Walikuwa wakizua uongo huo hali ya kuwa kwanza ni kwamba katika mji wa Makka, watu waliokuwa wakijua kusoma na kuandika walikuwa wachache mno. Na watu wote walikuwa wakijua kwamba Bwana Mtume Muhammad SAW hakujifunza kusoma na kuandika kwa mtu yeyote yule na wala hakuwa na mawasiliano yoyote na Mayahudi wa Madina na Ahlul Kitab wengine hata awaombe msaada na kuandika kitabu kiitwacho Qur'ani. Isitoshe ni kwamba ni sehemu tu ya Qur'ani ndiyo inayohusu visa vya kaumu zilizopita. Lakini sehemu kubwa ya yaliyomo ndani ya kitabu hicho cha mbinguni inahusu mafundisho ya kiitikadi, hukumu za kivitendo au maamrisho ya kiakhlaqi ambayo mengi yao hayakuwepo asilani katika utamaduni wa zama za kudhihiri Bwana Mtume wala ndani ya vitabu vya mbinguni vilivyokuwepo katika zama hizo. Na kwa hiyo katika kuwajibu watu hao kwa tuhuma zao hizo zisizo na msingi, Allah SW anasema: aya za Qur'ani hazitokani na fikra ya mwanadamu yeyote, bali zinatokana na elimu mutlaki ya Mwenyezi Mungu ambaye si mjuzi wa ya dhahiri tu ya mbinguni na ardhini, bali Yeye ni mwelewa na mwenye habari ya siri za maumbile pamoja na habari za yaliyopita na yajayo katika mbingu na ardhi ambayo nyinyi hamna elimu nayo; na baadhi ya hayo yametajwa ndani ya hiyo hiyo Qur'ani. Na tab'an ikiwa wapinzani wataacha ubishani na ukaidi wao na kuikubali haki na ukweli watanufaika na rehma na uraufu wake Mola, na Yeye Allah atawaghufiria na kuwasamehe. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba chimbuko la Qur'ani ni elimu mutlaki na isiyo na ukomo ya Allah SW, na kitabu hicho kinatoka kwa yule aliye mjuzi wa siri zote za ulimwengu. Kwa hivyo si kitabu kilichotungwa na mwanadamu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa mlango wa toba uko wazi kwa watu wote, hata kwa makafiri wanaoitusi Qur'ani kwa kuiita kuwa ni hekaya na ngano, na wanaomvunjia heshima Bwana Mtume kwa kumwita muongo.

Darsa yetu ya leo inahatimishwa na aya za saba, nane na tisa ambazo zinasema:

وَقَالُوا مَالِ هَذَا الرَّسُولِ يَأْكُلُ الطَّعَامَ وَيَمْشِي فِي الأَسْوَاقِ لَوْلا أُنزِلَ إِلَيْهِ مَلَكٌ فَيَكُونَ مَعَهُ نَذِيرًا

Na wakasema: Ana nini Mtume huyu? Anakula chakula, na anatembea masokoni! Mbona hakuteremshiwa Malaika akawa mwonyaji pamoja naye?

أَوْ يُلْقَى إِلَيْهِ كَنزٌ أَوْ تَكُونُ لَهُ جَنَّةٌ يَأْكُلُ مِنْهَا وَقَالَ الظَّالِمُونَ إِن تَتَّبِعُونَ إِلاَّ رَجُلا مَّسْحُورًا

Au akaangushiwa khazina, au akawa na bustani ale katika hiyo? Wakasema madhaalimu: Nyinyi hamumfuati ila mtu aliyerogwa.

انظُرْ كَيْفَ ضَرَبُوا لَكَ الأَمْثَالَ فَضَلُّوا فَلا يَسْتَطِيعُونَ سَبِيلا

Tazama jinsi wanavyokupigia mifano. Basi wamepotea, wala hawataweza (kuishika) Njia.

Aya zilizotangulia zilizungumzia tuhuma chafu za makafiri dhidi ya Bwana Mtume Muhammad SAW. Aya hizi zinaashiria matarajio yasiyo na msingi wala maana yoyote ya watu hao na kueleza kwamba wao walikuwa wakimwambia Bwana Mtume kuwa hailaiki hata kidogo kwa mtu aliyebaathiwa na kufanywa Mtume na Mwenyezi Mungu kuwa sawa na wanadamu wa kawaida  na hivyo akahitajia chakula; na ili kukipata, akalazimika kwenda sokoni. Inapasa yeye awe na mali na utajiri wa kiasi cha kuwashangaza watu na kuwatia bumbuazi, na muda wote aweko pamoja naye malaika ambaye watu watamwona ndipo watayakubali maneno yake. Baadhi ya wapinzani wa nabii huyo wa rehma hawakutosheka na hayo, bali walifika mbali zaidi hata kumwita Bwana Mtume majinuni aliyeathiriwa na uchawi na marogo na kuondokewa na hali ya kawaida ya mtu. Mwenyezi Mungu Mtukufu akayajibu maneno hayo yasiyo na msingi yaliyoropokwa na wapinzani hao wa haki kwa kusema: Watu hao wamekosea kwa kuwafananisha Mitume na wafalme; kwani kama ambavyo wafalme wanaishi na kupitisha muda wao ndani ya makasri yao ya fahari na kwenye mabustani yao yaliyonawiri na wala hawainui mguu wao kwenda sokoni wala kuchanganyika na watu, wanawatarajia Mitume pia wawe vivyo hivyo. Hali ya kuwa kazi ya Manabii ni kuwaongoza na kuwaelekeza watu kwenye uongofu, si kujilimbikizia mali na utajiri au kutaka mamlaka na madaraka! Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba viongozi wa dini wanatakiwa wachanganyike na wawe pamoja na watu na wala wasijitenge nao ndipo wataweza kufanikiwa katika suala la tablighi na uelimishaji wa jamii. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kuwa mwanadamu ni jambo la ukamilifu kwa Mitume, kwani malaika hawawezi kuifanya kazi ya waja hao wateule wa Allah. Kwa haya machache wapenzi wasikilizaji tunaifunga darsa yetu hii. Tunamwomba Mola atujaalie kuwa watiifu kwa maamrisho yake na wenye kujiepusha na makatazo yake. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)