Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 11 Septemba 2016 12:24

Wimbi la utakfiri katika ulimwengu wa Kiislamu sehemu ya 39 na Sauti

Wimbi la utakfiri katika ulimwengu wa Kiislamu sehemu ya 39 na Sauti

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni tena katika sehemu ya 39 na ya mwisho ya vipindi hivi vinavyoangazia macho chimbuko la makundi yenye kuwakufurisha Waislamu wengine na kutekeleza jinai na mauaji ya kutisha dhidi yao.

Katika kipindi kilichopita tuliashiria idadi ya makundi ya kitakfiri na kigaidi yanayoendesha harakati zao nchini Syria, tukasema kuwa mbali na magenge ya Daesh na Jab'hatu Nusra, kuna makumi ya makundi mengine ya kigaidi na kitakfiri ndani ya nchi hiyo. Kwa hakika hivi sasa Syria imegeuka na kuwa maficho na ngome ya maelfu ya wanachama wa kitakfiri kutoka mataifa mbalimbali ya dunia. Hii ni kusema kuwa, wanamgambo kutoka Ulaya, Afrika, Marekani, Australia na mataifa ya Asia ya Kati na Caucasus wako nchini Syria wakiendeleza jinai na uharibifu wa kila namna ndani ya taifa hilo. Hata hivyo isisahaulike kuwa, baadhi ya nchi zina raia wake wengi nchini Iraq na Syria ambapo raia hao wanatekeleza jinai kwa namna ya uwakilishi. Na hii inatokana na siasa za kupenda migogoro zinazofuatwa katika eneo, sanjari na kueneza mirengo ya kufurutu ada na ukatili. Katika fremu hiyo, ndipo kukatolewa takwimu tofauti ya kiwango cha makundi ya kigaidi, ambapo raia wa nchi 80 hadi 90 walitajwa kuwepo nchini Syria pekee. Kwa mujibu wa ripoti, nchi za Kiarabu ndio chimbuko kuu la wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh. Hii ni kwa kuwa asilimia 72 ya raia wanaounda kundi hilo, wanatoka mataifa ya Kiarabu. Aidha wanachama wengi wa kundi hilo wanatoka nchi za Saudia, Tunisia, Morocco na Misri. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, asilimia 25 nzima ya wanachama wa genge hilo linaloungwa mkono na Marekani na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel, inaundwa na raia wa Saudia pekee. Uepo wa raia wengi wa Saudia miongoni mwa makundi ya kigaidi, kunadhihirisha ni kwa kiasi kigani nchi hiyo inavyohusika moja kwa moja katika uchocheaji wa migogoro, vita na mauaji ya maelfu ya watu wasio na hatia. Kwa mujibu wa ripoti, magaidi wanaotoka nchini Saudia ni kati ya elfu 20 hadi 22. Tunaweza kusema kuwa, raia wa Saudia ndio wanaoongoza upinzani na ugaidi nchini Syria. Utawala wa Saudia ambao wenyewe ni dhihirisho la udikteta na uliokosa aina yoyote ya demokrasia hii leo unawahadaa walimwengu kwamba unapambana na udikteta na kutaka kuweka demokrasia nchini Syria. Ukweli ni kwamba, baada ya kuibuka wimbi la mwamko wa Kiislamu katika nchi za kidikteta za Kiarabu, Saudia ilihisi hatari ya kupoteza nafasi na kupungua ushawishi wake katika eneo. Ni kwa ajili hiyo Iraq na Syiria zikageuka na kuwa shabaha ya Saudia na waungaji wake mkono katika uwanja huo. Saudia ilichukua hatua hiyo kwa lengo la kupotosha mwamko huo wa Kiislamu baina ya walimwengu.

***************************************

Utawala wa kidikteta wa Aal-Saudi kwa kushirikiana na Uturuki na kadhalika madola ya Magharibi yakaifanya Syria kuwa uwanja kwa ajili ya kuendeleza malengo yao ya muda mrefu. Muhimu Zaidi ikiwa ni kuhitimisha muqawama dhidi ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel. Ni vyema kuashiria hapa kwamba, utawala wa Aal-Saudi kwa kipindi kirefu umekuwa na kinyongo na chuki ya hali ya juu dhidi ya Ushia, ambapo tangu kulipojiri mapinduzi ya Kiislamu ya Iran nchini hapa, ulifuata mkondo wa siasa za kueneza propaganda za kuuonyesha Ushia kuwa ni tishio katika eneo la Mashariki ya Kati. Ushindi mbalimbali wa Harakati ya Kiislamu ya Hizbullah nchini Lebanon katika vita vyake na utawala wa Kizayuni na kufeli kukubwa ambako hakujawahi kushuhudiwa katika historoia ya utawala huo ghasibu, ni jambo ambalo halikuufurahisha utawala wa Aal-Saudi ambao daima umekuwa rafiki mkubwa na Israel. Ni kufuatia hali hiyo sanjari na kuunga mkono makundi yenye mahusiano na madola ya Magharibi na pia kufanya upatanishi na utawala wa Kizayuni, nchi hizo za Saudia na waitifaki wake zikawa zimekusudia kutoa pigo kwa muqawama wa Kiislamu. Wakati huo huo nafasi na juhudi ya serikali ya Syria katika kuunga mkono harakati za muqawama dhidi ya utawala huo wa Kizayuni, zilikuwa hazifichiki. Kwa upande wake Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tangu mwanzoni mwa mapinduzi ya Kiislamu ya nchini hapa, ilikuwa ikipiga nara za kutekeleza siasa za kupambana na Israel katika eneo la Mashariki ya Kati. Kwa kuzingatia kuwa, muqawama una mafungamano ya moja kwa moja na serikali ya Iran ya Kiislamu, hivyo Saudia ikaichukia vikali pia harakati hiyo ya muqawama. Kwa msingi huo, machafuko nchini Syria ilikuwa ni fursa nzuri ya Aal-Saud kwa ajili ya kuhitimisha muqawama kama ilivyokuwa dhana yao hiyo. Katika fremu hiyo Saudia ilidhania kuwa, ingeweza kumuondoa madarakani Rais Bashar al-Assad wa Syria kwa kipindi kisichozidi miezi mitatu tu na hivyo kuweza kufikia malengo yake machafu katika eneo la Mashariki ya Kati. Ni kwa ajili hiyo ndipo ikapeleka idadi kubwa ya magaidi kutoka Saudia na baadhi ya nchi za Kiarabu kwenda Syria kwa lengo la kufanikisha mpango wa huo. Hata hivyo ni mapema mno ambapo ndoto yao ilifeli kutokana mpambamano ya jeshi la serikali ya Damascus. Hii ni kwa kuwa marafiki wa kweli wa Syria hawakuwa tayari kuona makundi ya kitakfiri na mabwana zao yanafikia malengo yao hayo. Licha ya makundi hayo ya kigaidi na kitakfiri yanayoungwa mkono na Saudia, Uturuki na baadhi ya nchi za Kiarabu na Magharibi, kushadidisha wimbi la hujuma zao nchini Syria, yalikabiliana na kizingiti imara cha muqawama na hivyo yakaamua kutumia njia ya kufanya uharibifu mkubwa na mauaji ya kutisha kwa lengo la kuwatia khofu wanamapambano wa muqawama sanjari na kudhoofisha na kulegeza azma thabiti ya muqawma.

 

Sauti na Video

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)