Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 21 Aprili 2008 21:54

Suratul Anfal: Aya ya 46-49

Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Bismillahi Rahmani Rahiim. Hii
darsa ya quran, inayotoa tarjumi na maelezo kwa ufupi ya sura za quran tukufu kwa
kuzingatia mpangilio wa sura hizo ndani ya Mas-haf. Katika darsa yetu ya juma hili
tutaangazia yale yaliyomo kwenye aya 4 za sura hiyo tukianza na aya ya 46 ambayo
inasema:

Na mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake wala msizozane msije mkaharibikiwa na
kupotea nguvu, na vumilieni. Bila shaka Mweyenzi Mungu yu pamoja na wanaovumilia.

Katika mfululizo wa darsa kadhaa, tumekuwa tukizungumzia aya zinazosimulia yale
yaliyojiri katika vita vya Badr na jinsi Waislamu walivyoshinda vita hivyo kutokana na
msaada wa ghaibu kutoka kwa Mola wao. Aya hii ya 46 inaendeleza yale yaliyokuja
katika aya zilizotangulia kwa kueleza kwamba siri ya ushindi dhidi ya maadui zenu iko
katika mambo matatu. La kwanza ni kumtii Mola wenu na Mtume wake, pili ni kuwa na
umoja na kujiepusha na mifarakano, na tatu ni kuwa na subira na uvumilivu
mnapokabiliwa na matatizo. Ijapokuwa tumekuwa tukiyasikia mataifa yote
yakizungumzia suala la umoja wa kitaifa, lakini umoja na mshikamano wa watu huwa na
thamani pale unapofanywa kwa lengo la kutii maamrisho ya Allah sw. Vinginevyo kama
umma au taifa lolote litaungana na kuwa kitu kimoja kwa lengo la kuasi na kupinga amri
za Mwenyezi Mungu, umoja na mshikamano wao huo hautokuwa na thamani yoyote.
Baadhi ya mafunzo tunayoyapata kutokana na aya hii ni kuwa Quran na Bwana Mtume


saw ndio wanaotakiwa Waislamu kuwafanya mhimili mkuu wa kujenga umoja na
mshikamano baina yao. Aidha aya hii inatuelimisha kuwa mizozo, hitilafu na mifarakano
kati ya Waislamu ndivyo vinavyowafanya wadhoofike na kushindwa kirahisi na maadui
zao. Na vile vile tunabainikiwa hapa kuwa Allah huwapa nusra na msaada wake watu
walio na imani thabiti, ama wale wanaoyumba kiimani hawawezi kuipata rehma hiyo.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa kuitegea sikio aya ya 47 ambayo inasema:

Wala msiwe kama wale waliotoka katika majumba yao kwa fakhari na kujionyesha kwa
watu na kuzuilia (watu) njia ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ameyazunguka
( kuyajua yote wanayoyafanya).

Mojawapo ya hatari inayowakabili Waislamu hususan mujahidina wanaojitolea muhanga
maisha yao kupigana katika njia ya Allah ni kuingiwa na ghururi mtu na hata kufikia hadi
ya kufanya ria ili wengine waone anavyojitolea katika njia ya Allah. Ilhali yeyote
anayejitolea nafsi yake na kuingia kwenye medani ya Jihadi anatakiwa afanye hivyo kwa
ajili ya kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu tu na isije ikawa pengine mtu anapigana na
hata kumuua mtu kwa nia nyengine isiyokuwa hiyo. Hata hivyo inawezekana mtu
akaelekea kwenye uwanja wa vita vya Jihadi akiwa moyoni mwake na nia safi ya kutaka
kuinusuru dini ya Allah na kutafuta radhi za Mola Karima tu, lakini mara akabadilika na
kuingiwa na ghururi na hisia za ria na hivyo badala ya kumfikiria Mwenyezi Mungu
akataka kuonyesha kwamba yu jabari, shujaa na mwenye nguvu kuwapita wengine wote.
Au pia akataka kujaribu kuonyesha kuwa mchango wake katika Jihadi ulikuwa mkubwa


na kwamba alikabili na kuvumilia tabu kubwa na mashaka mengi katika njia hiyo. Natija
ya kufanya yote hayo haiwi nyengine isipokuwa kuporomosha thawabu za mema yote
hayo aliyoyafanya na kumfanya awe miongoni mwa waliokhasirika. Hivyo aya
tuliyosoma inaashiria hatari mbili hizo na kuwaambia Waislamu tahadharini musije
mkawa kama Mushrikina ambao huingia vitani kwa madhumuni ya kutaka kujionyesha
na kujikweza mbele ya wengine huku lengo lao kuu likiwa ni kuwazuilia watu njia ya
Mwenyezi Mungu. Miongoni mwa mafunzo tunayoyapata kutokana na aya hii ni kuwa
tofauti iliyopo kati ya Jihadi na vita vinginevyo ni katika nia na lengo la kuingia vitani.
Wakati wengine wanaanzisha vita dhidi ya wenzao kwa sababu za kibeberu na za kuteka
ardhi za wengine, Mujahidina katika njia ya Allah huingia katika medani za vita kwa
lengo la kuondoa fitna na dhulma. Funzo jengine linalopatikana hapa ni kuwa pamoja na
njama zote wanazotekeleza maadui wa Uislamu ili kuwazuilia watu njia ya Mwenyezi
Mungu, Allah sw anaendelea kuwa mlinzi na mwenye kuinusuru dini yake ya haki.
Ifuatayo sasa ni aya ya 48 ambayo inasema:

Na ( kumbukeni ) Shetani alipowapambia vitendo vyao (wale makafiri) na kusema :"Leo
hakuna watu wa kukushindeni, mimi ni mlinzi wenu," lakini yalipokutana majeshi mawili
alirudi nyuma na kusema:" Mimi si pamoja nanyi, mimi naona msiyoyaona, mimi
ninamuogopa Mwenyezi Mungu ; na Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.


Aya hii wapenzi wasikilizaji inaashiria tena moja ya matukio yaliyojiri wakati wa vita
vya Badr na kubainisha kuwa kama ambavyo upande wa jeshi la Waislamu walikuwepo
Malaika ambao waliwapa moyo na msaada waumini, Shetani naye akiwa katika umbo la
binaadamu alifanya kazi ya kulichochea jeshi la makafiri wa Kikureishi huku akilipa
ahadi na hakikisho kuwa litashinda katika vita hivyo. Hata hivyo baada ya Shetani huyo
kubainikiwa kuwa kundi la Malaika liko pamoja na jeshi la Waislamu alitambua kwamba
Mwenyezi Mungu ameamua kuwanusuru Waislamu na hivyo hakuna njia yoyote ya
kulishinda jeshi hilo la haki. Hivyo akaamua kutimua mbio huku akitangaza kuwa
anaikhofu adhabu ya Mwenyezi Mungu. Aya hii kwa hakika inadhihirisha wazi kuwa
Shetani huwepo kwenye kambi ya batili akitoa ahadi zake za uwongo za kuwahadaa watu
wa batili mpaka akawafanya wawe tayari kutetea uovu na upotofu kwa tama ya ushindi.
Hata hivyo hakuna wanaloambulia watu hao ghairi ya hasara na majuto. Baadhi ya nukta
za kuzingatiwa katika aya hii ni kuwa kuyapamba machafu na maovu yaonekane mazuri
ni mojawapo ya kazi za Shetani, hivyo tusihadaiwe na kiumbe huyo muovu kwa
kuvutiwa na maovu yanayofanywa yaonekane mazuri. Nukta nyengine ya kuzingatiwa
katika aya hii ni kuwa sifa ya mashetani ni kuwasha na kuchochea moto wa fitna, ama
pale kweli inapodhihiri huwa wa kwanza kutafuta upenyo wa kuikwepa hatari. Nukta
nyengine ni kuwa Shetani anautambua vema uwezo na adhama ya Allah kuanzia hapa
duniani hadi huko akhera; pamoja na hayo ameamua kumkufuru Mola Muumba, hii
ikidhihirisha kwamba kutambua kitu ni jambo kimoja na kukiamini na kuakifuata ni kitu
kingine kabisa.

Aya ya 49 ndiyo inayotuhitimishia darsa yetu ya juma hili. Aya hiyo inasema:


(Kumbukeni) waliposema wanafiki na wale wenye ugonjwa nyoyoni mwao: "Watu hawa
(Waislamu) dini yao imewadanganya (hata wanajasirisha leo kukutana na nyinyi)." Na
mwenye kumtegemea Mwenyezi Mungu (atashinda kwani) Mwenyezi Mungu ndiye
ashindaye (na) Mwenye hikima.

Sifa ya watu wanafiki ni kuwa ndani ya nyoyo zao hawafurahi pale Waislamu
wanapopata ushindi. Na kwa kawaida tokea enzi za Bwana Mtume saw sifa yao ilikuwa
ni kwamba pamoja na wao wenyewe kutokuwa tayari kuingia hatarini kwa ajili ya
Uislamu lakini pia walikuwa wakijaribu kuwarai na kuwashawishi wengine wasiende
kwenye vita vya Jihadi. Si hayo tu lakini pia wakijaribu kuonyesha kuwa Waislamu
walighururiwa na dini yao hata wakajusurisha kukabilina na makafiri siku hiyo ya Badr.
Hali ya kuwa Waislamu waliingia vitani na kupata ushindi kutokana na kutawakal na
kumtegemea Mwenyezi Mungu neema ambayo wanafiki hawakuwa nayo. Baadhi ya
mambo ya kuzingatia katika aya hii ni kuwa unafiki ni maradhi ya kinafsi yasiyoweza
kutibika kwa dawa yoyote nyengine ghairi ya ile ya kuiamini haki. Aidha tunatakiwa na
aya hii tuelewe kuwa Muislamu wa kweli hufanya jitihada na juhudi ukomo wa uwezo
wake katika mambo yake, lakini kupata matunda na natija ya juhudi zake hizo
anakufungamanisha na Allah sw. Kwa maneno mengine ni kuwa anatawakal kwa Mola
Muweza. Kwa haya machache darsa ya 270 inaishia hapa. Inshaallah Mwenyezi Mungu
atujaalie kuwa waumini wa kweli wanaoshikamana ipasavyo na maamrisho yake na
kujiepusha kikamilifu na makatazo yake. Wassalamu.../

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …