Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 21 Aprili 2008 21:55

Suratul Anfal: Aya ya 50-54

Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Bismillahi Rahmani Rahiim.
Shukrani na kila sifa njema zinamstahikia Allah sw ambaye kwa rehma na taufiki yake
tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa darsa ya kila wiki ya quran. Darsa
ambayo lengo lake kuu ni kutoa tarjumi na maelezo kwa ufupi ya sura za quran kulingana
na mpangilio wa sura hizo ndani ya mas-haf. Kwa wale wafatiliaji wa kawaida wa darsa
hii, bila shaka mnaelewa kuwa sura tunayoendelea kuizungumzia ni ya nane ya al Anfal,
tukiwa hadi sasa tumeshatoa tarjumi na maelezo ya aya 49 za sura hiyo. Katika darsa yetu
hii tutaangazia yale yaliyomo kwenye aya tano za sura hiyo, tukianza na aya za 50 na 51
ambazo zinasema:

Na laiti ungaliona Malaika wanapowafisha wale waliokufuru wakiwapiga nyuso zao na
migongo yao na (kuwaambia) : Ionjeni adhabu ya moto.

"Hayo ni kwa sababu ya (maasi) yale yaliyofanywa na mikono yenu. Na hakika
Mwenyezi Mungu si mwenye kuwadhulumu waja (wake).

Katika darsa zilizopita tuliwahi kusoma aya zinazozungumzia njama za makafiri na
wanafiki za kutaka kuwaangamiza Waislamu pamoja na kuyavunjia heshima mafundisho
matukufu ya Uislamu ambapo Mwenyezi Mungu sw aliwaahidi Waislamu kuwa endapo
watasimama imara na kutoyumba kiimani basi yeye atatoa nusra na msaada wake kwao


na kuwashinda maadui zao na njama zao. Baada ya hayo aya hizi za 50 na 51 zinasema
makafiri hao wanaoupiga vita Uislamu sio tu hawatofaulu katika lengo lao hilo ovu hapa
duniani bali hata wakati watakapotaka kutoka roho wataionja adhabu kutoka kwa
Malaika ya kutandikwa nyuso na migongo yao huku wakizikongoa roho zao. Kinyume na
ilivyo kwa Waislamu wema ambao kwa mujibu wa aya ya 32 ya suratu Nahl hutolewa
roho zao na Malaika kwa raha na upole huku wakikaribishwa kuelekea kwenye pepo ya
Mola wao. Miongoni mwa yale tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kuwa adhabu ya
kweli ya Mwenyezi Mungu kwa makafiri huanzia kwenye lahadha ya kutolewa roho.
Aidha aya zinatuelimisha kuwa malipo hasa ya adhabu atakayoyapata mja yatatokana na
yale yaliyotangulizwa na mikono yake mwenyewe na si eti kwamba Allah sw
atamuadhibu mja wake kwa madhumuni ya kulipiza kisasi.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 52 ambayo inasema:

(Hali yao hawa) ni kama hali ya watu wa Firauni na wale waliokuwa kabla yao:
walizikataa Aya za Mwenyezi Mungu, kwa hivyo Mwenyezi Mungu akawaadhibu kwa
sababu ya yale makosa yao. Bila shaka Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, na Mkali wa
kuadhibu.

Aya hii inawaliwaza na kuwapoza Waislamu kwa kuwaambia kwamba musidhani
muamala huo unaoonyeshwa na makafiri kweni ni jambo geni na kwamba ni nyinyi tu
ndio mliofikwa na masaibu hayo ya kukutana na wapinzani wa haki wanaokataa
kuuamini na kuufuata uongofu kwa inadi na ukaidi tu, bali katika kipindi chote cha


historia, hiyo imekuwa ndiyo desturi na mwenendo wa wale waliowapinga Mitume; ni
kwamba sifa yao ilikuwa ni kuikana na kuikadhibisha haki bila hoja. Kwani
mumeyasahau aliyoyafanya Firauni na wasaidizi wake kwa Musa as, au yaliyofanywa
kabla ya hapo na Namrud kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu Ibrahim as? Lakini je
hamkuona jinsi Mwenyezi Mungu alivyowadhalilisha na kuwaonjesha adhabu mataghuti
hao kutokana na maovu yaliyotendwa na mikono yao? Basi la kufanya nyinyi Waislamu
ni kumtegemea Mola wenu tu na kuendelea kukabiliana na watu hao mkijua kwamba
Allah yu pamoja nanyi. Kutokana na aya hii tunajielimisha kuwa kila pale kufru na
kumuasi Allah yanapokuwa ndio mazowea na mwenendo wa watu katika jamii, basi watu
wa jamii hiyo wajiandae na kushukiwa na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Aidha
inatubainikia kwamba mwenendo na utaratibu wa Allah sw katika kipindi chote cha
historia ni ule ule; hauja na wala hautobadilika. Nusra ma msaada kwa waliomuamini, na
adhabu na mateso kwa waliomkufuru. Ifuatayo sasa ni aya ya 53 ambayo inasema:

Hayo (ya kuwafika balaa hizi) ni kwa sababu Mwenyezi Mungu habadilishi kabisa
neema alizowaneemesha watu, mpaka wabadilishe wao yaliyomo nyoyoni mwao. Na
hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia na ni Mwenye kujua.

Aya tuliyoisoma inaashiria mojawapo ya suna muhimu za Mwenyezi Mungu yaani
utaratibu usiobadilika ambao amejiwekea katika kuamiliana na waja wake, na kueleza
kuwa kwa kawaida Allah huwaneemesha waja wake kwa neema na suhula mbali mbali
na wala haitokei kwa yeye kuwanyima, kuwaondolea na kuwabadilishia neema hizo ila


pale waja wenyewe watakapofanya mambo yatakayokuwa sababu ya kuondokewa na
kubadilishiwa neema hizo. Kwa mujibu wa aya nyengine za Quran na pia Hadithi tukufu,
kitendo cha mtu kuwafanyia dhulma wengine ni moja ya sababu kuu inayomfanya mtu
aondokewe na neema alizonazo na kupatwa na tabu, mashaka na misukosuko ya kila
aina. Kama ambavyo kutubia mtu madhambi yake na kurejea kwa Mola wake
humfungulia njia ya kushukiwa na anuai ya neema na baraka za Mwenyezi Mungu.
Baadhi ya nukta za kuzingatiwa katika aya hii ni kuwa kufuzu na kuangamia kwa
mwanaadamu kuko mikononi mwake mwenyewe, na kwa hakika ni mtu mwenyewe
anayejiamulia ipi iwe hatima na majaaliwa yake na wala hafanyiwi hilo na mwengine
yeyote. Halikadhalika tunajielimisha kuwa alivyojiwekea Allah sw ni kuendelea
kuwateremshia waja wake neema; hivyo hilo linaposita huwa ni sisi wenyewe waja ndio
tuliosababisha hayo. Vile vile tunabainikiwa kutokana na aya hii kuwa mwanadamu
ndiye mtengenezaji wa tarikh na historia, na kwa hivyo amepewa uwezo wa kubadilisha
mkondo wa historia hiyo.

Ni aya ya 54 ya sura yetu ya Anfal ndiyo inayotuhitimishia darsa yetu ya juma hili. Aya
hiyo inasema:

(Hali yao hao) ni kama hali ya watu wa Firauni na wale waliokuwa kabla yao;
walizikadhibisha Aya za Mola wao, kwa hivyo tukawaangamiza kwa sababu ya
madhambi yao , na tukawazamisha watu wa Firauni. Na wote walikuwa madhalimu.


Tumeona jinsi aya iliyotangulia ya 53 ilivyobainisha kwa uwazi kabisa juu ya kawaida ya
Mwenyezi Mungu sw kuhusiana na kuwateremshia neema waja wake. Ama aya hii ya 54
inabainisha desturi ambayo wamekuwanayo makafiri katika kipindi chote cha historia
katika ukanushaji wao wa aya za Mwenyezi Mungu na kueleza kuwa hii ni sifa
waliyonayo makafiri ya kutokubali haki na kuipinga kwa inadi na ukaidi tu .Tabaan kama
sehemu ya mwisho ya aya ya 53 ilivyosema, Mwenyezi Mungu huwakosesha watu wa
aina hiyo rehma zake zisizo na kikomo na kuwatia kwenye misukosuko na kila aina ya
masaibu; dogo kabisa miongoni mwao yakiwa ni mateso wakati wa kutolewa roho. Hata
hivyo udogo wa mateso hayo wakati wa kifo ni kama ule wa kugharikishwa Firauni
katika zama za Nabii Musa as. Pamoja na mambo mengine aya hii inatuelimisha kwa
kututaka tutadabari na kujifunza kutokana na yale yaliyowasibu waliotutangulia ili tuje
kuwa na mustakbali na hatima njema. Aidha tunajifunza kuwa dhulma huwa sababu ya
mtu kupatwa na ghadhabu za Mwenyezi Mungu. Iwe dhulma hiyo mtu amejifanyia
mwenyewe, amemtendea mwenziwe au ameifanya dhidi ya dini ya Mwenyezi Mungu.
Darsa yetu hii inaishia hapa. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa miongoni mwa wale
wanaoendelea kushukiwa na neema zake kutokana na kumtii yeye na si katika wale
wanaokatiwa neema hizo kutokana na maovu yao ya kuzikufuru neema
hizo.Wassalamu.../

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …