Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 21 Aprili 2008 21:59

Suratul Anfal: Aya ya 70-72

Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahi Rahmani Rahiim.
Shukrani na sifa zote njema zinamstahikia Mwenyezi Mungu Mtukufu ambaye
ametujaalia taufiki ya kukutana tena katika mfululizo mwengine wa darsa ya quran, darsa
inayotoa tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya aya za kitabu kitukufu cha Allah,
kulingana na mpangilio wa sura zake. Sura tunayoendelea kuizungumzia ni ya nane ya al
Anfal ambapo hadi sasa tumeshatoa tarjumi na maelezo ya aya 69 za sura hiyo. Katika
darsa hii tutatupia jicho aya tatu za sura hiyo tukianza na aya ya 70 ambayo inasema:

Ewe Mtume! Wambie wale mateka waliomo mikononi mwenu: "Kama Mwenyezi Mungu
akiona wema wowote nyoyoni mwenu (mkasilimu), basi atakupeni vizuri kulko
vilivyochukuliwa kwenu na atakusameheni. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa
kusamehe (na) Mwingi wa kurehemu.

Katika vita vya Badr baadhi ya wakubwa wa Makka akiwemo Abbas Ami yake Bwana
Mtume saw walikuwa katika jumla ya wapignaji wa jeshi la Makureishi waliokamatwa
mateka. Baadhi ya Masahaba walipendekeza isichukuliwe fidia yoyote kwa ajili ya
kuachiwa huru Abbas. Lakini Bwana Mtume hakukubali rai hiyo na akasema yeye pia
atoe fidia ili aachiwe huru kama walivyofanyiwa mateka wengine. Hivyo aya tuliyosoma
inasema waambieni hao mliowakamata mateka na mkawaachia huru baada ya kutoa fidia
ya kwamba kama watasilimu na kuwa Waislamu basi mlango wa rehma za Mwenyezi


Mungu uko wazi kwao na kwa njia hiyo watapata zaidi ya kile walichotolea fidia nayo ni
maghufira, msamaha na rehma za Mola Karima. Baadhi ya mambo tunayojifunza
kutokana na aya hii ni kuwa katika vita vya Jihadi waislamu wanatakiwa waamiliane na
mateka kwa wema na insafu ili kuweza kutoa nafasi ya watu hao kuweza kuifuata njia ya
haki ya Uislamu endapo nyoyo zao zitakuwa na muelekeo wa kuifuata njia ya uongofu.
Halikadhalika aya inatuelimisha kuwa waislamu wanatakiwa muda wote watoe fursa na
kuandaa mazingira kwa watenda madhambi na walio katika batili ya kuweza kurejea
kwenye njia ya haki ya fitra na kimaumbile ya Uislamu, hata kama watu hao watakuwa
wametenda dhambi ya kushiriki vita dhidi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa kuitegea sikio aya ya 71 ambayo inasema:

Na kama wanataka kukufanyia khiyana (haitakudhuru khiyana yao); wao
walikwishamfanyia Mwenyezi Mungu khiyana kabla ya hapa (kwa ukafiri wao na
kutengua kwao ahadi), lakini akakupa ushindi. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi (na)
Mwenye hikima.

Ikiendeleza yale yaliyokuja katika aya iliyotangulia juu ya suala la kuwaachia huru
mateka wa vita aya hii inasema kuchelea na kukhofu kwamba maadui hao wanaweza
kufanya khiyana kusiwe sababu ya kukufanyeni muamiliane nao vibaya, bali ni kinyume
chake, yaani amilianeni nao kwa wema na insafu mpaka waweze kuvutiwa na Uislamu.
Jueni kwamba kama mtawatendea wema mateka hao na kuamilina nao vizuri sio tu
hawatoasimama na kukupigeni vita bali watageuka na kuwa wenzenu. Hivyo suala la


kufikiria na kukisia tu kwamba yamkini wakakuendeeni kinyume haliwezi kuwa sababu
ya kukuzuieni muache kutimiza wajibu wenu . Baadhi ya nukta za kuzingatiwa katika aya
hii ni kuwa kama sisi tutakeleza wajibu wetu Mwenyezi Mungu anatosha kuwa mlinzi wa
waumini kwa ajili ya kukabiliana na njama zozote zitakazopangwa na maadui zao. Nukta
nyengine ya kuzingatiwa katika aya hii ni kuwa hakuna kitu cha kutarajia kutoka kwa
adui zaidi ya njama na khiyana, pamoja na hayo muislamu yeye anatakiwa badala ya
yeye pia kufanya khiyana ajaribu zaidi kumuonyesha adui njia ya uongofu na kutumia
kila suhula aliyonayo na fursa aipatayo kufanikisha jambo hilo.

Darsa yetu ya 275 inahitimishwa na aya ya 72 ambayo inasema:

Hakika wale walioamini na wakahama na wakapigani dini ya Mwenyezi Mungu kwa mali
zao na nafsi zao;(Nao ni wale Muhajirina). Na wale waliowapa (Muhajirina ) mahala pa
kukaa(Nao ni Ansari) na wakainusuru (dini ya Mwenyezi Mungu); hao ndio marafiki wao
kwa wao. Na walioamini, lakini hawakuhama, nyinyi hamna haki ya kurithiana nao hata
kidogo mpaka wahame. Lakini wakiomba msaada kwenu katika dini, basi ni juu yenu
kuwasaidia, isipokuwa juu ya watu ambao kuna mapatano baina yenu na wao. Na
Mwenyezi Mungu anayaona (yote) mnayoyatenda.


Kama taarikh ya Uislamu inavyoonyesha, baada ya mateso, njama na vitimbi vya
mushirikina wa kikureishi dhidi ya waislamu kukithiri huko Makka, Bwana Mtume
Muhammad saw alihama Makka na kuhamia Madina. Kufuatia hatua hiyo ya Bwana
Mtume waislamu wengine wengi, nao pia waliamua kusamehe kila chao zikiwemo mali
na nyumba zao na kuhajiri kutoka Makka na kuelekea Madina. Watu hawa katika historia
ya Uislamu wanajulikana kama Muhajirina. Huko Madina nako walikohamia waislamu
hao walikuwepo watu waliokuwa tayari wameshamuamini Bwana Mtume kabla ya yeye
kuhamia huko na ambao walijitahidi kadiri ya uwezo kuwasaidia ndugu zao wa
Muhajirina kwa hali na mali ikiwemo hata kuwapatia makazi ya kuendeshea harakati za
maisha. Watu hawa nao wanajulikana katika taarikh yaani historia ya Uislamu kwa jina la
Ansaar. Katika harakati ya kujenga na kuimarisha udugu wa Kiislamu kati ya makundi
hayo mawili ya waislamu Bwana Mtume aliwafungisha ahadi Muhajirina na Ansaar
inayowataka pamoja na mambo mengine wajiepushe na vitendo vya kuleta hitilafu na
mfarakano baina yao. Ikiashiria ahadi na makubaliano hayo yaliyopelekea kuzidi
mapenzi, urafiki na moyo wa kusaidiana kati ya Muhajirina na Ansaar, aya tuliyosoma
inasema wale ambao hawakuwa tayari kuhajiri na wakafadhilisha kunusuru nyumba na
watu badala ya dini na imani yao, hao hawaingii katika ahadi hii iliyofungwa baina ya
Muhajirina na Ansaar, ila pale nao pia watakapohama huko Makka na kujiunga na
wenzao huko Madina. Hata hivyo aya inaendelea kwa kueleza kuwa baadhi ya hao
waislamu wasiohajiri wanakabiliwa na hali ngumu ya kuwafanya hata washindwe
kuhama kuelekea Madina . Hivyo kama waislamu hao watakuombeni msaada italazimu
kuwasaidia ila kama watakuwa wanaishi katika jamii za kaumu na watu ambao nyinyi
waislamu mumefungiana nao mikataba ya kuacha uhasama, uadui na vita baina yenu.


Ambapo katika hali hiyo hamna la kufanya isipokuwa kuendelea kuheshimu makubaliano
hayo. Miongoni mwa mafunzo tunayoyapata kutokana na aya hii ni kuwa ni lazima kwa
muislamu kuihama ardhi na mazingira ya kufru, shirki na maovu ikiwa kufanya hivyo
ndiko kutakomwezesha kuinusuru imani yake na kutekeleza wajibu wake wa kidini.
Funzo jengine tunalolipata katika aya hii ni kuwa mipaka ya mikataba inayofungwa baina
ya nchi na nchi haimuondolei muislamu jukumu na wajibu wake wa kidini. Endapo
muislamu wa pembe moja ya dunia atakuwa anakabiliwa na dhulma, uonevu na
ukandamizaji na kuhitajia msaada, muislamu mwengine atakuwa na wajibu wa kumsaidia
kadiri inavyowezekana. Na aidha aya inatuelimisha kuwa ni lazima waislamu waheshimu
mikataba na makubaliano hata ikiwa wametiliana na makafiri. Hivyo madamu makafiri
hao wanaendelea kuheshimu mkataba hiyo waislamu hawana haki ya kuivunja. Kwa haya
machache ndiyo tumefikia mwisho wa darsa hii ya quran. Inshaallah Mwenyezi Mungu
atuajaalie kuwa miongoni mwa waislamu wa kweli ambao imani zao husadikishwa na
vitendo vyao. Wassalamu.../

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …