Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 21 Aprili 2008 21:50

Suratul Anfal: Aya ya 30-33

Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Bismillahi Rahmani Rahiim. Hii
darsa ya quran, inayotoa tarjumi na maelezo kwa ufupi ya sura za quran tukufu kwa
kuzingatia mpangilio wa sura hizo ndani ya Mas-haf. Katika mfululizo huu tutaendelea
na tarjumi na maelezo ya sura ya nane ya al Anfal tukianza na aya 30 ambayo inasema:

Na (kumbuka Ewe Nabii Muhammad) walipokufanyia hila wale waliokufuru ili
wakufunge au wakuue au wakutoe( kwa hali mbaya katika Makka); na wakafanya hila
(zao barabara); Na Mwenyezi Mungu akazipindua hila hizo. Na Mwenyezi Mungu ni
mbora wa kupindua hila (za watu wabaya).

Kwa kupita miaka 13 tokea abaathiwe Mtume Mtukufu katika mji wa Makka na kuenea
umashuhuri wake katika mji huo na hasa miongoni mwa tabaka la vijana, wazee wa
washirikina wa mji huo walikusanyika pamoja kwa lengo la kupanga njama ya
kukabiliana na wimbi hilo la kuenea Uislamu katika mji huo. Katika mkutano wao
walioandaa kwa lengo hilo, walikubaliana kutekeleza mojawapo ya mipango mitatu
tofauti. Wa kwanza ulikuwa ni kumfunga jela Mtume, wa pili kumbaidishia katika
maeneo ya mbali na wa tatu, kumuua. Hatimaye waliafikiana kumuua ambapo ili
kuepusha matokeo mabaya ya kulipiza kisasi ukoo wa Mtume, waliamua kila kabila
limtoe mtu mmoja ambao wote wangeshirikiana kwa pamoja katika kumuua Mtume na
hivyo kuzuia ukoo huo wa Mtume kuliandama kabila fulani mahsusi kwa lengo la
kulipiza kisasi.


Kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu, Mtume alifahamishwa njama hizo za washirikina
kupitia Malaika Jibril na Mtume kulazimika kuondoka mjini Makka usiku kuelekea
sehemu iliyokuwa na usalama zaidi. Usiku huo Imam Ali (AS), aliamua kulala kwenye
kitanda cha Mtume na hivyo kujitolea mhanga kumlinda Mtume katika jukumu lake zito
la kueneza Uislamu duaniani. Aliamua kulala kwenye kitanda hicho ili kuwafanya
washirikina wadhani kwamba Mtume alikuwa angali yupo nyumbani kwake ili
wamvamie wakati mnasibu. Aya hii inaashiria njama hiyo iliyofanywa na makafiri kwa
lengo la kumuua Mtume na mikakati aliyofanya Mwenyezi Mungu kwa shabaha ya
kumlinda Mtume wake kwa kubatilisha njama za washirikiana. Alitekeleza mikakati hiyo
ili kuvunja majivuno na majigambo ya washirikina na kuwathibitishia kwamba,
hawakuwa na ujanja kuliko Mwenyezi Mungu na kuwahakikishia waumini kwamba
alikuwa pamoja nao na kwa hivyo hakukuwepo na sababu ya wao kukata tamaa na
rehema yake. Tunajifunza yafuatayo kutokana na aya hii:

1- Mantiki ya wapinzani ni jela, ugaidi, na ubaidishaji na njia ya Mitume ni
mafunzo, utakasaji na malezi.
2- Mwenyezi Mungu ni mlinzi wa Mitume wa haki na kila mtu anayefanya njama
dhidi yao huwa anakabiliana moja kwa moja na Mwenyezi Mungu.


Sasa na tusikilize aya ya 31 ya sura hii:

Na (Maqureshi) wanaposomewa Aya zetu, husema: "Tumekwishasikia (hayo zamani). Na


lau tungependa tungesema kama haya. Haya si chochote ila ni hadithi tu za watu wa
kale."

Aya tuliyosoma mwanzoni inazungumzia suala la kutaka kuuliwa Mtume na washirikina
wa Makka ilhali aya hii inagusia ukaidi wa washirikina hao katka kuzifanyia istihzai na
kuzikejeli aya za Mwenyezi Mungu kiasi cha kuzitaja kuwa ni hadithi na ngano tu
zilizotungwa na watu. Hii ni katika hali ambayo, kwanza, sehemu ya Qur'ani Takatifu
inazungumzia historia ya baadhi tu ya kaumu zilizopita na sio zote, na pili hadithi zote
zinazowahusu Mitume zilizozungumziwa katika Qur'ani, ni ukweli mtupu. Nyingi ya
hadithi hizo zimethibitishwa na wasomi pamoja na wataalamu wa masuala ya kihistoria
kupitia nyaraka za kihistoria na kijografia. Kwa msingi huo kuzitaja hadithi hizo kuwa ni
ngano tu ni tuhuma zisizo na msingi na zilizokuwa na lengo la kuwapotosha watu.
Kutokana na aya hii, tunajifunza yafuatayo:

1- Wapinzani wa Uislamu wanadai kwamba, Qur'ani Takatifu si kitabu muhimu na
kwamba wanaweza kubuni na kutunga kitabu kama hicho, madai ambayo
hawajaweza kuyathibitisha hadi sasa.
2- Tuhuma za ujinga na kuabudu mambo ya kale ni miongoni mwa tuhuma za kale
mno ambazo hutolewa dhidi ya waumini na kitabu chao kitakatifu.


Aya ya 32 ya Surat al-Anfaal inasema:

Na (kumbuka) waliposema (makafiri): "Ee Mwenyezi Mungu! Kama haya (aliyokuja


nayo Muhammad) ni haki itokayo kwako, basi tupige kwa mvua ya mawe yanayotoka
mbinguni au tuletee adhabu nyingine iumizayo (yoyote ile; lakini sisi hatufuati)."

Aya hii inaonyesha wazi kilele cha ukaidi na inadi ya wapinzani wa Mtume Mtukufu
(SAW). Kutokana na kuwa hawawezi kustahamili maneno ya kweli ya Mtume,
wanamwambia Mtume kwamba, kama kweli anayoyasema ni kweli na kwamba kuna
Mwenyezi Mungu anayeweza kumuadhibu yeyote anayempinga Mtume wake, basi
amwambie Mwenyezi Mungu huyo awateremshie adhabu kali zaidi ya kuwanyeshea
mvua ya mawe. Ni wazi kuwa, kuna uwezekano wa baadhi ya watu wa kawaida
wasioelewa mambo wakadhani kwamba wapinzani hao wa Mtume walikuwa na haki, na
kwamba kulikuwepo na mambo walioyoyajua wapinzani hao ambao wao hawakuyajua,
kwa kutaka adhabu ya Mwenyezi Mungu iwateremkie kama msimamo wao huo ulikuwa
ni batili! Lakini ni wazi kuwa huo sio ukweli wa mambo. Kutokana na aya hii tunajifunza
kwamba:

1- Wakati mwingine kiburi, ukaidi na inadi humfikisha mwanadamu katika ukingo
wa yeye kutaka kujiangamiza mwenyewe.
2- Baadhi ya wapinzani wa Mtume walikuwa miongoni mwa Watu wa Kitabu
ambao pamoja na kumwamini Mwenyezi Mungu lakini hawakuwa tayari kuamini
Qur'ani Takatifu wala Uislamu.


Aya ya 33 inasema:

Lakini Mwenyezi Mungu hakuwa wa kuwaadhibu maadamu wewe (Nabii Muhammad)


umo pamoja nao (hapa Makka), wala Mwenyezi Mungu hakuwa wa kuwaadhibu pia hali
ya kuwa (baadhi yao wamesilimu) wanaomba msamaha.

Aya hii inaashiria neema ya Mtume kuwemo miongoni mwa watu na kusema kwamba,
Waislamu wameondolewa adhabu ya umati kwa kuwepo Mtume miongoni mwao. Kama
ambavyo kuhusiana na kuadhibiwa kwa kaumu ya Lut, Mwenyezi Mungu alimtaka
Mtume wake huyo aondoke katika mji ulimoshuka adhabu kabla ya kutokea adhabu hiyo,
nukta hii inasisitizwa katika riwaya kadhaa kwamba, Mwenyezi Mungu hujiepusha
kuteremsha adhabu ya wote katika maeneo ambako kuna watu wasafi waliotakasika. Ni
wazi kwamba, maisha ya Mtume na zama za maisha yake zilihusiana na kipindi maalumu
katika historia na jambo linalozuia kuteremka kwa adhabu hiyo katika kila zama na
sehemu, ni toba ambayo imesisitizwa sana katika aya hii. Wakati Mtume alipoaga na
kuondoka humu duniani, Imam Ali (AS) alisema: "Salama moja imeondoka miongoni
mwetu basi na tuilinde salama nyingine ambayo ni toba."

Tunajifunza yafuatayo kutokana na aya hii:

1- Kuwepo kwa mawalii wa Mwenyezi Mungu miongoni mwetu ni kinga na ngao
dhidi ya balaa na hutukinga na dhabu ya Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo, tunapasa
kuwaheshimu na kuwathamini.
2- Toba na maghfira si tu kwamba hutukinga na adhabu ya Akhera bali na ya
duniani pia na kwa hivyo hatupasi kughafilika nayo.


Darsa hii inaishia hapa. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …