Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 21 Aprili 2008 21:46

Suratul Anfal: Aya ya 15-21

Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Bismillahi Rahmani Rahiim
Shukrani na sifa zote njema zinamstahikia Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa neema zote
alizotuneemesha, tunazozijua na zile tusizozijua. Katika darsa hii tutaanza kuizungumzia
sura ya nane ya quran tukufu yenye jina la al Anfal.
Katika mfululizo huu tutatupia jicho yale yaliyomo kwenye aya zake 7 tukianza na aya za
15 na 16 ambazo zinasema:


Enyi mlioamini! Mkutanapo vitani na wale waliokufuru basi msiwageuzie migongo
mkakimbia.
Na atakayewageuzia mgongo wake siku hiyo -isipokuwa amegeuka kwa kushambulia au
amegeuka akaungane na sehemu nyigine za jeshi hili hili la Waislamu-(ikiwa si hivyo)
atastahiki ghadhabu ya Mwenyezi Mungu; na mahala pake ni Jahannam. Napo ni mahali
pabaya pa kurudia (mtu).


Katika darsa kadhaa zilizopita tumekuwa tukizisoma aya zinazozungumzia vita vya Badr.
Zikiendelea kuizungumzia maudhui hiyo hiyo aya hizi za 15 na 16 zinaashiria nidhamu


maalumu wanayotakiwa kuwa nayo wapiganaji wa jeshi la Kiislamu katika uwanja wa
mapambano na kueleza kwamba haifai wala haijuzu wakati wowote ule waislamu
kukimbia na kurudi nyuma katika uwanja wa vita hata kama idadi ya maadui itakuwa
kubwa kiasi gani; ila pale kama kufanya hivyo kutakuwa na lengo la kujizatiti upya kwa
zana na silaha au kujiunga na safu nyengine ya jeshi la Kiislamu kwa ajili ya kufanya
shambulio la pamoja dhidi ya adui. Baadhi ya yale tunayojifunza kutokana na aya hizi ni
kuwa kukimbia katika medani ya Jihadi ni moja kati ya madhambi makubwa, na mwenye
kutenda hilo ataandamwa na ghadhabu za Mwenyezi Mungu. Aidha tunajifunza kuwa
inajuzu kwa jeshi la Kiislamu kurudi nyuma kimbinu kwa lengo la kumhadaa adui.
Halikadhalika aya inatuelimisha kuwa kitendo cha kukimbia katika uwanja wa vita vya
Jihadi vya kunusuru dini ya Mwenyezi Mungu humfanya mtu apate idhlali ya hapa
duniani na vile vile adhabu ya huko akhera .
Zifuatazo sasa ni aya za 17 na 18 ambazo zinasema :


Hamkuwaua nyinyi lakini Mwenyezi Mungu ndiye aliyewaua; na hukutupa wewe (Mtume
ule mchanga) ulipotupa walakini Mwenyezi Mungu ndiye aliyeutupa. Alifanya haya
Mwenyezi Mungu ili awape walioamini hidaya nzuri itokayo kwake. Hakika Mwenyezi
Mungu ndiye asikiaye na ajuaye.


Basi haya (mumefanyiwa safari hii). Na hakika Mwenyezi Mungu atazidhoofisha nguvu
za makafiri.

Zikiendelea kutoa somo lenye mazingatio makubwa kuhusiana na yale yaliyojiri siku ya
vita vya Badr, aya hizi tulizosoma hivi punde zinawaasa na kuwatahadharisha waislamu
wasije wakaingiwa na ghururi na kudhani kwamba ni nguvu na uwezo wa kijeshi tu
waliokuwa nao katika uwanja wa vita ndio uliowafanya washinde; na hivyo
kuwabainishia kwamba ulikuwa ni msaada wa ghaibu kutoka kwa Mola wenu ndio
uliochangia pia kuwasambaratisha na kuwaangamiza makafiri, na si mishale, mikuki au
panga zenu tu. Sababu ni kwamba alikuwa ni Mwenyezi Mungu sw ndiye aliyeziwezesha
panga na mishale yenu kuwa na shabaha nzuri ya kuwalenga maadui zenu, na kwa hakika
yaliyojiri siku hiyo katika uwanja wa Badr ulikuwa ni mtihani na majaribu ya Allah ya
kuwapima waislamu imani zao. Na je kuna mtihani mkubwa zaidi ya ule wa kumjua yule
aliye tayari kutoa muhanga damu yake na roho yake kwa ajili ya dini ya Allah. Aya
zinaendelea kwa kuwataka waislamu watambue kuwa kuna wakati mitihani na majaribu
ya Mwenyezi Mungu inakuwa ni ya kupata neema na ushindi, hali inayojulikana kama
mtihani wa habari njema; na wakati mwengine mtihani huo huambatana na misiba na
mashaka na kujulikana kama mtihani wa habari mbaya. Miongoni mwa mambo ya
kuzingatia katika aya hizi ni kuwa vita hasa vya Jihadi ni mojawapo ya njia za
kutahiniwa waislamu ili waweze kupambanuka wale walio na imani thabiti na wale
wenye imani dhaifu. Nukta nyengine ya kuzingatiwa hapa ni kuwa lolote analotenda
mwanaadamu hunasibishwa na yeye mweyewe kuwa ndiye mtendaji kutokana na
kulitenda hilo kwa hiyari yake mwenyewe. Hata hivyo kwa kuwa nguvu za kutendea
jambo hilo hazipati kwa mwengine isipokuwa Mwenyezi Mungu sw ndiyo maana


mwanaadamu hawezi kujihesabu kuwa kila afanyalo linatokana na matakwa yake
mwenyewe tu pasina kuwepo irada ya Allah sw. Aidha aya zinatuonyesha kuwa
Mwenyezi Mungu siku zote ni mwenye kuwapa nusra na msaada wale waumini wa kweli
na yeye pia ndiye mzimaji wa njama za maadui wa dini yake ya haki. Tunaiendeleza
darsa yetu kwa aya ya 19 ambayo inasema:


Kama mnataka hukumu basi hukumu imekwisha kufikieni. Na kama mkijizuia basi
itakuwa bora kwenu. Na kama mtarudia na Sisi pia tutarudia. Na watu wenu
hawatakufaeni cho chote hata wakiwa wengi. Na Mwenyezi Mungu yu pamoja na
wanaoamini.

Baadhi ya wafasiri wa quran wamesema, baada ya kupata ushindi dhidi ya maadui zao
wa Kikureishi, Waislamu walianza kuzozana juu ya ngawira, yaani mali zilizopatikana
katika vita na hata wakafikia kubishana na Bwana Mtume saw juu ya suala hilo. Hivyo
kwa mtazamo wa wafasiri hao aya hii inawahutubu waislamu hao. Lakini wafasiri walio
wengi zaidi wanasema ni makfiri na mushirikina ndio waliosemezwa katika aya hii. Alaa
kulli haal kinachoelezwa katika aya hii ni kuwa ushindi ndio huo umewaendea Waislamu
na hivyo Mwenyezi Mungu ameshaifanya haki ibainike wazi. Hivyo wasemezwa wa aya
liwe lolote kati ya makundi mawili ya Waislamu au Makafiri al muhimu ni kwamba
kitendo cha kubishana na Bwana Mtume na kulalamikia amri yake hakitakuwa na
matokeo mengine ghairi ya kushukiwa na ghadhabu za Mwenyezi Mungu. Na


hakutakuwa na mtu au kundi lolote la watu watakaoweza kumlinda mtu na adhabu ya
Mwenyezi Mungu iliyokwisha hukumiwa imshukie. Baadhi ya mafunzo tunayoyapata
kutokana na aya hii ni kuwa lenye kheri na mwanaadamu na hasa muislamu ni kujiepusha
na tabia ya kukhalifu amri za Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Vile vile aya
inatufunza kuwa imani ya kweli ndilo sharti la kumfanya mtu apate nusra na msaada wa
Mwenyezi Mungu, kama ambavyo wingi wa watu hauwezi kuwa na athari yoyote ya
kuweza kuzuia ghadhabu na adhabu ya Allah isimshukie mtu.
Aya za 20 na 21 za sura yetu ya Anfal ndizo zinazotuhatimishia darsa yetu ya juma hili.
Aya hizo zinasema:


Enyi mlioamini! Mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na wala msijiepushe naye na
hali mnasikia.
Na wala msiwe kama wale wanaosema: "Tumesikia (tumetii) na kumbe hawasikii (yaani
hawatii chochote).


Katika sehemu ya mwisho ya mjumuiko wa aya hizi quran tukufu inawataka waislamu
wayatii kikamilifu maamrisho ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake na kujiweka mbali
kabisa na maasi kwa kutokhalifu maamrisho hayo. Aya zinasema nyinyi waislamu ambao
mnayasikia vema maneno ya Mtume hali ya kuwa mumemuamini, jiepusheni kabisa na


tabia ya kukaidi mafundisho yake, kwani sharti la kukamilika imani ya muislamu juu ya
Mwenyezi Mungu ni kumtii Mtume wake, vinginevyo nyinyi pia mutakuwa sawa na
wale wanaosema kwa ndimi zao tu kwamba tumeyasikia maneno ya Mtume na
tumeyakubali ilhali matendo yao hayaonyeshi athari yoyote ya kuwa kweli
wameyakubali maneno hayo ya mjumbe wa Mwenyezi Mungu. Miongoni mwa mambo
tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kuwa, pamoja na mtu kusema kwamba yu
muislamu, lakini bado wakati wowote ule anaweza akakhalifu kutekeleza maamrisho ya
dini; hivyo basi mawaidha ya maonyo ni mambo anayoyahitajia mtu kila wakati. Jengine
tunalojifunza hapa ni kuwa pale mtu anapoisikia na kuitambua haki basi ajue kuwa tayari
ameshakuwa na dhima na jukumu mbele ya Mola wake, na wala hatoweza kuja kujitetea
kwa kisingizio cha kutojua. Na pia aya zinatutaka tuelewe kwamba imani si majisifu na
kujidai mtu kuwa ni muislamu au muumini wa kweli, bali imani hasa ni ile ya matendo
na utiifu wa kweli kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Darsa ya 263 inaishia hapa.
Tunamwomba Mwenyezi Mungu atujaalie kuwa miongoni mwa waislamu wenye imani
ya kweli inayoambatana na amali njema na si waislamu wa majina tu wa kujikweza na
kujivuna.../

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …