Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 21 Aprili 2008 21:51

Suratul Anfal: Aya ya 34-37

Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Bismillahi Rahmani Rahiim
Shukrani na sifa zote njema zinamstahikia Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa neema zote
alizotuneemesha, tunazozijua na zile tusizozijua. Huu ni mfululizo mwengine wa darsa
ya quran. Darsa hii inaanzia kwenye aya ya 34 ya sura yetu ya Anfal ambayo inasema:

Lakini wao (Maqureshi) wana jambo gani (zuri) hata Mwenyezi Mungu asiwaadhibu; na
hali ya kuwa wanazuilia (watu) na huo Msikiti Mtakatifu? Nao hawakuwa walinzi wake
(msikiti huo). Hawakuwa walinzi wake (na walinzi wa kila msikiti) isipokuwa wacha
Mungu tu, lakini wengi katika wao hawajui lolote, (wanajisemea tu).

Tulisema katika kipindi kilichopita kwamba, kuwepo Mitume katika kaumu mbalimbali
kulizuia kaumu hizo kupatwa na adhabu ya Mwenyezi Mungu na kwamba kuwepo kwao
katika kaumu hizo kulihesabiwa kuwa baraka kubwa. Aya hii inasema kwamba, watu hao
walistahili kupata adhabu kutokana na kuwa walijipa jukumu la kulinda msikiti mtakatifu
wa al- Haram hali ya kuwa hawakufaa kufanya hivyo kutokana na hali yao ya ukafiri.
Kwa hivyo, Mwenyezi Mungu atawaadhibu siku ya Kiama kutokana na suala hilo na pia
kuwapa adhabu humu duniani kwa kuwazushia balaa, vita na kuwapelekea watekwe
nyara.

Tunajifunza yafuatayo kutokana na aya hii:


1- Wale wote wanaowazuia kwa njia yoyote ile waumini kuingia katika Nyumba ya
Mwenyezi Mungu al-Kaaba, na kuidhibiti nyumba hiyo, wasubiri adhabu ya
Mwenyezi Mungu. Mfano wa watu hao ni Wazayuni ambayo kwa kuudhibiti na
kuuweka chini ya usimamizi wao msikiti wa al-Aqswa wamekuwa wakiwazuia
kwa njia mbalimbali Waislamu kuingia katika msikiti huo.
2- Usimamizi wa misikiti unapaswa kufanywa na watu wasafi na wanaofaa na sio
wachafu na wasiofaa kisheria wala kimaadili.


Ifuatayo sasa ni aya ya 35:

Na haikuwa ibada yao (hao makafiri) hapo katika hiyo nyumba tukufu ila kupiga miunzi
(mbija) na kupiga kofi. Basi (wataambiwa) onjeni adhabu (leo) kwa sababu ya kule
kukufuru kwenu.

Katika kuendelea kutoa dalili za kutofaa makafiri kusimamia masuala ya msikiti wa al-
Haram katika zama za Mtume Mtukufu (SAW) katika aya iliyopita, aya hii imeendelea
kuzungumzia suala hilo na kusema kuwa, makafiri walikuwa wakidhani kwamba wao ni
wapenda dua, kwa kuomba dua kwa njia waliyotaka wao na kuifadhilisha na wala sio
kwa namna waliyotakiwa wafanye na Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo, walikuwa
wakikusanyika kando ya Nyumba ya Mwenyezi Mungu na kupiga chini miguu, kupiga
makofi, mbinja na miluzi wakidhani kwamba walikuwa wakimwabudu na kumwomba
dua Mwenyezi Mungu kwa njia inayofaa. Katika zama hizi pia, kuna baadhi ya
Waislamu wanaofanya vitendo kama hivyo kwa kujikusanya katika sehemu maalumu na


kucheza dansi kwa kuimba wakidai kwamba, wanamwabudu Mwenyezi Mungu, jambo
ambalo halina msingi wowote katika Uislamu.

Tunajifunza yafuatayo kutokana na aya hii:

1- Katika kipindi kirefu cha historia, baadhi ya amali za kidini zimepotoshwa na
kuingizwa humo mambo na imani zisizo na msingi.
2- Kuyafanyia dharau matukufu ya Mwenyezi Mungu huandamana na adhabu kali
ya MwenyeziMungu.


Hebu sasa na tuitegee sikio aya ya 36 ya Sura hii:

Hakika wale waliokufuru hutoa mali zao ili kuzuilia (watu wasipate kuamini) njia ya
Mwenyezi Mungu. Basi watazitoa, kisha zitakuwa majuto juu yao, kisha watashindwa. Na
wale waliodumu katika ukafiri watakusanywa katika Jahannamu (Watakaosilimu
baadaye Mungu atawasamehe).

Aya hii inaashiria bajeti na gharama kubwa zilizokuwa zikitolewa na makafiri kwa lengo
la kuharibu na kuvuruga mipango ya Mtume Mtukufu (SAW) kwa lengo la kueneza
Uislamu. Inasema kwamba, makafiri ambao hawakuweza kukabiliana na Mtume
Mtukufu kimantiki walitoa pesa nyingi kwa lengo la kuwazuia watu wasikubali wito wa
kidini wa Mtume. Kwa kuanzisha vita ambavyo viligharimu fedha nyingi, makafiri hao
pia walijaribu kumuua Mtume na kutokomeza dini yake tukufu. Pamoja na hayo lakini
waliendelea kufedheheka na kujuta baadaye kwa sababu fedha zao zilendelea kupotea


lakini hawakuweza kufikia lengo walilotaka la kuuharibu Uislamu pamoja na Mtume
wake. Qur'ani inasema kwamba, majuto na kushindwa huko kulitokana na mfungamano
wao wa kupindukia wa masuala ya kidunia na kwamba juu ya hayo, bado adhabu ya
Akhera ilikuwa inawasubiri.

Tunajifunza kutokana na aya hii kwamba:

1- Tusidhani kwamba maadui wetu wamekaa kimya bila ya kutufanyia njama
yoyote, hata kama wataonekana kidhahiri kwamba hawafanyi lolote dhidi yetu.
Kwa hakika huwa wanatumia fedha nyingi kisiri kwa lengo la kutekeleza
mipango ya kiuadui dhidi ya Waislamu na Uislamu.
2- Waumini wawe na matumaini kuhusiana na mustakbali wao. Hii ni kwa sababu,
ukafiri pamoja na nguvu na utajiri wote ulionao, lakini mwishowe utashindwa tu.


Sasa tunasikiliza aya ya 37 na tarjuma yake:

Ili Mwenyezi Mungu apate kuwapambanua walio wabaya na walio wazuri na kuwaweka
wabaya juu ya wabaya wengine na kuwarundika wote pamoja na kuwatupa katika
Jahannamu. Hao ndio waliokhasirika.

Baada ya kuashiriwa mipango ya maadui katika aya iliyopita, aya hii inasema mgongano
baina ya haki na batili ambayo ni machaguo ya hiari ya mwanadamu, ni uwanja wa
mtihani wa Mwenyezi Mungu ili wema wapate kupambanuliwa kutokana na waovu na
hivyo kuweza kufahamika vyema makundi mawili hayo mbele ya watu wengine. Watu


waovu wanapaswa kufahamu kuwa, si tu kwamba hawatalipwa wema humu duniani bali
pia huko Akhera watatupwa motoni kwa mrundiko na madhila kama pote chafu
lisilokuwa na thamani yoyote. Kwa hakika, ni kilele cha hasara kwa mwanadamu kukosa
dunia na Akhera kwa wakati mmoja.

Tunajifunza yafuatayo kutokana na aya hii:

1- Utenganishwaji wa wafuasi wa haki na batili ni sunna ya Mwenyezi Mungu ili
kubainisha hali halisi ya wanadamu.
2- Urundikwaji, mbano na mbinjo ni miongoni mwa sifa za Jahanamu na watu wa
Jahanamu.


Kwa haya machache ndio tumefikia mwisho wa darsa hii. Mwenyezi Mungu atujaalie
kuwa miongoni mwa waja wake wema wanaoshikamana na maamrisho yake na
kujiepusha na makatazo yake. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh../

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …