Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 21 Aprili 2008 21:53

Suratul Anfal: Aya ya 42-45

Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahi Rahmani Rahiim.
Shukrani na sifa zote njema zinamstahikia Mwenyezi Mungu Mtukufu ambaye
ametujaalia taufiki ya kukutana tena katika mfululizo mwengine wa darsa ya quran, darsa
inayotoa tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya aya za kitabu kitukufu cha Allah,
kulingana na mpangilio wa sura zake. Sura tunayoendelea kuizungumzia ni ya nane ya al
Anfal ambapo hadi sasa tumeshatoa tarjumi na maelezo ya aya 41 za sura hiyo. Katika
darsa hii ambayo ni ya 269, tutaangazia yale yaliyomo kwenye aya zake nne tukianza na
aya ya 42 ambayo inasema:

(Kumbukeni) mlipokuwa kando ya bonde lililo karibu (na Madina), nao (wenye jeshi la
makafiri) walikuwa kando ya bonde lililo mbali, na ule msafara ( wa Makureishi
uliokuwa una mali yao) ulipokuwa chini yenu (upande mwengine kabisa); na kama
mngelipeana miadi mngelihitilafiana. Lakini (mmekutana vivi hivi na jeshi lao la vita) ili
Mwenyezi Mungu alipitishe jambo lililokuwa lazima litendeke, kusudi yule aangamiaye
(akakhitari ukafiri) aangamie kwa dalili zilizo dhahiri (alizokataa kuzifuata), na
anayehuika (yaani anayefuata Uislamu) ahuike kwa dalili zilizo dhahiri. Na hakika
Mwenyezi Mungu ni Mwenye Kusikia Mwenye Kujua.


Tangu tulipoanza kuizungumzia sura hii ya Anfal tumekutana na aya kadhaa ambazo
zimetoa taswira ya jinsi mambo yalivyokuwa katika vita vya Badr. Aya ya 42
tuliyoisoma hivi punde inatoa picha ya hali ya kijografia na jinsi zilivyokuwa safu za
jeshi la waislamu na jeshi la makafiri katika vita hivyo na kueleza kuwa nyinyi waislamu
mlikuwa kati kati baina ya makundi mawili ya adui; moja likiwa ni la jeshi lililojizatiti
kwa silaha likiwa linatokea Makka kukufuateni nyinyi, na jengine ni lile la msafara wa
biashara uliokuwa ukielekea Makka. Katika mazingira hayo nyinyi mlipendelea kuufuata
msafara wa biashara ili muweze kujipatia ngawira kutokana na mali za msafara huo, na
kwa njia hiyo kulihatimisha suala la vita. Lakini Mwenyezi Mungu mtukufu alitaka
badala ya msafara wa biashara, mkabiliane na jeshi la makafiri; na kwa msaada wake wa
ghaibu muwashinde makafiri hao, ili tukio hilo lizipe nguvu na kuziimarisha imani zenu
na pia kuwathibitishia makafiri kwamba nyinyi ndio mlio katika haki. Na kwa hivyo
yeyote miongoni mwao aliye na nia ya kutaka kuutambua na kuufuata uongofu asilimu
na kuufuata Uislamu, na kwa yule ambaye hayuko tayari kuifuata haki, basi afanye hivyo
pia kwa uelewa na utambuzi kamili. Maelezo ya aya hii yanatuonyesha kuwa Waislamu
hawakuwa wamejiandaa kukabiliana na jeshi la makafiri wa Makka huko Badr; na kwa
maelezo ya quran ni kwamba hata kama wangekuwa wamepanga tokea hapo awali
kwenda kupigana na maadui wa Mwenyezi Mungu mahala hapo, basi siku hiyo
wasingekuwa tayari kufanya hivyo. Baadhi ya mafunzo tunayoyapata kutokana na aya hii
ni kuwa ushindi wa Waislamu katika vita vya Badr ilikuwa ni hoja ya wazi ya
kuthibitisha kwamba Uislamu ulikuwa katika haki na Shirki ya Makureishi ilikuwa
upande wa batili. Funzo jengine tunalolipata hapa ni kuwa imani na ufuataji wa uongofu


huwa na thamani ya kweli pale unapofanywa kwa utambuzi na uelewa sahihi na si
kutokana na taasubi au mazowea tu.

Tunaiendeleza darsa hii kwa aya ya 43 ambayo inasema:

(Kumbuka) Mwenyezi Mungu alipokuonyesha katika usingizi wako (kwamba wao
makafiri ) ni wachache. Na kama angelikuonyesha kwamba wao ni wengi mngalivunjika
moyo na mngalizozana katika jambo hilo. Lakini Mwenyezi Mungu akakulindeni (na
hayo). Bila shaka Yeye ni Mjuzi wa yaliyomo vifuani.

Msaada mmojawapo wa ghaibu walioupata Waislamu katika siku ya vita vya Badr
ulikuwa ni usingizi uliowachukua wapiganaji wengi wa Kiislamu kabla ya vita kuanza,
usingizi ambao uliowaondolea machovu na kuwafanya wawe tayari kikamilifu kiroho na
kimwili kuingia kwenye medani ya vita kukabiliana na adui. Ikilizungumzia suala hilo
aya ya 43 ya sura yetu ya Anfal inasema msaada mwengine wa ghaibu waliopata
Waislamu ni kwamba Allah sw alimuonyesha Bwana Mtume saw usingizini kuwa jeshi
la Makafiri ni lenye wapiganaji wachache na hivyo pale Bwana Mtume alipowasimulia
masahaba zake ndoto hiyo Waislamu hao walipata ujasiri mkubwa na hivyo kutotishika
na wingi halisi wa jeshi la makafiri wa Kikureishi. Miongoni mwa mambo tunayojifunza
kutokana na aya hii ni kuwa ndoto za kweli ni mojawapo ya njia za mawasiliano kati ya
waja wema na Allah sw. Halikadhalika aya hii inatuelimisha kuwa katika vita na maadui
ni marufuku kuwatangazia wapiganaji wa jeshi la Kiislamu ukubwa wa jeshi la makafiri


na silaha zao. Kwani kufanya hivyo kunaweza kuwadhoofisha na kuwavunja moyo
wapiganaji hao.

Tunaiendeleza darsa hii kwa aya ya 44 ambayo inasema:

Na (kumbukeni) alipokuonyesheni machoni mwenu mlipokutana kwamba wao ni
wachache na akakufanyeni nyinyi kuwa wachache (mno kabisa) machoni mwao ili
alitimize jambo aliloamrisha litendeke. Na mambo yote hurejeshwa kwa Mwenyezi
Mungu.

Tumesema kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu alimuonyesha Bwana Mtume saw katika
ndoto kuwa idadi ya makafiri ni ndogo kinyume na hakika yao. Lakini mbali ya Bwana
Mtume, hata katika uwanja wa mapambano Mwenyezi Mungu aliwafanya makafiri
waonekane wachache mbele ya macho ya wapiganaji wa Kiislamu hali iliyozidi kuwapa
moyo wapiganaji hao na kupata nguvu zaidi ya kukabiliana na adui. Ama mbele ya
macho ya makafiri, wapiganaji wa Kiislamu walionekana ni wachache mno zaidi ya
ilivyokuwa hakika yao, jambo ambalo liliwatia ghururi makafiri na kuhisi kwamba vita
hivyo ni vyepesi na wala hakuna haja ya wao kuomba msaada wa askari wa dhiba. Aya
hii inatufunza pamoja na mambo mengine kuwa ushindi haupatikani kwa kutegemea
wingi wa kiidadi tu, kwani kama watu watakuwa Waislamu wa kweli walio na imani
thabiti juu ya Mola wao, basi yeye Mwenyezi Mungu anaweza hata kuwafanya wengi
waonekane wachache, na wachache waonekane wengi kiidadi.


Aya ya 45 ya sura yetu ya Anfal, ndiyo inayotuhitimishia darsa yetu hii. Aya hiyo
inasema:

Enyi mlioamini! Mkutanapo na jeshi (la makafiri) kazaneni barabara (wala msikimbie)
na mumkumbuke Mwenyezi Mungu kwa wingi ili mpate kufaulu.

Katika sehemu hii ya mwisho ya aya hizi Allah sw anawaambia Waislamu kwamba
baada ya sisi kukupeni msaada wetu wa ghaibu, nanyi pia inakubidini mujikaze na
kutolegalega wala kukhofu au kuogopa chochote. Daima muwe mkinikumbuka mimi
Mola wenu, kwani kufanya hivyo kutazifanya nyoyo zenu ziwe thabiti, na tambueni pia
kwamba nusra na uokovu unapatikana kwa kudumu katika kushikamana na dini tukufu
ya Mwenyezi Mungu. Baadhi ya mafunzo tunayoyapata kutokana na aya hii ni kuwa
mojawapo ya masharti ya imani ya kweli ni kuwa na msimamo thabiti na usiolegalega
katika masuala yote ya dini, msimamo thabiti ambao ndio siri ya ushindi katika vita na
maadui wa Allah. Aidha aya inatutaka tuelewe kuwa kumtaja na kumkumbuka kwa dhati
Mola Mwenyezi humlinda muumini na ghururi inayoweza kumuingia kutokana na
ushindi anaopata dhidi ya maadui wa Uislamu. Kwa haya machache ndiyo tunafikia
tamati ya darsa yetu hii. Inshaallah Mwenyezi Mungu atujaalie kuwa miongoni mwa
Waislamu wa kweli walio tayari kuinusuru dini yake ya haki kwa mali zao na nafsi zao.
Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh../

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …