Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 21 Aprili 2008 21:52

Suratul Anfal: Aya ya 38-41

Assalamu Alaykum Warahamatullahi Wabarakaatuh. Bismillahi. Shukrani na sifa njema
zote zinamstahikia Allah sw, Muumba wa kila kitu. Tunaendelea na darsa yetu ya quran
inayotoa tarjumi na maelezo kwa ufupi ya kitabu kitukufu cha quran, kulingana na
mpangilio wa sura zake. Katika darsa hii tunaanza na aya ya 38 ya Sura yetu ya al-
Anfaal:

Waambie wale waliokufuru: "Kama wataacha (yale mabaya waliyokuwa nayo)
watasamehewa yaliyopita, na wakiyarudia (tutawatesa kama tulivyowatesa wao mara
zilizopita na kama tulivyoitesa hiyo mijikafiri mikubwa ya zamani); imekwisha kuwapitia
mifano ya (mambo yaliyowapata) watu wa zamani."

Mojawapo ya rehema kubwa za Mwenyezi Mungu kwa waja wake ni kwamba,
ameuwacha wazi mlango wa toba na kuwachana na dhambi katika kila zama na
mazingira. Rehema hiyo si kwa waumini watenda dhambi tu, bali na hata kwa makafiri
wasio na imani wanapoachana na upotofu wao wa kifikra na kivitendo na kuamua
kumrejea Muumba wao. Hata hivyo, baada ya kupata imani na kutubu, makafiri
hawalazimiki kulipa swala wala amali nyingine za kiibada zilizopita wakati wa ukafiri
wao. Aya hiyo inaendelea kusema kwamba, kama makafiri hao watarudia tena maovu
yao, Mwenyezi Mungu atawafanya alivyowafanya watu waliowatangulia. Tunajifunza
yafuatayo kutokana na aya hii:

1- Kipimo cha kupimia watu ni hali yao ya hivi sasa na wala sio ya zamani.


2- Uislamu si dini ya vita, bali husaidia kurekebisha na kuwaongoza makafiri.

Sasa tuitegee sikio aya ya 39:

Na piganeni nao (makafiri) mpaka yasiweko mateso (nyinyi kuteswa na wao kwa ajili ya
dini kama wanavyokuteseni sasa); na dini iwe kwa ajili ya Mwenyezi Mungu
(asitaaradhiwe mtu kuabudu dini anayoitaka). Lakini wakiacha, basi hakika Mwenyezi
Mungu anayaona wanayoyatenda.

Baada ya aya iliyopita kuwaita makafiri katika Uislamu na kuwacha wazi mlango wa
toba kwao, aya hii inasema kwamba, kama makafiri hao hawataacha mwenendo wao huo
na kuendelea na njama zao za kumpiga vita Mtume, kabilianeni nao vilivyo hadi waamue
kuachana na fitina zao na haki kutawala. Kimsingi jihadi katika Uislamu haina maana ya
kuteka nchi kupitia vita, bali ina maana ya kuondoa dhulma na uonevu na kuleta usawa,
uadilifu na amani ya kudumu duniani. Lengo hilo linaweza kufikiwa tu kwa kutekelezwa
kikamilifu amri na sheria za Mwenyezi Mungu. Ni wazi kuwa, lengo hilo halijafikiwa
lakini kwa msingi wa hadithi za kuaminika kutoka kwa Mtume (SAW), uadilifu, haki na
usawa huo utaletwa na mtu kutoka katika kizazi chake aitwaye Imam Mahdi ambaye
atadhihiri ulimwenguni katika siku za mwisho za dunia hii.

Kutokana na aya hii tunajifunza kwamba:

1- Washirikina na makafiri ndio hueneza vita duniani. Hutekeleza njama na fitina
kwa lengo la kuendelea kuitawala dunia.2- Madamu maadui wanaeneza fitina, amri ya kukabiliana nao ingalipo na hapasi
mtu kuzembea katika kutekeleza amri hiyo.


Aya ya 40 inasema:

Na kama wakigeuka basi jueni kwamba Mwenyezi Mungu ndiye Mola wenu, ni Mola
Mwema na Msaidizi Mwema (atakuhifadhini nao).

Mojawapo ya mambo yanayohatarisha maisha ya mwanadamu humu duniani, ni
kutokuwa na uthabiti wa kifikra, kiitikadi na kivitendo. Kama tunavyoshuhudia, baadhi
ya watu huwa hawana msimamo na leo utawaona wakiwa na kundi hili na kesho kujiunga
na kundi jingine ambalo lina fikra na mitazamo tofauti kabisa na kundi la kwanza. Leo ni
waumini na kesho ni makafiri. Leo ni wema na kesho washari.

Katika aya hii, Mwenyezi Mungu anawahutubu waumini kwa kuwaambia kwamba, hali
hiyo ya kulegalega inayoonekana katika baadhi ya watu isiwafanye wao kupata shaka
kuhusiana na njia ya haki wanayoifuata wala kudhoofisha uthabiti wa fikra zao.
Anawataka wawe wathabiti katika njia na msimamo wao na wafahamu kwamba,
Mwenyezi Mungu yu pamoja nao, ni Mola wao na kwamba atawasaidia kwa kila njia.
Hata kama watu wote watakosa kuwaunga mkono au hata kusimama dhidi yao, hawapasi
kuwa na wasiwasi kwa sababu wana Mwenyezi Mungu na makafiri hawana msaidizi
yoyote wa kuwanusuru.

Tunajifunza yafuatayo kutokana na aya hii:


1- Tunapasa kumtegemea Mwenyezi Mungu tu katika uendeshaji wa mambo yetu.
Hii ni kwa sababu, kuna watu wengi wanaotuunga mkono leo lakini kesho huenda
wakatukimbia wakati wa haja na dhiki.
2- Mwenyezi Mungu ndiye Mola mzuri zaidi. Hatutupilii mbali kwa watu wengine
wala kutusahau. Hatuhitajii sisi wala kukosa kutulipa kutokana na usumbufu
tunaoupata.


Aya ya 41 inasema:

Na jueni ya kwamba, chochote mnachokiteka (mnachokipata ngawira), basi sehemu yake
ya tano ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na Mtume na jamaa (zake Mtume) na mayatima
na masikini na wasafiri (walioharibikiwa); ikiwa nyinyi mumemuamini Mwenyezi Mungu
na tuliyoyateremsha kwa mja wetu siku ya kipambanuzi, siku (inayowafikiana na siku)
yalipokutana majeshi mawili (siku ya vita vya Badri - jeshi la Waislamu na jeshi la
makafiri). Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye uweza juu ya kila kitu.

Kufuatia jihadi iliyosisitizwa katika aya zilizopita, aya hii inasema kwamba, Waislamu
wanapasa kutumia thumuni moja ya ngawira wanayoipata katika vita kwa malengo
aliyoyakusudia Mwenyezi Mungu. Kama kweli mnapigana kwa njia ya Mwenyezi
Mungu mnapasa kutekeleza kwa makini maagizo yake kuhusiana na jihadi. Hata kama
Waumini hujitolea na kuwacha kila kitu kwa lengo la kwenda kupigana jihadi, lakini ni


wazi kwamba, utajiri na mali nyingi inayopatikana katika vita hivyo kwa anwani ya
ngawira huwashawishi sana Waislamu na kwa hivyo ni rahisi hata kwa waumini
kuhadaika na mvuto wa mali hizo na hatimaye kushawishika kutotoa khumsi ya mali
hiyo kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu ili itumike katka kuendeshea masuala ya serikali
ya Kiislamu, kukiwemo kukidhi mahitaji ya mayatima, masikini na wasafiri. Kwa hivyo,
aya hii inasema kwamba, kama kweli mna imani thabiti, baada ya kutoa maisha yenu kwa
ajili ya Mwenyezi Mungu, mnapasa pia kutoshawishika na ngawira mnazopata vitani na
kuzitumia kwa njia zinazotakikana. Ni wazi kuwa neno "ghanimat" ambalo limetumika
katika ya hii kwa maana ya ngawira, linajumuisha pato lolote analopata Muislamu hata
nje ya vita. Kwa mujibu wa Hadithi za Ahlul Beit (AS), Muislamu anapasa kutoa khumsi
moja ya pato hilo kwa ajili ya kutumika katika njia zilizobainishwa katika aya hii.

Hata kama aya hii iliteremka kuhusiana na ngawira zinazopatikana vitani, lakini ni wazi
kuwa, ina maana pana zaidi kuliko vita tu na kwa hivyo katika zama hizi ambapo Mtume
wa kupewa ngawira hizo hayuko tena miongoni mwetu, ni wanazuoni wanaofuatwa
katika masuala ya kidini na waadilifu tu ndio wanaopaswa kupewa khumsi za pato kwa
shabaha ya kutumika kwa maslahi ya kidini. Kuna baadhi ya sehemu na watu waliotajwa
wazi katika matumizi ya khumsi hizo, nao ni kama vile mayatima, masikini na wasafiri.
Maana ya Dhulqurba katika aya hii ni watu wa Nyumba ya Mtume waliofikia daraja la
uimamu na uongozaji wa umma wa Kiislamu. Kwa msingi huo, hisa ya Mwenyezi
Mungu, Mtume na Maimamu inapasa kutumika katika kuendeshea masuala ya serikali ya
Kiislamu na sio kufanywa kuwa ni mali yao binafsi. Tunajifunza yafuatayo kutokana na
aya hii:


1- Watu masikini katika jamii wanapaswa kupewa msaada kutokana na pato la watu
wenye uwezo kwenye jamii na kwa hivyo ni washiriki katika kunufaika na mali
za matajiri.
2- Vita na jihad ni mtihani wa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kupambanuliwa kati
ya wakweli, waongo, waumini na wanafiki.
3- Vita vya Badr ni mfano mzuri wa msaada wa Mwenyezi Mungu kwa lengo la
kuwapa ushindi Waislamu, msaada ambao ameuashiria katika sehemu nyingi
kwenye kitabu chake kitakatifu cha Qur'ani.


Hadi hapa ndio tumefikia mwisho wa darsa hii. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi
Wabarakaatuh../

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …