Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 21 Aprili 2008 21:49

Suratul Anfal: Aya ya 26-29

Assalamu Alaykum Warahamatullahi Wabarakaatuh. Bismillahi. Shukrani na sifa njema
zote zinamstahikia Allah sw, Muumba wa kila kitu. Tunaendelea na darsa ya yetu ya
quran inayotoa tarjumi na maelezo kwa ufupi ya kitabu kitukufu cha quran, kulingana na
mpangilio wa sura zake. Katika darsa hii tunaanza na aya ya 26 ya Sura yetu ya al-
Anfaal:

Na kumbukeni (enyi Waislamu) mlipokuwa wachache, mkionekana madhaifu katika
ardhi; mkawa mnaogopa watu wasikunyakueni (kukuibeni); akakupeni mahala pazuri pa
kukaa (napo ni hapa Madina) na akakutieni nguvu kwa nusura yake, na akakupeni riziki
nzuri ili mpate kushukuru.

Kabla ya kuhijiri Mtume Mtukufu (SAW) kutoka Makka kwenda Madina, Waislamu
walikuwa daima wakipata udhia na mateso makubwa kutoka kwa washirikina wa mjini
Makka. Kwa hivyo, walishauriwa na Mtume wahajiri na kuhamia katika maeneo
mengine ya dunia ambako wangekuwa salama na kuishi kwa utulivu huko. Kundi moja
lilielekea Habasha yaani Ethiopia ya leo, jingine Yemen na mengine katika maeneo ya
Taif na Madina. Waislamu walioelekea Madina, hawakuwa na nyumba wala makazi na
waliishi katika hali ya umasikini kabisa. Aya hii inaashiria hali hiyo ngumu iliyowakabili
Waislamu mwanzoni mwa Uislamu walipofika Madina na kuwakumbusha kwamba,
katika hali hiyo, Mwenyezi Mungu aliwapa nguvu na uwezo mkubwa wa kuweza


kukabiliana na matatizo yaliyowakabili, na kwamba wanapaswa kumshukuru Mwenyezi
Mungu kwa neema hiyo kubwa na kuithamini kwa kila njia. Tunajifunza yafuatayo
kutokana na aya hii:

1- Hatupasi kuwa na hofu wala kuingiwa na woga kutokana na uchache wetu wala
uchache wa suhula tulizonazo. Hatupasi kuacha njia yetu ya haki na bila shaka
Mwenyezi Mungu atafidia upungufu wetu.
2- Hatupasi kusahau machungu na magumu tuliyoyapitia maishani na kumshukuru
Mwenyezi Mungu tunapopata faraja.


Aya ya 27 inasema:

Enyi Mlioamini! Msimfanyie Khiana Mwenyezi Mungu na Mtume (mkaacha kufuata
mlioamrishwa na mliokatazwa) wala msikhini amana zenu (mnazoaminiana wenyewe
kwa wenyewe); na hali mnajua (kuwa ni vibaya hivyo).

Kufuatia aya iliyotangulia inayozungumzia kipindi cha utawala wa Waislamu mjini
Madina, aya hii inawataka Waislamu wawe waangalifu sana na wasije wakadanganyika
na maslahi ya kimaada na ya humu duniani na hivyo kumfanyia hiana Mwenyezi
Mungu, Mtume wake na umma mzima wa Kiislamu.

Kwa mujibu wa riwaya za Kiislamu, katika mojawapo ya vita vilivyopiganwa kati ya
Waislamu na Mayahudi, Muislamu mmoja alifanya hiana na kuwafahamisha maadui wa
Kiyahudi mpango wa kushambuliwa na Waislamu. Baada ya kuvujisha habari hizo


Muislamu aliyefanya hiana hiyo hatimaye alijuta na kutubu kuhusiana na kosa alilofanya,
toba ambayo baadaye ilikubaliwa.

Kwa mtazamo wa utamaduni wa Kiislamu, amana ina maana pana ambayo inajumuisha
neema zote za kimaada na kimaanawi ambazo Mwenyezi Mungu amempa mwanadamu.
Hata mwili na roho ya mwanadamu ni neema kubwa ambazo amepewa na Mwenyezi
Mungu na wala hana ruhusa ya kuzichezea na kuzifanya atakavyo. Sheria na dini ya
Mwenyezi Mungu pia ni neema ambazo mwanadamu amepewa na Muumba wake na
anawajibika kuzilinda neema hizo kwa uwezo wake wote. Tunajifunza yafuatayo
kutokana na aya hii:

1- Imani inafungamana moja kwa moja na ulindaji amana na kupingana na hiana.
2- Ubaya wa hiana unafahamika na kila mmoja wetu na kwa hivyo kila hiana
inayofanyika kwa ufahamu kamili wa anayeifanya, huwa na matokeo mabaya na
hatari sana.


Aya ya 28 inasema:

 

 

Na jueni ya kwamba mali zenu na watoto wenu ni mtihani ( huo aliokupeni Mwenyezi
Mungu kutazama mtaendesha vipi) na jueni ya kwamba kwa Mwenyezi Mungu yako
malipo makuu (kabisa).

Katika kuendelea na aya iliyopita ambayo inaashiria onyo dhidi ya hiana, aya hii
inaashiria masuala mawili muhimu yanayopelekea kufanyika hiana. Inatuonya tusije
tukaufanyia hiana umma wa Kiislamu kwa lengo la kulinda mali zetu za humu duniani au


kwa madhumuni ya kuwafurahisha watoto wetu tu. Inatuonya dhidi ya kutanguliza na
kufadhilisha mali na watoto wetu juu ya maslahi ya umma wa Kiislamu. Sababu kuu
zinazopelekea kufanyika dhambi na hiana katika nyanja za kiuchumi na kijamii kama vile
kufanya ghashi, ulanguzi, kuacha kutoa khumsi na zaka, ushuhuda wa uongo kukimbia
kutoka kwenye medani ya vita na jihadi zinatokana na mvuto wa mali na watoto. Qur'ani
Takatifu inasema kwamba, mambo hayo mawili ndiyo yanayomplelekea mwanadamu
kuteleza na kutofikia malengo yake matukufu maishani. Kwa hivyo, tunapaswa kujilinda
kutokana na masuala hayo ili tusije tukatumbukia katika dhambi ya kuwafanyia hiana
wenzetu. Ni wazi kuwa, Mwenyezi Mungu atatupa jazaa kubwa pindi tutakapofanikiwa
kujiepusha na maovu hayo. Mali na watoto vimetajwa kwa pamoja katika aya tano za
Qur'ani Takatifu kuwa mambo yanayomtelezesha mwanadamu maishani:

Tunajifunza kutokana na aya hiyo kwamba:

1- Tamaa kubwa na ya kupindukia ya mali na watoto, humuelekeza mwanadamu kwenye
maovu na hiana, la sivyo, hamu ya kawaida kuhusiana na vitu viwili hivi ni jambo la
kawaida kabisa na aliloumbwa nalo mwanadamu.

2- Mali na watoto, pamoja na uzuri wote vilionavyo, havina thamani yoyote mbele ya
neema nyingine nyingi alizotupa Mwenyezi Mungu na kwa hivyo, havipasi kutuweka
mbali naye.

Sasa tunategea sikio aya ya 29 ya Surat al-Anfaal:

 

 


Enyi mlioamini! Mkimcha Mwenyezi Mungu atakupeni tamyizi ya kupambanua baina ya
haki na batili na atakufutieni makosa yenu na kukusameheni. Na Mwenyezi Mungu ni
mwenye fadhila kubwa kabisa.

Aya hii inasema kwamba, siri ya kufanikiwa mwanadamu humu duniani ni uchaji Mungu
na kujiepusha na maovu. Inatwambia kwamba, mja hupata neema nyingi kutoka kwa
Mwenyezi Mungu kwa kutekeleza maamrisho na kujiepusha na makatazo yake.
Mwenyezi Mungu humpa hekima na uoni mpana mja wake anayepambanua vyema haki
kutokana na batili na kutohadaika na upotofu. Watu kama hao wanapofanya makosa kwa
kutojua, Mwenyezi Mungu huwasamehe dhambi zao na hata kufunika aibu na makosa
yao kwa sababu huwa wameazimia kufuata njia ya haki. Neema hizi zote zinatokana na
ukweli kwamba, Mwenyezi Mungu huamiliana kwa fadhila kubwa na waja wake wema,
fadhila ambazo kwa hakika hazina mwisho.

Tunajifunza yafuatayo kutokana na aya hii:

1- Matendo ya mwanadamu huwa na athahri kubwa katika fikra na mtazamo wake.
Kama ambavyo fikra huwa na athari muhimu katika matendo ya mwanadamu,
takwa huwa na nafasi muhimu katika kuainisha fikra na muelekeo wake.
2- Takwa hulinda na kumkinga mwanadamu asikosee katika matendo yake na
vilevile kumlinda asije akatumbukia katika moto wa Jahannam.


Darsa hii inaishia hapa, Wassalamu Alaykum Warahamtullahi Wabarakaatuh

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …