Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 21 Aprili 2008 21:58

Suratul Anfal: Aya ya 65-69

Assalamu Alaykum Warahamatullahi Wabarakaatuh. Bismillahi. Shukrani na sifa njema
zote zinamstahikia Allah sw, Muumba wa kila kitu. Tunaendelea na darsa ya yetu ya
quran inayotoa tarjumi na maelezo kwa ufupi ya kitabu kitukufu cha quran, kulingana na
mpangilio wa sura zake. Katika darsa hii tutaangazia yale yaliyomo kwenye aya zake
tano tukianza na aya ya 65 ambayo inasema:

Ewe Mtume! Wahimize walioamini waende vitani. Wakipatikana kwenu watu ishirini
wanaosubiri watashinda mia mbili (katika hao makafiri). Na kama wakiwa watu mia
moja kwenu watashinda elfu moja ya wale waliokufuru, maana hao ni watu
wasiofahamu.

Katika darsa iliyopita tulisema kuwa Mwenyezi Mungu sw alimtaka Bwana Mtume saw
pamoja na masahaba zake walikubali pendekezo la suluhu lililotolewa na makafiri kwa
kuwaambia kwamba kama adui ametoa pendekezo la kutaka suluhu, likubalini pendekezo
hilo, na wala msikhofu juu ya kile kinachoweza kutokea kutokana na hatua yenu hiyo
kwani Mwenyezi Mungu ndiye msaidizi wenu. Baada ya hayo aya hii ya 65 inamuelekea
Bwana Mtume na kumwambia kuwa kama adui hatotaka suluhu na badala yake akawa
anaendelea kupanga njama dhidi ya Uislamu basi watangazie waumini wito wa kupigana
Jihadi dhidi ya makafiri hao na waeleze kwamba wasihofu juu ya uchache wa idadi yao,
kwani Mola wenu ameshaahidi kuwa endapo nyinyi mtakuwa na istiqama na imani ya


kweli, basi kila mmoja kati yenu atakuwa na uwezo wa kukabiliana na maadui kumi, na
hayo ni matunda ya imani, kitu ambacho yeye adui yenu hana. Kwa hakika historia ya
mwanzoni mwa Uislamu inathibitisha ukweli wa maelezo ya aya hii, kwani kila pale
waislamu waliposimama imara na kwa imani thabiti, walishinda licha ya kuwa wachache
kiidadi kulinganisha na makafiri. Katika vita vya Badr waislamu walikuwa 313
kulinganisha na jeshi la wapiganaji elfu moja wa kikureishi, katika vita vya Uhud
waislamu 700 walikabiliana na makafiri 3000, katika vita vya Khandak wapiganaji wa
kiislamu walikuwa ni elfu tatu tu kulinganisha na elfu kumi wa makafiri, na katika vita
Mu-ta wakati jeshi la kiislamu lilikuwa na wapiganaji elfu kumi, idadi ya askari wa jeshi
la makafiri ilifikia laki moja. Baadhi ya yale tunayojifunza kutokana na aya hii ni kuwa
katika medani ya vita, imani na istiqama ni mambo yenye kuchangia mno katika ushindi
wa jeshi la kiislamu, na si silaha na zana za kijeshi peke yake. Aidha aya inatuelimisha
kuwa kiongozi wa jamii ya kiislamu anatakiwa awe anawaweka tayari kila wakati
wananchi kwa ajili ya Jihadi na mapambano ya kukabiliana na adui.

Ifuatayo sasa ni aya ya 66 ambayo inasema:

Sasa Mwenyezi Mungu amekukhafifishieni, maana anajua kwamba kuna udhaifu (sasa)
kwenu. Kwa hivyo wakiwa watu mia moja kwenu wenye subira na wawashinde watu mia
mbili kwao; na kama wakiwa elfu moja miongoni mwenu na wawashinde elfu mbili kwa
amri ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu yu pamoja na wanaosubiri.


Kwa mujibu wa aya iliyotangulia tumeona kuwa wakati wa mwanzoni mwa Uislamu
hukumu ya Jihadi ilikuwa ikithibiti hata pale idadi ya jeshi la Kiislamu ilipokuwa moja
ya kumi la jeshi la makafiri, na kwa mantiki hiyo kila mpiganaji mmoja wa kiislamu
alipaswa kusimama na kupambana na askari kumi wa adui. Lakini ilipofika wakati
waislamu wakawa wamedhofu kimorali na kiimani Mwenyezi Mungu sw aliwapa
takhfifu na hivyo akamtaka kila mpiganaji mmoja wa jeshi la kiislamu ajizatiti
kukabiliana na wapiganaji wawili tu wa jeshi la adui. Hii ikiwa ni ithbati juu ya nafasi ya
imani na istiqama katika ushindi dhidi ya adui, kwa maana kwamba kila pale umma wa
kiislamu unapokuwa dhaifu kiimani basi uwezo wake wa kiistiqama unapungua mara
tano. Miongoni mwa nukta za kuzingatia katika aya hii ni kuwa katika suala la uongozaji
wa jamii, baadhi ya wakati inalazimu viongozi wabadilishe kanuni kutokana na
kubadilika kwa mazingira na kwa kutilia maanani uwezo na hali ya watu. Aidha aya
inatutaka tuelewe kuwa sababu kuu ya kushindwa hutokana na hali ya ndani ya waislamu
wenyewe na si ile ya nje ya maadui. Kila pale imani, subira na istiqama ya waislamu
inapokuwa dhaifu ndipo adui anapoweza kuwashinda waislamu. Tunaiendeleza darsa
yetu hii kwa aya ya 67 ambayo inasema:

Haimpasii Nabii kuwa na mateka mpaka apigane (sana) na kushinda katika ardhi.
Mnataka vitu vya dunia hali Mwenyezi Mungu anataka (mpate thawabu za akhera). Na
Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu (na) Mwenye hikima.


Ikiendeleza yale yaliyokuja kwenye aya iliyopita katika kubainisha mbinu za kupambana
na adui, aya hii inasema wakati wa vita waislamu wanatakiwa wafikirie mambo mawili
tu, nayo ni Mwenyezi Mungu na ushindi wa dini yake dhidi ya ukafiri na shirki, na wala
wasiwe wakiwaza na kufikiria juu ya kujikusanyia ghanima na ngawira na mateka
watakaowashikilia, kwani yote hayo ni starehe za kupita za kidunia na zisizo na thamani,
na wala haziwezi kulinganishwa hata chembe na yale Mwenyezi Mungu aliyowaahidi
waislamu huko akhera. Kwa hali hiyo basi kama haitokuwa imedhihirika wazi kuwa jeshi
la waislamu limelisambaratisha jeshi la makafiri waislamu hawatakiwi kabisa
kushughulikia suala la ngawira na badala yake waendelee na mapambano tu. Baadhi ya
mafunzo tunayoyapata kutokana na aya hii ni kuwa waislamu wanatakiwa muda wote
wajihadhari na hatari ya kupaparikia dunia hata pale wanapokuwa kwenye mazingira
magumu kabisa ya vita vya Jihadi . Vile vile aya inatutaka tuelewe kuwa lengo la Jihadi
katika uislamu ni kutekeleza wajibu wa kidini na kufikia kwenye neema za akhera na si
kutaka kujipatia ngawira na kushikilia adui mateka kwa ajili ya kujipatia maslahi ya
kidunia.

Tunaihitimisha darsa hii ya 274 kwa aya za 68 na 69 ambazo zinasema:

 


Isingalikuwa hukumu iliyotangulia kutoka kwa Mwenyezi Mungu, bila shaka
ingalikupateni adhabu kubwa kwa yale mliyoyachukua.

Basi kuleni katika vile mlivyoteka (vitani), ni halali (yenu sasa) na vizuri., na mcheni
Mwenyezi Mungu . Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe (na) Mwingi wa
kurehemu.

Aya hizi kwa mara nyengine tena zinawataka waislamu wazingatie sana lengo kuu na
halisi la Jihadi la kupambana na makafiri na kueleza kuwa lau isingekuwa hukumu ya
Allah kuwa hamuadhibu mja wake kwa sababu ya jambo ambalo hajalitolea hukumu
yake, basi hapana shaka mungefikwa na adhabu kali kwa kitendo chenu hicho cha
kuchukua mateka wakati mkiwa vitani. Isitoshe ni kuwa Mwenyezi Mungu alishakadiria
kuwa nyinyi waislamu mushinde katika vita vya Badr, na kama si hivyo basi kitendo
chenu cha kuchukua mateka kingekufanyeni mpate kipigo kikali . Na muhimu zaidi
kuliko yote ni kwamba Mtume yuko pamoja nanyi, na kwa hivyo Mwenyezi Mungu
amekuepusheni na adhabu kwa heshima yake yeye. Zikiendelea, aya zinasema kile
mlichopata na kuchukua kama ngawira katika vita kinakuwa halali kwenu baada ya kutoa
khumsi au sehemu moja ya tano ya mali hiyo, ambayo ni haki ya serikali ya kiislamu. Na
mcheni Mwenyezi Mungu katika hali zote, ili kwa njia hiyo Allah akusameheni makosa
yenu. Baadhi ya nukta za kuzingatiwa katika aya hizi ni kuwa matokeo ya kitendo cha
kuchukua mateka wakati vita vinaendelea ni kupata pigo la duniani na akhera. Hivyo
hakuna maana yoyote kwa mtu kutaka kwenda kwenye Jihad kwa sababu ya maslahi ya


kidunia, kwani badala ya kwenda peponi kupitia Jihadi hiyo ajue kuwa mwisho wake
utakuwa ni motoni tu. Halikadhalika kutokana na aya hizi tunabainikiwa kuwa moja kati
ya madhihirisho ya rehma za Allah sw kwa waja wake ni kusamehe makosa na
madhambi yao; hivyo ima tujitahidi tusifanye makosa na madhambi, au kama tutateleza
na kufanya madhambi basi tuzikimbilie haraka rehma za Mola wetu kwa kumwomba
maghufira na kutubia kwake. Darsa hii ya quran tukufu imefikia tamati. Tunamwomba
Mola wetu atupe katika dunia hii yaliyo mema na atupe huko akhera yaliyo mema na
atulinde na adhabu ya moto. Wassalamu ..../

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …