Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 21 Aprili 2008 21:44

Suratul Anfal: Aya ya 5-9

Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Bismillahi Rahmani Rahiim. Hii
darsa ya quran, inayotoa tarjumi na maelezo kwa ufupi ya sura za quran tukufu kwa
kuzingatia mpangilio wa sura hizo ndani ya Mas-haf. Katika mfululizo huu
tutaendelea na tarjumi na maelezo ya sura ya nane ya al Anfal tukianza na aya ya 5 na
ya 6 ambazo zinasema:


(Atakunusuru) kama alivyokutoa Mola wako katika nyumba yako kwa haki, na kundi
moja la walioamini halipendi (utoke).
Wakabishana nawe katika (lile jambo la) haki baada ya kubainika (haki ile;
wanachukiwa kwenda huko vitani) kama kwamba wanasukumwa katika mauti na
huku wanaona.


Aya hizi zinazungumzia vita vya Badr vilivyopiganwa katika mwaka wa pili Hijria.
Ni kwamba Bwana Mtume Muhammad saw alipata taarifa kuwa msafara mkubwa wa
biashara wa makafiri wa Kikureishi ukiongozwa na Abu Sufyan uko njiani kuelekea
Makka. Hapo aliwaamuru Masahaba zake waufuate msafara huo ili kutoa pigo la
kiuchumi kwa adui na pia kuzirejesha mikononi mwa Waislamu mali za Muhajirina
yaani Waislamu waliohama Makka na kuhamia Madina ambazo zilikuwa zimeporwa
na kunyakuliwa na Makureishi hao. Hata hivyo Abu Sufyan naye alipata khabari


kuwa kuna kundi la Waislamu wanaofuata msafara wake; hivyo kwanza
akawafikishia khabari hiyo Makafiri wenzake wa Kikureishi huko Makka na kisha
akageuza njia ya msafara wake huo. Ilipofika khabari hiyo huko Makka Makuresihi
waliandaa jeshi kubwa la wapiganaji wapatao elfu moja, kamanda wake akiwa ni Abu
Jahl, ambalo liliondoka huko Makka ili kulifuata jeshi la Waislamu. Jeshi hilo
lilielekea eneo lenye visima vya maji la Badr katika uwanda ulioko baina ya Makka
na Madina. Bwana Mtume aliwakusanya Masahaba zake ili kushauriana nao kama
waufuate msafara wa biashara wa Abu Sufyan au wakabiliane na jeshi lililojizatiti la
Makafiri. Kwa kuzingatia kuwa Waislamu hawakuwa wameondoka Madina kwa
lengo la kupigana vita, na kwa kutilia maanani kuwa kiidadi jeshi la Makuresihi
lilikuwa kubwa mara tatu zaidi kulinganisha na lile la Waislamu, baadhi ya Masahaba
hawakulipendelea shauri la kuingia vitani badala ya kuufuata msafara wa biashara.
Hivyo walifikia hata hadi ya kujadiliana na kubishana na Bwana Mtume juu ya suala
hilo; lakini kwa kuwa masahaba wengi waliunga mkono shauri la kuingia vitani
Bwana Mtume aliamua kukabiliana na jeshi la makafiri. Vita vya Badr vilipiganwa,
na kwa msaada wa Allah jeshi la Waislamu likalishinda jeshi la Makafiri. Abu Jahl ,
aliyekuwa jemadari wa jeshi hilo la Makureishi, na Makafiri wenzake sabini
waliuawa na wengine sabini walikamatwa mateka, wakati ambapo ni waislamu 14 tu
ndio waliouawa shahidi. Sehemu ya aya tulizozisoma inasema kundi moja miongoni
mwa Waislamu, pamoja na kwamba lilikuwa limemuamini Mwenyezi Mungu na
Mtume wake, lakini pale ilipofikia suala la kujitoa muhanga maisha na kuihami dini
ya Mwenyezi Mungu walitetereka na hata wakafikia hadi ya kubishana na Bwana
Mtume juu ya suala la kuingia vitani. Miongoni mwa mafunzo tunayoyapata kutokana
na aya hizi ni kuwa kupigana Jihadi dhidi ya maadui wa dini ya Mwenyezi Mungu ni
katika wajibu mkubwa wa kidini unaodhihirisha imani ya kweli aliyonayo Muislamu,


ijapokuwa kimaumbile binaadamu huchukizwa na mambo ya umwagaji damu, vita na
mapigano. Funzo jengine tunalolipata kutokana na aya hizi ni kuwa waislamu waoga
wasio na imani thabiti sio tu hawawi tayari kushiriki katika Jihadi lakini pia hufikia
hata hadi ya kubishana na kupingana na viongozi wa dini juu ya suala hilo.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa kuzitegea sikio aya za 7 na 8 ambazo zinasema:


Na (kumbukeni) Mwenyezi Mungu alipokuahidini moja katika mataifa mawili ya
kwamba ni lenu. Nanyi mkapenda mupate lile lisilo na nguvu; na Mwenyezi Mungu
anapenda kuthubutisha haki kwa maneno yake na kuikata mizizi ya makafiri.
Ili kuthubutisha haki na kuiondoa batili; hata wakichukia watu wabaya.

Aya hizi zinawahutubu waislamu na kuwaambia kuwa ijapokuwa mulifunga safari ya
kuufuata msafara wa Makureishi kwa matumaini ya kuzitia mkononi mali za maadui
na wala hamukutarajia kuwa mtalazimika kukabiliana na jeshi la vita, lakini lengo la
Mwenyezi Mungu la kukutakeni nyinyi mtoke kwenda huko ni kutaka kuipa nguvu
haki na kuitokomeza batili, ili iweze kuthibiti ile suna na ahadi yake kwamba haki
siku zote ndiyo hatimaye yenye kushinda, na mwisho wa batili ni kutoweka. Tabaan
hadi sasa takwa hilo la Allah halijathibiti kikamilifu na hivyo hutokea baadhi ya
wakati Waislamu wakashinda na wakati mwengine wakashindwa; lakini kwa mujibu
wa Quran na Hadithi itakapofika akhiri zaman, wakati atakapodhihiri Imam Mahdi


Ajjalallahu taala farajahu sharif, ahadi hiyo ya Allah itathibiti kikamilifu, tena basi
kwa ulimwengu mzima, ambapo haki na uadilifu vitatawala na dhulma na batili kwa
jumla vitatoweka. Baadhi ya nukta zenye mafunzo tunazozipata kutokana na aya hizi
ni kuwa ushindi kwa mtazamo wa Uislamu haupatikani kwa kuwa na jeshi kubwa la
wapiganaji na kujizatiti kwa zana na silaha za kisasa tu, bali sababu za kiroho na
kimaanawi pia zinachangia katika ushindi huo ikiwemo imani na moyo wa muumini
mwenyewe pamoja na msaada wa ghaibu wa Allah sw. Nukta nyengine ya
kuzingatiwa hapa ni kuwa lengo la Jihadi katika Uislamu ni kusimamisha haki na
kuondoa batili na wala si kupanua jografia ya kiislamu na kujikusanyia ngawira.
Aidha kutokana na aya hizi tunajifunza kuwa tusitarajie kuwa tutaweza kupigania
haki bila kuwafanya maadui wakasirike. Kwani kusimama na kutawala haki maana
yake ni kughadhibika na kuchukizwa makafiri na waovu.
Darsa yetu inahitimishwa na aya ya 9 ambayo inasema:


(Kumbukeni) mlipokuwa mkiomba msaada kwa Mola wenu, naye akakujibuni kuwa:"
Kwa yakini Mimi nitakusaidieni kwa Malaika elfu moja watakaofuatana
mfululizo(wanaongezeka tu)".

Aya hii tukufu inabainisha wazi wazi juu ya kuwateremkia waislamu msaada wa
ghaibu katika vita vya Badr, msaada ambao ulikuwa ni wa kushuka Malaika. Katika
aya hii kunaashiriwa kushuka kwa malaika elfu moja ambapo katika aya ya 124 na
125 za suratu ali Imran imeashiriwa idadi ya Malaika elfu tatu na elfu tano, hali
inayomaanisha kwamba idadi tofauti ya Malaika walishuka katika lahadha tofauti za
vita hivyo. Tabaan ni wazi kwamba Malaika hao hawakuingia vitani na kupambana


moja kwa moja na jeshi la Makafiri wa Kikureishi; lakini kuwepo kwao katika uwanja
wa mapambano kando ya wapiganaji wa Kiislamu kuliimarisha moyo wa mapambano
na kuongeza imani ya wapiganaji hao na pia kuliwatia khofu na kiwewe wapiganaji
wa jeshi la makafiri. Aya hii pia inatilia mkazo nafasi ya dua katika vita na kueleza
kwamba siri ya mafanikio na ushindi wa waislamu katika vita vya Badr ilikuwa ni
kule kunyenyekea na kumuomba kwao Allah kwa khushuu na kuitikiwa dua yao hiyo.
Miongoni mwa mambo tunayojifunza kutokana na aya hii ni kuwa pamoja na
kwamba Mwenyezi Mungu anaweza kumtunuku na kumruzuku mja wake bila hata
kumuomba, lakini kwa waumini, dua humuinua daraja yake mja na kumweka katika
hali bora zaidi ya kupokea atia na neema zake Allah na vile vile kuijenga na kuikuza
kiroho nafsi ya muumini huyo. Funzo jengine tunalolipata kutokana na aya hii ni
kuwa Malaika ni viumbe wenye nafasi malumu katika maisha ya watu na ni imani juu
ya Allah aliyonayo muislamu ndiyo inayowafanya viumbe hao wateule wawe karibu
na muislamu huyo. Halikadhalika tunabainikiwa hapa kuwa msaada wa ghaibu kutoka
mbinguni humshukia mtu pale kwanza yeye mwenyewe anapofanya jitihada na kisha
akadhihirisha kwa ikhlasi kuwa yu muhitaji kwa Mola na anategemea msaada wake
yeye tu. Darsa hii ya quran tukufu inaishia hapa. Tuifunge darsa yetu kwa kumwomba
Allah atujaalie kuwa waislamu wa kweli kiimani na kimatendo na wastahili wa kupata
msaada wake wa ghaibu katika kuisimamisha kalimatu tauhiid ya Lailaha illa llah...../

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …