Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 21 Aprili 2008 21:42

Suratul Anfal: Aya ya 1-4

Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Bismillahi Rahmani Rahiim
Shukrani na sifa zote njema zinamstahikia Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa neema zote
alizotuneemesha, tunazozijua na zile tusizozijua. Katika darsa hii tutaanza kuizungumzia
sura ya nane ya quran tukufu yenye jina la al Anfal.
Suratul Anfal iliteremshwa Madina na ina jumla ya aya 75. Katika darsa yetu hii ya
kwanza kuzungumzia sura hiyo tutaangazia yale yaliyomo kwenye aya zake nne tukianza
na aya ya kwanza ambayo inasema:


Wanakuuliza juu ya (mali iliyotekwa ya) ngawira (igaiwe vipi)? Sema: " Mali iliyotekwa
ni ya Mwenyezi Mungu na Mtume (fuateni watakavyokugawieni). Basi muogopeni
Mwenyezi Mungu na suluhisheni mambo baina yenu, na mtiini Mwenyezi Mungu na
Mtume wake ikiwa nyinyi ni katika wanaoamini (kweli).

Katika mwaka wa pili Hijria tangu pale Bwana Mtume Muhammad saw alipohama
Makka na kuhajiri kwa kuhamia Madina vilipiganwa vita katika eneo liitwalo Badr
ambapo Waislamu walipata ushindi pamoja na ngawira chungu nzima. Kufuatia hali hiyo
Waislamu walimuendea Bwana Mtume na kumuuliza namna ya kuzigawa ngawira hizo.
Naye Bwana Mtume akasubiri jibu la suali hilo kutoka mbinguni hadi pale
ilipoteremshwa aya ya kwanza tuliyoisoma, ya sura hii ya Anfal ambayo iliweka bayana
kwamba mamlaka ya ugawaji ngawira yako mikononi mwa mtukufu huyo. Katika
ugawaji wa ngawira, kinyume na mfumo wa kibaguzi uliokuwa umezoeleka kwa


waarabu, Bwana Mtume aligawa ngawira hizo mafungu sawa kwa wapiganaji wote wa
jeshi la Kiislamu ili kufuta ubaguzi usio na msingi uliokuwa umerithiwa tokea zama za
ujahiliya.
Tabaan neno Anfal mbali ya kuwa na maana ya ngawira au ghanima yaani mali
inayopatikana katika vita, linatumika pia kwa aina yoyote ile ya mali ya umma au
maliasili kama vile misitu na madini ambavyo vyote hivyo mamlaka yake yako mikononi
mwa Bwana Mtume na wale walio warithi wa nafasi yake kiuongozi. Hivyo mwishoni
mwa aya hii waislamu wanausiwa waikubali hukumu inayotolewa na Bwana Mtume saw
kwa kuambiwa: "Kama kweli mmeamini, basi mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake.
Aya hii aidha imeashiria suala la waislamu kutengeneza na kusawazisha mambo baina
yao na kueleza kwamba msiruhusu masuala ya mali na ya kidunia yasababishe
mparaganyiko na mgawanyiko baina yenu na kuwasha moto wa chuki, husuda na
uhasama ndani ya nyoyo zenu; bali mcheni Mwenyezi Mungu kwa kujiweka mbali na
matamanio ya nafsi na ya shetani, huku muda wote mukijenga hali ya masikilizano,
amani na upendo kati yenu. Baadhi ya mafunzo tunayoyapata kutokana na aya hii ni
kuwa Uislamu ni dini ya kijamii na kiuchumi kwani ina mfumo na ratiba maalumu kwa
ajili ya masuala ya kiuchumi ya jamii. Na hivyo waislamu wanatakiwa waifanye Quran
na Bwana Mtume saw kuwa ndio marejeo yao kwa ajili ya masuala yao ya kiuchumi.
Funzo jengine tunalolipata kutokana na aya hii ni kuwa ijapokuwa mafundisho ya
kiislamu yanawataka waumini wawe wakali na wasio na mzaha kwa maadui, lakini
wakati huo huo yanawausia waamiliane wenyewe kwa wenyewe kwa upole na upendo.
Halikadhalika tunajifunza kutokana na aya hii kuwa sharti mojawapo la imani ya kweli ni
kutii na kunyenyekea amri ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake.


Tunaiendeleza darsa yetu kwa kuitegea sikio aya ya pili na aya tatu ambazo zinasema:

 

Hakika waumini wa kweli ni wale ambao anapotajwa Mwenyezi Mungu nyoyo zao hujaa
khofu; na wanaposomewa Aya zake huwazidishia imani, na wakamtegemea Mola wao tu
basi.
Ambao wanasimamisha sala na wanatoa katika yale tuliyowapa.
Zikiendeleza yale yaliyokuja katika aya ya kwanza juu ya masharti ya imani, aya hizi
zinafafanua sifa za waumini na waislamu wa kweli kwa kusema, hao ni wale watu ambao
nyoyo zao hujawa na khofu na kupata mtikisiko maalumu pale linapotajwa jina tukufu la
Mwenyezi Mungu, na pia wanaposoma au kusomewa aya tukufu za quran basi imani zao
huongezeka.Utambuzi wao wa kuilelewa barabara adhama ya Mwenyezi Mungu
huwafanya wale waislamu wa kweli wawe wanyenyekevu na wenye khushuu kwa Mola
wao. Watu hao huwa hawako tayari kumuelekea na kumnyenyekea yeyote mwengine
ghairi ya yeye Allah sw. Kwa hakika khofu ya adhabu kali ya Mwenyezi Mungu
huutetemesha moyo wa muislamu wa kweli kama ambavyo pale anapozifikiria rehma
zisizo na kikomo za Mola Karima hupata utulivu usioelezeka. Hali hiyo anayokuwa nayo
muumini huwa ni sawa na ya mtoto mdogo kuhusiana na wazazi wake ambaye huwa na


khofu maalumu kwao ya kutowafanyia utovu wa adabu lakini wakati huo huo hujidekeza
kwao kutokana na mapenzi yao kwake. Hali tuliyoizungumzia ya kiroho juu ya khofu na
utulivu anaouhisi muumini, inahusu hali yake ya ndani ya nafsi, ama kwa upande wa hali
yake ya nje muumini wa kweli huthibitisha ukweli wa imani yake kwa kusimamisha Sala
na kutoa Zaka. Wakati ambapo Sala hudumisha na kuimarisha utajo wa Allah ndani ya
moyo wa muislamu , utoaji wa mali ya zaka huzidisha mahusiano ya muumini na waja
wa Mwenyezi Mungu. Baadhi ya mafunzo tunayoyapata kutokana na aya hizi ni kuwa
ishara za mtu mwenye imani ya kweli huthibiti kwa khofu ya ndani ya moyo na pia
matendo yake ya dhahiri. Aidha aya zinatufunza kuwa imani ni kitu chenye kiwango na
daraja mbali mbali, kinachoweza kupanda na kushuka. Kukisoma kitabu kitukufu cha
quran, huongeza na kuzidisha imani ya muislamu. Halikadhalika inatubainikia kutokana
na aya hizi kuwa kutoa mtu sehemu ya mali yake ni mojawapo ya masharti ya kuwa
muumini wa kweli, na kwa hakika mtu aliye bakhili hujiweka mbali na rehma za
Mwenyezi Mungu.
Aya ya nne ya sura yetu ya Anfal ndiyo inayotuhitimishia darsa yetu hii. Aya hiyo
inasema:


Hao ndio wanaoamini kweli kweli. Wao wana vyeo (vikubwa) kwa Mola wao, na
msamaha na riziki bora kabisa.

Aya hii inaashiria jaza na malipo mema ya waumini wa kweli na kueleza kuwa imani si
kujisifu na kujikweza kwa maneno matupu, bali ni hakika inayopasa kuthibiti na kukita


ndani ya nafsi ya mtu mpaka iweze kumfanya astahiki kuitwa muumini wa kweli. Hivyo
kama mtu ataweza kuifikia hali hiyo ya imani huwa na daraja ya juu ya utukufu mbele ya
Allah sw. Mtu wa aina hiyo hurehemewa kwa kupata maghufira na msamaha wa Mola
Karima pamoja na kuruzukiwa riziki na neema zilizo bora. Ni wazi kuwa malipo mema
ya Allah kwa waja wake hayahusiani na siku ya malipo tu huko akhera bali hata hapa
duniani huwaruzuku waja wake walio waumini wa kweli anuai za malipo mema na ya
kheri tabaan kwa kuzingatia hali ya kidunia. Miongoni mwa mafunzo tunayoyapata
kutokana na aya hii ni kuwa imani za watu ni hali yenye daraja na kiwango kinachoweza
kupanda na kushuka. Na hivyo daraja ya mja kwa Mola wake pia inaweza kuongezeka na
kupungua. Funzo jengine tunalolipata hapa ni kuwa hata wale walio waumini wa kweli
nao pia wanaweza kuteleza, hivyo wanahitajia maghufira na msamaha wa Mola
aliyetukuka. Darsa hii ya quran inaishia hapa. Tunamwomba Mola atujaalie kuwa
miongoni mwa waumini wa kweli walio na sifa zilizozungumziwa ndani ya aya
tulizosoma katika darsa yetu hii. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh../

 

 

Zaidi katika kategoria hii: « Suratul Anfal: Aya ya 5-9

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …