Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 21 Aprili 2008 21:56

Suratul Anfal: Aya ya 55-59

Assalamu Alaykum Warahamatullahi Wabarakaatuh. Bismillahi. Shukrani na sifa njema
zote zinamstahikia Allah sw, Muumba wa kila kitu. Tunaendelea na darsa yetu ya quran
inayotoa tarjumi na maelezo kwa ufupi ya kitabu kitukufu cha quran, kulingana na
mpangilio wa sura zake. Katika darsa hii inayoendelea kuzungumzia sura ya nane ya al
Anfal tutazungumzia aya tano za sura hiyo tukianza na aya ya 55 ambayo inasema:

Nyama walio waovu kabisa mbele ya Mwenyezi Mungu ni wale waliokufuru (kwa inadi
tu) Basi hawatoamini.

Katika darsa kadhaa zilizopita tulisoma aya zilizozungumzia radiamali na majibu ya
kiinadi ya makafiri kwa maneno ya haki waliyoambiwa na Bwana Mtume Muhammad
saw na tukasema kuwa muamala huo waliokuwa nao makafiri wa Kikuresihi huko
Makka na makafiri wengine katika kipindi chote cha historia ndio uliowafanya
waikadhibishe haki na kutokuwa tayari kuifuata kwa namna yoyote ile. Ama aya hii
tuliyoisoma hivi punde inasema kufru ya aina hii inayotokana na inadi, ukaidi na chuki tu
dhidi ya haki humfanya mwanaadamu apoteze ile hadhi aliyonayo mbele ya Mwenyezi
Mungu na kuwa duni kuliko mnyama yoyote. Ukiirejea aya ya 22 ya sura hii hii ya Anfal
utaona imeelezwa kuwa viumbe duni kabisa ni wale watu wasiotafakari na kutumia akili
zao, na hapa tunaona katika aya hii inaelezwa kuwa viumbe walio duni kabisa ni wale
ambao hawako tayari kuamini na kuikubali haki. Kwa maana hiyo basi tunaweza kufikia
natija kwamba chanzo na chimbuko la ukafiri ni kukosa mtu kutumia akili yake sawa
sawa na kwa njia sahihi. Kwa hivyo hata kama makafiri wanaweza kuonekana mbele ya
watu wengine kuwa ni shakhsiya wenye hadhi na pengine wenye ukubwa huu na ule


lakini mbele ya Allah hawana thamani yoyote zaidi ya kuwa ni sawa au duni kuliko
mnyama. Miongoni mwa mambo tunayojifunza kutokana na aya hii kuwa thamani ya
mwanaadamu iko katika kuwa kwake muamini Mungu na mwenye kuitumia akili yake
ipasavyo. Ama kufru inapomvaa mtu humvua ile sifa yake tukufu ya ubinaadamu. Funzo
jengine tunalolipata kutokana na aya hii ni kuwa wanyama wengi wana faida kwa ajili ya
maisha ya wanaadamu, kwa hiyo makafiri wasioikubali haki ni duni zaidi kulinganisha
na wanyama hao.

Ifuatayo sasa ni aya ya 56 ambayo inasema:

Ambao umepeana nao ahadi, kisha wanavunja ahadi yao kila mara wala hawaogopi.

Aya hii inaashiria uhusiano na muamala waliokuwanao mayahudi wa Madina na Bwana
Mtume saw na kueleza kuwa ijapokuwa Mayahudi hao walifunga mkataba na waislamu
kuwa hawatoshirikiana na mushrikina wa Makka dhidi ya waislamu, au wao wenyewe
kuchukua hatua yoyote kuwadhuru waislamu huko Madina, lakini watu hao waliuvunja
mkataba na makubaliano hayo mara kadhaa na hata wakashirikiana na mushrikina wa
kikureshi kuanzisha vita vya Khandaq dhidi ya Bwana Mtume na masahaba zake. Ingawa
aya hii inaashiria tabia na mwenendo wa kukhalifu makubaliano uliofanywa na makafiri
lakini kwa mujibu wa Hadithi mbali mbali kitendo cha kukhalifu ahadi na makubaliano
ni alama mojawapo ya mtu mnafiki hata kama atakuwa anasali na kufunga. Baadhi ya
nukta za kuzingatiwa katika aya hii ni kuwa inajuzu kwa Waislamu kufunga mikataba na
makafiri na mushrikina; na waislamu wana wajibu wa kuheshimu na kutovunja


makubaliano hayo maadamu makafiri hao nao wanayaheshimu. Nukta nyengine ya
kuzingatiwa hapa ni kuwa kutokuwa na taqwa ni moja ya mambo yanayochangia
kumfanya mtu avunje na kukhalifu kirahisi makubaliano aliyofikia na mwenzake.

Tunaiendeleza darsa yetu hii kwa aya ya 57 ambayo inasema:

Basi ukiwakuta vitani (pigana nao) uwakimbize, walio nyuma yao wapate kufahamu.

Kufuatia aya iliyotangulia ambayo imedhihirisha mwenendo wa makafiri na mushrikina
wa kuvunja makubaliano, aya hii ya 57 inamuelekea Bwana Mtume saw akiwa kiongozi
wa jamii ya kiislamu na kumhutubu kwamba maadamu makafiri hao na maadui wa dini
ya Mwenyezi Mungu wameshaamua kupanga njama ya kukupigeni vita basi na nyinyi
kabilianeni nao kwa nguvu zenu zote, kwa namna itakayowafanya maadui hao waingiwe
na khofu na kiwewe na kutofikiria tena suala la kuwashambulia waislamu. Bila shaka ili
waislamu waweze kukabiliana vilivyo na hali hiyo inapasa wawe macho na makini na
kuelewa vitisho vya adui, hapo ndipo wataweza kuwasambaratisha maadui zao na wale
wanaoshirikiana nao. Miongoni mwa mafunzo tunayoyapata kutokana na aya hii ni kuwa
katika vita dhidi ya maadui tusiishie kufikiria namna ya kutoa pigo kwa jeshi la adui
lililoko kwenye medani ya mapambano tu na kughafilika na suala la kukabiliana na
kuzima fitna za maadui wa nyuma ya pazia wanaopanga njama dhidi yetu. Aidha tuwe na
uoni wa mbali katika kuangalia mambo, utakaotuwezesha kubaini njama na wapangaji
wa njama hizo dhidi ya waislamu na hivyo kuweza kupambana nao na kuwashinda.
Funzo jengine linalopatikana katika aya hii ni kuwa Uislamu ni dini ya amani na utulivu,
pamoja na hayo haiko tayari kuvumilia vitendo vya uhaini na uvurugaji amani katika
jamii ya kiislamu.


Darsa hii ya 272 inahitimishwa na aya za 58 na 59 ambazo zinasema:

 

Na kama ukiogopa khiyana kwa watu (mliofanya nao ahadi) basi watupie (ahadi yao)
kwa usawa; hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wafanyao khiyana.

Wala wale waliokufuru wasifikiri kwamba wao wamekwishatangulia (mbele Mungu
hawapati), la wao hawatamshinda (Mwenyezi Mungu).

Baada ya aya ile tuliyosoma inayozungumzia kitendo cha mayahudi wa Madina cha
kuvunja makubaliano waliyofikia na Bwana Mtume, aya hizi zinaashiria mojawapo ya
kanuni kuu na kueleza kuwa kiongozi wa jamii au nchi ya kiislamu anatakiwa awe macho
na makini, kwa kadiri kwamba mara tu anapobaini ishara za kuwepo njama zinaopangwa
na maadui, basi achukue hatua haraka ya kutoa msimamo utakaomnyima adui fursa ya
kuuweka umma wa kiislamu chini ya udhibiti wake na kufanya atakalo. Kwa maana hiyo
kama ni suala la mkataba baina ya pande mbili, endapo Kiongozi wa kiislamu atabaini
kuwepo njama na hatari inayowakabili waislamu achukue hatua ya kuuvunja mkataba
huo na kuwaweka tayari waislamu kwa ajili la kulinda mipaka ya nchi yao. Na kwa
hakika hivyo ndivyo inavyotakiwa, kwamba mara tu unapopatikana ushahidi
unaoonyesha kuwa kuna njama dhidi ya umma lazima zichukuliwe hatua za kuzima
njama hiyo ; tabaan kama kuna makubaliano, basi Kiongozi wa kiislamu achukue hatua
ya kuyasimamisha lakini bila ya kuanzisha vita maadamu adui hajaanza kuchukua hatua


kama hiyo. Miongoni mwa mafunzo tunayoyapata kutokana na aya hizi ni kuwa muda wa
kwamba hakuna khofu ya kuwepo njama dhidi ya waislamu, dola ya kiislamu itapaswa
kuendelea kuheshimu mikataba na makubaliano ya kimataifa. Aidha aya zinatufunza
kuwa kitendo cha kuvunja mkataba kinatakiwa kifanyike kwa madhumuni ya kulipiza
waislamu walivyotendewa, vinginevyo kama adui hajatangulia kufanya hivyo, haifai
kabisa kwa dola ya kiislamu kuwa ya kwanza katika kuvunja na kukhalifu makubaliano.
Halikadhaika aya zinawapa changamoto viongozi wa jamii ya kiislamu ya kuwataka
wawe macho na kudhibiti hali ya mambo kikamilifu ili isije ikampitikia adui kwamba
anaweza kupata upenyo wa kuwatawala na kuwadhibiti waislamu. Darsa ya juma hili ya
quran tukufu inaishia hapa. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa waumini wa kweli na
kuzisafisha nyoyo zetu na maradhi mbali mbali yakiwemo ya unafiki. Wassalamu...../

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …