Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 21 Aprili 2008 22:00

Suratul Anfal: Aya ya 73-75

Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Bismillahi Rahmani Rahiim
Shukrani na sifa zote njema zinamstahikia Allah sw, ambaye ametuwafikisha kukutana
tena katika mfululizo mwengine wa darsa ya quran; darsa inayotoa tarjumi na maelezo
kwa muhtasari ya sura za quran tukufu kulingana na mpangilio wake ndani ya mas-haf.
Kwa wale wafatiliaji wa kawaida wa darsa hii, bila shaka mngali mnakumbuka kuwa
tungali tunaendelea kuzungumzia sura ya nane ya al Anfal ambapo hadi sasa tumeshatoa
tarjumi na maelezo ya aya 72 za sura hiyo. Katika darsa yetu hii tutatupia jicho yale
yaliyomo kwenye aya tatu za sura hiyo tukianza na aya ya 73 ambayo inasema:

Na wale waliokufuru ni marafiki wenyewe kwa wenyewe. Msipofanya hivi itakuwako
chokochoko katika ardhi na maharibiko makubwa.

Katika darsa zilizopita tulizungumzia juu ya namna waislamu wanavyotakiwa
waamiliane na maadui zao. Katika aya tuliyoisoma Mwenyezi Mungu sw anatuambia
kuwa endapo hamtatekeleza hayo niliyokuamrisheni juu ya hilo jueni kwamba vitazuka
vita na umwagaji damu mkubwa, kwani makafiri, wao wako kitu kimoja huku kila
mmoja akiwa tayari kumunga mkono mwenzake katika kufikia malengo yake. Katika aya
zilizopita Mwenyezi Mungu aliwataka waislamu wafunge mikataba na kuwekeana ahadi
za kusaidiana wao kwa wao na kuungana mkono pale mmoja wao anapokabiliwa na
hatari, badala ya kufungiana mikataba ya aina hiyo na makafiri. Hata hivyo kama
tulivyowahi kutangulia kusema, endapo waislamu watakabiliwa na mazingira ya


kulazimika kufungiana mkataba na makafiri, basi hawana budi kuheshimu mkataba na
makubaliano hayo. Aidha wajiepushe na hatua ya kutaka kutoa msaada kwa kundi la
watu, hatua ambayo itampa kisingizio adui cha kuanzisha hujuma kubwa ya
mashambulio dhidi ya waislamu; kwani hiyo itazusha balaa na fitna kubwa bali si hasha
ikawa sababu ya kuteketea roho chungu nzima za waumini. Baadhi ya mafunzo
tunayoyapata kutokana na aya hii ni kuwa hata kama kutakuwepo na kila aina ya hitilafu
na tofauti ndani ya kambi ya makafiri, lakini linapokuja suala la Uislamu, makafiri wote
huungana na kuwa kitu kimoja . Hivyo waislamu waelewe kwamba wasipoungana na
kufungiana mikataba wao kwa wao wataandamwa na fitna na uharibifu wa makafiri.
Aidha aya inatuelimisha kuwa waislamu wanatakiwa wajiepushe na kufanya mambo
yatakayompa adui kisingizio cha kuanzisha vita na umwagaji damu. Ni sifa yao makafiri
kutafuta kisingizio ili waweze kuzusha fitna na balaa hili na lile.

Ifuatayo sasa ni aya ya 74 ambayo inasema:

Na wale walioamini wakahama (kuja Madina) na wakaipigania dini ya Mwenyezi
Mungu. Na wale waliowapa (hao) mahala pa kukaa na wakainusuru (dini ya Mwenyezi
Mungu na Mtume wake). Hao ndio waislamu wa kweli. Watapata msamaha (wa
Mwenyezi Mungu) na kuruzukiwa kuzuri (kabisa huko akhera).

Aya hii kwa mara nyengine tena inabainisha kipimo cha waislamu na waumini wa kweli
na kueleza kuwa muumini hasa ni yule ambaye inapolazimu huwa tayari kuhajiri na
kuelekea kwenye medani ya Jihadi kwa ajili ya dini ya Mwenyezi Mungu . Au kwa akali


huwa tayari kuwapa hifadhi na msaada wale waliohajiri kwa ajili ya Allah sw. Tabaan
kama tujuavyo, katika mafundisho ya kiislamu hukumu ya hijra na jihadi haifungamani
na masuala ya vita tu na maadui wa Mwenyezi Mungu, bali kuhajiri na kuhama mtu
kwao na kuelekea nchi nyengine kwa ajili ya kutafuta elimu na kwenda kuwafundisha
watu wake elimu hiyo pale anaporejea kwao, ni miongoni mwa mambo yaliyousiwa sana
na Uislamu. Kama ambavyo kuhajiri pia mtu kwa ajili ya kwenda kuhudumia na
kuwasaidia watu wanyonge na walio kwenye hali duni, nayo pia inahesabiwa kuwa ni
Jihadi kubwa katika Uislamu, na yote hayo ni vielelezo vya imani ya kweli ya muislamu.
Ni wazi kwamba haiwezekani kwa watu wote katika jamii au taifa la kiislamu kuwa na
uwezo wa kuhajiri na kwenda kwenye Jihadi ya vita. Pamoja na hayo hilo halimuondolei
mtu dhima na jukumu lake la kidini. Kwani bado unabaki wajibu wa kila muislamu
kuwasaidia kifedha na kwa suhula nyenginezo wale waliohajiri, pamoja na mujahidina
walioamua kujitolea muhanga maisha yao kwa ajili ya dini ya Mwenyezi Mungu, ili kwa
njia hiyo jamii na taifa la Kiislamu lizidi kuwa imara, lenye nguvu na lililopiga hatua
mbele zaidi za ustawi na maendeleo. Na kwa hakika ni kwa njia hiyo ndipo umma wa
kiislamu utakapoteremkiwa na rehma zake Mola na waumini kughufiriwa na
kusamehewa madhambi na makosa yao na kuzidishiwa baraka na ukunjufu wa riziki
katika maisha yao. Miongoni mwa mafunzo tunayoyapata kutokana na aya hii ni kuwa
kila amali njema, hata ikiwa kubwa na ngumu, huwa na thamani pale muislamu
anapokuwa ameifanya kwa ajili ya kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu na si kwa sababu
na malengo yake mwenyewe binafsi. Hakika ni ikhlasi ndiyo inayoyafanya mema ya mtu
yadumu na kumpatia malipo mema katika maisha ya milele huko akhera. Funzo jengine
tunalolipata hapa ni kuwa muislamu hawezi kuepukana moja kwa moja na madhambi au


makosa. Na kwa njia hiyo yeye ni kiumbe anayehitajia kila wakati maghufira na
msamaha wa Mola wake.

Aya ya 75 ndiyo inayotufungia darsa yetu hii na ndiyo pia inayotuhitimishia sura yetu hii
ya Anfal. Aya hiyo inasema:

Na wale watakaoamini baadaye wakahajiri nao, wakapigana pamoja nanyi (katika
kupigania dini), basi hao ni katika nyinyi. Na ndugu wa nasaba wanastahikiana wenyewe
kwa wenyewe (katika kurithiana. Ndivyo ilivyo) katika kitabu cha Mwenyezi Mungu.
Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.

Baada ya aya zilizotangulia kubainisha nafasi na utukufu wa hijra yaani kuhama kwa ajili
ya dini ya Mwenyezi Mungu na kwenda kupigana jihadi kwa ajili ya kuinusuru dini ya
Allah aya hii ya 75 inasema, msidhani kwamba thamani hizi za kidini zinahusiana na
waislamu wa mwanzoni tu wa zama Mtume waliolazimika kukabilina na kupambana na
mushirikina wa Makka, bali wale wote watakaosilimu na kuifuata njia ya haki na
kuzitetea thamani hizo za hijra na jihadi, nao pia wataingia katika kundi la hao
waliotangulia. Pamoja na hayo waliotutangulia katika kuamini na kupigana jihadi kwa
ajili ya dini ya Mwenyezi Mungu bado wanabaki kuwa na daraja kubwa zaidi, kwani wao
walimwamini Bwana Mtume saw na wakasimama pamoja naye kuinusuru dini ya
Mwenyezi Mungu katika wakati mgumu kabisa pale Mtume alipokuwa peke yake na
kukiwa hakuna matumaini yoyote ya kufikia siku uislamu kustawi, na kuja kuwa na


nguvu na mamlaka. Hata hivyo hii haina maana kwamba suala la imani katika Uislamu
na kufikia daraja yake ya juu limefungwa kwa watu wa zama au mahali fulani tu, bali
mtu yeyote na wa zama zozote hata aliye kafiri endapo atasilimu na kuwa muislamu basi
naye pia atapata heshima na hadhi maalumu katika dini hiyo tukufu. Aya inaendelea kwa
kusema ijapokuwa waumini na waislamu kwa ujumla na hasa wale waliohajiri na
kupigana jihadi kwa ajili ya dini ya Allah wanapewa kipaumbele maalumu, lakini udugu
wa kiislamu ulioambatana na udugu wa nasaba unapewa kipaumbele zaidi, na ndiyo
maana watu walio na mahusiano ya aina hiyo wanarithiana, wakati ambapo hilo
halifanyiki kwa watu wasio na uhusiano wa damu. Baadhi ya mafunzo tunayoyapata
kutokana na aya hii ni kuwa dini ya kiislamu inawapokea kwa mikono miwili wale wote
walio tayari kuifuata nuru ya uongofu ya dini hiyo; na sheria na taratibu
walizofungamana nazo waislamu waliopita, ndizo hizo hizo zinazowahusu waislamu wa
sasa na wa baadaye. Halikadhalika aya inatuelimisha kuwa dini tukufu ya uislamu inatilia
mkazo mno katika mahusiano yake ya kijamii juu ya mafungamano ya kifamilia na
udugu wa damu. Alhamdulillah kwa taufiki yake Allah sw tumefikia tamati ya tarjumi na
maelezo ya suratul Anfal. Inshaallah Mwenyezi Mungu atujaalie tuwe watekelezaji wa
yale yote tuliyojifunza katika sura hii. Wassalamu.../

 

Zaidi katika kategoria hii: Suratul Anfal: Aya ya 70-72 »

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …