Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 21 Aprili 2008 21:57

Suratul Anfal: Aya ya 60-64

Assalamu Alaykum Warahamatullahi Wabarakaatuh. Bismillahi. Shukrani na sifa njema
zote zinamstahikia Allah sw, Muumba wa kila kitu. Tunaendelea na darsa ya yetu ya
quran inayotoa tarjumi na maelezo kwa ufupi ya kitabu kitukufu cha quran, kulingana na
mpangilio wa sura zake. Katika darsa hii tutaangazia yale yaliyomo kwenye aya 5 za sura
hiyo tukianza na aya ya 60 ambayo inasema:

Basi waandalieni nguvu kama muwezavyo, na kwa farasi waliofungwa tayari-tayari, ili
kuwatishia maadui wa Mwenyezi Mungu na maadui zenu, na wengineo ambao
hamuwajui, lakini Mwenyezi Mungu anawajua. Na chochote mtakachotoa katika njia ya
Mwenyezi Mungu mtarudishiwa kamili na wala hamtadhulumiwa.

Katika darsa iliyopita tulisema kuwa mayahudi wa Madina waliokuwa wamefungiana
mkataba na Bwana Mtume Muhammad saw wa kutohujumiana wala kushirikiana na
maadui wa kila upande walikhalifu makubaliano hayo wakaamua kushirikiana na
mushrikina wa Kikureishi wa huko Makka na kupanga njama dhidi ya Waislamu.
Kutokana na kitendo chao hicho cha khiyana, Bwana Mtume aliwatangazia watu hao
kuwa madamu nyinyi mmeamua kuvunja makubaliano nasi pia hatuna sababu tena ya
kuendelea kuyaheshimu. Kufuatia hatua hiyo aya hii ya 60 ya suratul Anfaal
inamuhutubu Bwana Mtume na Masahaba zake na kuwaambia kwamba jiandaeni kijeshi


kwa namna itakayowaogofya na kuwatia khofu maadui, na kuwafanya wasiwaze wala
kufikiria kabisa kutekeleza hujuma dhidi yenu. Aya inaendelea kuwataka Waislamu
wahakikishe wanajizatiti na kujiimarisha kijeshi kadiri wanavyoweza ili kuilinda na
kuihami ardhi ya Kiislamu. Inaawaambia kwamba kama ni zana za kijeshi, basi jiandaeni
pia kwa silaha imara ili kulifanya jeshi la Kiislamu liwe na nguvu na uwezo kamili wa
kuinusuru dini ya Mwenyezi Mungu, na tambueni kuwa Mwenyezi Mungu atakulipeni
ujira kamili kwa hayo mtakayoyafanya. Baadhi ya mambo ya kuzingatiwa tunayojifunza
kutokana na aya hii ni kuwa haifai Waislamu kukaa na kusubiri adui awashambulie ndipo
waanze kufikiria namna ya kuandaa zana za kijeshi na kujiimarisha kiulinzi, bali
inavyotakiwa jeshi la Kiislamu liwe muda wote limeshajizatiti na kujiimarisha, kwa
namna itakayomfanya adui hata isimpitikie kufikiria njama ya kutaka kuishambulia nchi
au ardhi ya Kiislamu. Aidha aya inatuelimisha kuwa kwenda kwenye medani ya Jihadi na
kushiriki kwa namna moja au nyengine katika kuligharamia jeshi la Kiislamu lililoko
kwenye mapambano ya kuinusuru dini ya Allah ni wajibu wa kila Muislamu.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa kuzitegea sikio aya za 61 na 62 ambazo zinasema:

Na kama (hao maadui) wakielekea katika amani, na wewe pia ielekee na mtegemee
Mwenyezi Mungu. Hakika yeye ndiye asikiaye (na) ajuaye.


Na kama wakitaka kukukhadaa basi Mwenyezi Mungu atakutosheleza. Yeye ndiye
aliyekusaidia kwa nusura yake na kwa waliokuamini.

Baada ya aya iliyotangulia ambayo imezungumzia umuhimu na ulazima wa Waislamu
kujiweka tayari na kujizatiti kijeshi muda wote kwa ajili ya kukabiliana na njama yoyote
ile ya adui, aya hizi zinasema, msidhani kuamrishwa hayo kuna maana ya
kukuhamasisheni muingie kwenye vita na umwagaji damu, hasha wa kalla.
Mumeamrishwa mfanye hayo kwa sababu moja tu, nayo ni kumzuia adui asifikirie
kukushambulieni kijeshi, na si kukufanyeni nyinyi muwe wapenda vita. Kwa mantiki
hiyo basi endapo adui ataonyesha kuwa amedhamiria kwa dhati kuachana na vitimbi
vyake na kutaka suluhu, basi nanyi pia muwe tayari kwa hilo; na hivyo kwa kutawakkal
na kumtegemea Mwenyezi Mungu tilianeni saini naye makubaliano ya suluhu. Na
kuhusu suala kwamba pengine adui ameamua kufanya hivyo kwa hila na ujanja tu, hilo
lisikutieni khofu, kwani Mwenyezi Mungu yu pamoja nanyi, na hivyo wakati wowote ule
atakapobaini kuwa adui anafanya hila na khadaa atahakikisha hila na njama zake hizo
zinamrudia mwenyewe. Tabaan kusema hivi hakumaanishi kwamba Waislamu wawe
watu wa kukubali kimbumbumbu kila aina ya pendekezo la suluhu bila kulichunguza na
kulitafakari kwa kina. Kama ambavyo haifai kuwa wakaidi na wenye kuliangalia kwa
jicho baya kila pendekezo la suluhu linalotolewa na adui na kuhisi kwamba yamkini
pendekezo hilo limetolewa kwa makusudio mabaya. Wawe makini katika kutafakari
hayo; lakini baada ya kulihisi pendekezo lililotolewa kwa ajili ya suluhu kuwa ni la
kimantiki, palipobakia wamwachie Mwenyezi Mungu na kutawakal kwake wakiwa na
hakika kuwa yeye ndiye Msaidizi wa kweli wa waumini. Baadhi ya mambo
tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kuwa Waislamu wanatakiwa wajiimarishe kijeshi


kwa kiwango ambacho badala ya adui kufikiria suala la kushambulia afadhilishe kufikia
nao kwenye suluhu. Funzo jengine tunalolipata kutokana na aya hizi ni kuwa Uislamu si
dini inayopenda na kushabikia vita, na kimsingi inausia waumini wake wapendelee zaidi
kufikia suluhu, lakini suluhu hiyo isiwe ya kubembeleza na kumpigia magoti adui.

Wasikilizaji wapenzi darsa yetu ya 273 inahitimishwa na aya za 63 na 64 ambazo
zinasema:

Na akaziunganisha nyoyo zao; Na lau wewe ungelitoa vyote vilivyomo duniani
usingeliweza kuziunganisha nyoyo zao, lakini Mwenyezi Mungu ndiye aliyewaunganisha.
Hakika yeye ndiye Mtukufu mwenye nguvu na mwenye hikima.

Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Mwenyezi Mungu anakutoshelezea wewe na Waumini
waliokufuata.

Zikiendeleza yale yaliyokuja katika aya zilizotangulia kuhusu msaada wa Allah kwa
Bwana Mtume na Masahaba zake, aya hizi zinamuhutubu Nabii Muhammad saw na
kumwambia kuwa Waislamu hawa unaowaona leo wako kitu kimoja pamoja nawe, kabla
ya kudhihiri nuru ya Uislamu walikuwa wamekaliana kichuki, kwa bughudha na uadui
kiasi kwamba lau wakati huo ungetumia kila kilichomo katika dunia kwa ajili ya kufuta
uadui uliokuwepo baina yao na kuziunganisha nyoyo zao, pamoja na kujenga mapenzi na
udugu baina yao, usingeweza kufanya hivyo. Lakini kutokana na nuru ya Uislamu


Mwenyezi Mungu amezikurubisha pamoja nyoyo zao na kufuta kabisa uadui uliokuwepo
baina yao, na kuwafanya wote wawe watiifu na watekelezaji wa miongozo na maelekezo
yako. Hivyo basi ewe Mtume usikhofu njama wala vitimbi vyovyote vile, elewa kwamba
Mwenyezi Mungu Mola wako na Waislamu walioshikana na kuwa kitu kimoja pamoja
nawe ndio wasaidizi wako. Miongoni mwa mafunzo tunayoyapata kutokana na aya hizi
ni kuwa kutokana na nuru ya imani ya Uislamu Allah sw hufuta kila aina ya kinyongo
kilichojengeka katika nafsi na kuziunganisha nyoyo za Waislamu wote na kuzifanya ziwe
kitu kimoja. Halikadhalika aya zinatuelimisha kuwa upendo, udugu na umoja
unaopatikana kati ya Waislamu ni katika neema zake Allah kwao, na hizo pia ni
miongoni mwa sifa wanazopambika nazo watu walio Waislamu wa kweli. Vile vile
inatubainikia hapa kuwa umma wa Kiislamu unatakiwa siku zote uwe bega kwa bega na
kiongozi wao ili adui asiweze kupata mwanya wa kuzusha hitilafu baina yao. Kwa haya
machache tumefikia tamati ya darsa ya hii ya quran tukufu. Tunamwomba Allah
aziunganishe nyoyo za Waislamu wote ulimwenguni, atie mapenzi na mshikamano baina
yao na ajaalie uthibiti umoja wa kweli wa umma wa Kiislamu.../

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …