Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatano, 28 Mei 2014 12:28

Sura ya Al Furqan, aya ya 1-3 (Darsa ya 620)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Baada ya kukamilisha tarjumi na maelezo ya sura ya 24 ya Annur, darsa hii ya 620 itaanza kuzungumzia sura ya 25 ya Al Furqan. Sura hii iliteremshwa Makka na ina jumla ya aya 77, na Furqan ni moja ya majina ya Qur'ani yenyewe yenye maana ya kipambanuzi baina ya haki na batili.

Tunaianza darsa yetu hii kwa aya ya kwanza ya sura hiyo ambayo inasema:

تَبَارَكَ الَّذِي نَزَّلَ الْفُرْقَانَ عَلَى عَبْدِهِ لِيَكُونَ لِلْعَالَمِينَ نَذِيرًا

Ametukuka aliyeteremsha Furqani kwa mja wake, ili awe mwonyaji kwa walimwengu wote.

Ujudi uliotukuka na wenye baraka ni ule ambao daima huwa chimbuko la heri; na manufaa yake kwa wengine huwa hayamaliziki na wala hayana mwisho. Qur'ani ni kitabu kinachotoka kwa Mwenyezi Mungu alichoteremshiwa Bwana Mtume Muhammad SAW, lakini manufaa na kheri zake zinawafikia waja mpaka Siku ya Kiyama, na kila atakaye anaweza kunufaika na uongofu wa kitabu hicho kitukufu. Na kuna baraka kubwa zaidi zinazotoka kwenye kitabu hiki cha mbinguni kuliko zile za kuutoa kwenye giza totoro la upotofu umati mkubwa wa wanadamu katika zama zote za historia tangu ilipoteremshwa Qur'ani yenyewe?

Kupambanua baina ya haki na batili ni kazi ngumu mno, kwa sababu kwa upande mmoja maarifa ya mwanadamu yana mpaka na kikomo katika kulijua la sahihi na lisilo sahihi; na kwa upande mwengine matashi ya batini na matarajio ya nje ya nafsi humuelekeza mtu kwenye upotofu au kumweka katika hali ya fadhaa na kutangatanga. Lakini Qur'ani tukufu ambayo imeteremshwa kwa msingi wa elimu mutlaki ya Allah SW na kufikishiwa wanadamu, imepambanua ya haki na ya batili katika masuala tofauti ya maisha na kumuelekeza mwanadamu katika namna ya kufahamu la sahihi na lisilo sahihi.

Kutokana na kitabu hicho hicho cha uongofu, Bwana Mtume Muhammad SAW naye pia anawatanabahisha watu na hatari ya kujiweka mbali na haki na kuwapa indhari juu kukubali rai na fikra batili na kufanya mambo ya upotofu. Onyo alilotoa mtukufu huyo haliwahusu watu wa zama zake tu, bali wito wake unawalenga watu wote wa kila kizazi na rangi, na wa kila mahala na zama. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba Qur'ani ni kitabu kilichobarikiwa ambacho kimeteremshwa kutoka kwenye chemchemi yenye baraka. Funzo jengine tunalopata katika aya hii ni kuwa aya za Qur'ani tukufu ndio wenzo bora kabisa wa kumwezesha mtu kutambua la sahihi na lisilo sahihi katika mambo tofauti. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba risala na ujumbe wa Nabii Muhammad SAW ni wa ulimwengu mzima na wala hauwahusu watu wa kabila, zama na mahali maalumu.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya pili ya sura yetu ya al Furqan ambayo inasema:

الَّذِي لَهُ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ وَلَمْ يَتَّخِذْ وَلَدًا وَلَمْ يَكُن لَّهُ شَرِيكٌ فِي الْمُلْكِ وَخَلَقَ كُلَّ شَيْءٍ فَقَدَّرَهُ تَقْدِيرًا

Ambaye ni wake ufalme wa mbingu na ardhi, wala hakujifanyia mwana, wala hakuwa na mshirika katika ufalme, na akaumba kila kitu na akakikadiria kwa kipimo.

Baada ya aya iliyotangulia ambayo imeashiria neema kubwa kabisa ya Allah SW na kubainisha nafasi ya Qur'ani na Bwana Mtume katika kuwaongoza wanadamu, aya hii inamkumbusha mwanadamu neema ya uumbwaji wa ulimwengu wa maumbile na tadbiri na uendeshaji mambo yake unaofanywa na Mola Muumba pekee wa vyote hivyo na kueleza kwamba Mungu ambaye amekuwekeeni mfumo wa sheria ndiye huyo huyo aliyeukadiria na kuutandika mfumo wa uumbaji kwa namna bora kabisa; na baina ya viwili hivyo kuna uwiyano na uratibu uliokamilika. Mwenyezi Mungu Tabaaraka wa Taala si Muumba tu, bali pia ni mtawala wa mfumo mzima wa uumbaji, na hakuna yeyote aliyekuwa au aliye mshirika wake kwa namna yoyote ile. Hakuna kitu chochote kilichoko nje ya mipaka ya mamlaka yake, bali mbingu na ardhi pamoja na viumbe na mahuluku wote muda wote wako chini ya ulezi wake. Yeye Allah ni Mkwasi na asiyehitaji chochote, hakuna aliye mfano wake wala anayefanana naye hata ahitajie mke na mwana. Kwa sababu kimsingi mtu huwa na haja ya mtoto kufidia kasoro na upungufu alionao; hivyo yule ambaye ni mmiliki na mtawala wa ulimwengu wote wa maumbile na kila kilichomo ndani yake si mpungukiwa wa chochote. Na hata Mitume pia, licha ya adhama na daraja walizonazo, nao pia ni viumbe wa Allah, na kuwaita wao wana wa Mungu ni unasibishaji mbaya kabisa na usiostahiki. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba katika ulimwengu mzima wa maumbile kuna mfumo mmoja, irada moja na uendeshaji wa mtawala mmoja tu; na utawala na uendeshaji wa ulimwengu mzima ni wa Allah SW pekee. Funzo jengine tunalopata katika aya hii ni kuwa viumbe vyote vimeumbwa na Muumba mmoja na Yeye ndiye muendeshaji wa mambo yao yote. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba mfumo wa ulimwengu wa maumbile si mfumo uliotokea kwa bahati na kwa sadfa tu, bali umetokana na mipango na vipimo makini kabisa; na kanuni zinazotawala juu yake zinafuata mahisabu na nidhamu iliyokamilika.

Tunaihatimisha darsa yetu hii kwa aya ya tatu ambayo inasema:

وَاتَّخَذُوا مِن دُونِهِ آلِهَةً لّا يَخْلُقُونَ شَيْئًا وَهُمْ يُخْلَقُونَ وَلا يَمْلِكُونَ لِأَنفُسِهِمْ ضَرًّا وَلا نَفْعًا وَلا يَمْلِكُونَ مَوْتًا وَلا حَيَاةً وَلا نُشُورًا

Na wamefanya badala yake miungu ambayo haiumbi chochote, bali hiyo inaumbwa, haijimilikii nafsi zao madhara wala manufaa, wala haimiliki mauti, wala uhai, wala ufufuo.

Baada ya sisitizo lililotolewa katika aya iliyotangulia kuhusu kuwa na Muumba na Mtawala mmoja tu ulimwengu mzima wa maumbile aya hii inaashiria mtazamo walionao washirikina juu ya Mwenyezi Mungu na kueleza kwamba watu hao wameyafanya masanamu yao kuwa kuwa washirika wa Allah katika tadbiri na uendeshaji wa masuala ya ulimwengu hali ya kuwa masanamu hayo hayakujiumba yenyewe wala hayazimiliki nafsi zao. Hayajachangia chochote katika kuwepo na kutokuwepo kwao na wala hayana taathira yoyote katika maisha ya watu. Si wapaji uhai kwa kiumbe chochote kile wala si waweza wa kumuondolea uhai mahuluku yeyote yule aliye na uhai. Hayakuwako wakati ulipoanza uumbaji wa mwanadamu na wala baada ya kufa viumbe hao hayatokuwa na uwezo wa kuwafufua na kuwapa uhai tena. Na si waweza wa kumtatulia mtu mushkili wowote katika dunia hii na wala hakuna yatakaloweza kumfanyia la kumsaidia Siku ya Kiyama huko Akhera. Ni wazi kwamba kuyaelekea na kuyashughulikia masanamu hayo ya mawe na miti humfungia mtu njia ya kumfikia Muumba wa ulimwengu na kuweka pazia zito la kizuizi kati ya Muumba na muumbwa. Na hiyo ni kinyume kabisa na wanavyoitakidi waabudu masanamu; kwani wao wanaamini kwamba masanamu hayo humuelekeza na kumuunganisha mwanadamu na Muumba wake. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba Qur'ani tukufu inazungumza na washirikina kwa hoja na mantiki katika kuzikana imani na itikadi zao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa si masanamu pekee, bali hata wanadamu pia hawana nafasi yoyote katika uhai na mauti ya wanadamu wenzao wala katika uendeshaji mambo yao, na kwa hivyo haifai kuwaweka katika hadhi na nafasi sawa na Allah SW. Na aidha aya hii inatutaka tufahamu kwamba yule ambaye hawezi kuizuia dhara isimfike yeye mwenyewe wala kujipatia manufaa yoyote hatoweza kuwafanyia wengine lolote lile. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 620 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atulinde na kila aina ya shirki, kubwa na ndogo, ya dhahiri na iliyojificha. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)