Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 21 Aprili 2008 21:45

Suratul Anfal: Aya ya 10-14

Assalamu Alaykum Warahamatullahi Wabarakaatuh. Bismillahi. Shukrani na sifa njema
zote zinamstahikia Allah sw, Muumba wa kila kitu Tunaendelea na darsa ya yetu ya
quran inayotoa tarjumi na maelezo kwa ufupi ya kitabu kitukufu cha quran, kulingana na
mpangilio wa sura zake. Katika mfululizo huu tutatoa tarjumi na maelezo ya aya 5 ya
sura hii tunayoendelea kuizungumzia ya Anfal tukianza na aya yake ya 10 ambayo
inasema:


Na Mwenyezi Mungu hakufanya haya ila iwe bishara (yaani habari ya furaha) na ili
nyoyo zenu zitue kwayo. Na hakuna msaada (wa kufaa) ila utokao kwa Mwenyezi Mungu.
Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima.

Katika darsa iliyopita tulisema kuwa katika vita vya kwanza kabisa walivyopigana
waislamu na mushirikina wa kikureishi yaani vita vya Badr, Mwenyezi Mungu mtukufu
aliteremsha malaika ili kuzitia mori na motisha nyoyo za wapiganaji wa kiislamu, na
ndiyo maana waislamu, pamoja na kuwa na jeshi dogo na silaha duni za kivita, waliweza
kulishinda jeshi kubwa la makafiri lililokuwa limejizatiti kwa silaha imara. Katika aya hii
ya 10 tuliyoisoma Mwenyezi Mungu anasema kuteremka malaika katika vita vya Badr
hakukuwa na maana ya kushuka na silaha mkononi na kupambana na adui bali ilikuwa ni
kuzitia nguvu na moyo wa matumaini ya ushindi nyonyo zenu, na kwa hakika ni
matumaini hayo yaliyojengeka kwa yakini ndani ya nyoyo zenu ndiyo yaliyokupeni nusra
ya ushindi. Miongoni mwa mafunzo tunayoyapata kutokana na aya hii ni kuwa bishara


njema zinazotolewa na Allah huzitia nguvu nyoyo za wapiganaji wa Kiislamu na
kuwafanya wapate ushindi katika vita vya Jihadi. Funzo jengine tunalolipata hapa kama
tulivyowahi kusema katika darsa iliyopita ni kuwa ushindi dhidi ya adui hautegemei
silaha na uwezo wa kijeshi tu bali unahitajia pia nusra na msaada wa Mwenyezi Mungu
Mtukufu.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 11 ambayo inasema:


(Kumbukeni) alipokuleteeni usingizi uliokuwa (alama ya) salama itokayo kwake, na
akakuteremshieni maji mawinguni ili kukutahirisheni kwayo na kukuondoleeni uchafu wa
shetani na kuzipa nguvu nyoyo zenu kuithubutisha miguu yenu chini (isiwe inazamazama
mchangani).

Kama mapokezi ya taarikh yaani historia ya uislamu yanavyoeleza ni kwamba awali
wakati jeshi la waislamu lilipoliona jeshi kubwa la makafiri wa Kikureishi huko katika
eneo la Badr lilifadhaika na kuemewa kidogo. Na ndipo katika aya tuliyoisoma
Mwenyezi Mungu akasema tulikupeni utulivu wa moyo ili muweze kupumzika vizuri
usiku wa kuamkia vita na kuiondoa kabisa hali ya kiwewe na khofu iliyokuwa
imejengeka ndani ya nyoyo zenu. Si hayo tu lakini pia tuliteremsha mvua ambayo
kwanza ilikidhi mahitaji yenu ya matumizi ya kunywa na mengineyo na vile vile iliifanya
ardhi ya mchanga unaopeperuka ya jangwa la Badr iwe tifutifu, hali ambayo ilikuwa na
faida kwenu. Lakini pia rasharasha hizo za mvua zilikupeni hali maalumu ya uchangamfu


na kukuwekeni tayari kwa vita pamoja na kukutoeni kila aina ya wasiwasi wa shetani juu
ya kushindwa katika vita hivyo. Miongoni mwa nukta za kuzingatiwa katika aya hii ni
kuwa kama mtu atakuwa na subra na imani ya kweli juu ya Allah, Mola naye huvijaalia
hata vitu vya kimaumbile vifanye kazi ya usaidizi kwa mtu huyo. Halikadhalika
tunajifunza kutokana na aya hii kuwa sambamba na usafi wa nje na wa kimwili muislamu
anatakiwa azingatie sana usafi na utakasifu wa ndani ya nafsi ambao ndio unaomkinga na
shari ya wasiwasi wa shetani.
Ifuatayo sasa ni aya ya 12 ambayo inasema:


(Kumbukeni) Mola wako alipowafunulia Malaika (akawaambia): "Hakika Mimi ni
pamoja nanyi, basi watieni nguvu wale walioamini; nitatia woga katika nyoyo za
makafiri. Basi wapigeni juu ya shingo (zao) na kateni kila ncha za vidole vyao".

Ikiendeleza yale yaliyozungumziwa katika aya iliyotangulia juu ya msaada wa Allah
katika vita vya Badr, aya hii ya 12 inasema, wakati Mwenyezi Mungu alipowateremsha
malaika ili kwenda kuzitia nguvu na motisha nyoyo za wapiganaji wa jeshi la kiislamu
aliwafunulia malaika hao kuwa mimi niko pamoja nanyi katika kulipa nguvu kundi la
waumini; hivyo kama ninavyowapa wao bishara na matumaini ya ushindi nazitia pia
nyoyo za makafiri khofu na woga. Pamoja na hayo si mimi wa kuwaangamiza moja kwa
moja makafiri hao, bali ni nyinyi waislamu wenyewe ndio wa kuingia kwenye uwanja wa
mapambano, na kwa nguvu na uwezo wenu wote muzikate kwa panga zenu shingo na


vichwa vya makafiri au muilenge mikono na miguu yao wasiweze tena kushika silaha na
kupigana na kukimbia huku na huko. Baadhi ya mafunzo tunayoyapata kutokana na aya
hii ni kuwa kama tutakuwa waislamu wa kweli basi Mwenyezi Mungu atazipa utulivu
nyoyo zetu na kuzitia khofu na mfadhaiko nyoyo za maadui zetu. Funzo jengine
tunalolipata hapa ni kuwa kama tutasimama kiume kukabiliana na adui basi tujue kuwa
nusra na msaada wa Allah utatushukia. Lakini sio tuwe watu wa kufikiria namna ya
kuokoa maisha yetu tu badala ya kuinusuru dini ya Mwenyezi Mungu kisha tutegemee
Mwenyezi Mungu atunusuru na kuwaangamiza maadui zetu.
Darsa hii ya quran inahitimishwa na aya za 13 na 14 ambazo zinasema:


Hayo ni kwa sababu wamemuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na mwenye kumuasi
Mwenyezi Mungu na Mtume wake (atamuadhibisha) kwani Mwenyezi Mungu ni mkali wa
kuadhibu.
Basi ionjeni (adhabu hiyo ya kuuawa hivyo na kutekwa hivyo). Na bila shaka makafiri
wana adhabu (nyingine) ya moto ( inawangojea Akhera).

Aya hii inalitaja shambulio la waislamu dhidi ya makafiri katika vita vya Badr kama ni
aina fulani ya adhabu kwa maadui hao wa Allah na kueleza kuwa watu hao ilikuwa ni
kawaida yao kuzipinga na kuzikataa aya za Mwenyezi Mungu na maneno ya Mtume
wake na kufikia hadi ya kutokuwa tayari hata ile kuyasikiliza tu maneno ya haki. Hivyo


ili kuwaadhibu, Allah sw aliwapa nguvu na nusra waislamu ili wawaangamize makafiri
hao na kulishinda jeshi lao. Hiyo ikiwa ni adhabu ya hapa duniani, na huko akhera
wameshaandaliwa adhabu kali ya moto wa jahannam. Miongoni mwa mambo ya
kuzingatiwa katika aya hizi ni kuwa adhabu na ghadhabu za Mwenyezi Mungu hazimpati
mja bure bure na bila sababu, bali huwa ni matokeo ya kuasi na kukhalifu amri za Mola
wake. Aidha tunajifunza kutokana na aya hizi kuwa suna na utaratibu uliowekwa na
Allah ni kwamba yeyote atakayekamia kuizima nuru ya haki ajue kwamba mwishowe
ataangamia tu. Darsa yetu hii inaishia hapa. Tunamwomba Allah aupe izza na nguvu
uislamu na waislamu na aidhalilishe shirki na mushirikina na awaangamize maadui wa
dini yake tukufu. amin..../

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …