Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 11 Septemba 2016 12:20

Wimbi la utakfiri katika ulimwengu wa Kiislamu sehemu ya 38 na Sauti

Wimbi la utakfiri katika ulimwengu wa Kiislamu sehemu ya 38 na Sauti

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni tena katika mfululizo wa vipindi hivi vinavyoangazia macho chimbuko la makundi yenye kuwakufurisha Waislamu wengine na kutekeleza jinai na mauaji ya kutisha dhidi yao hii leo ikiwa ni sehemu ya 38 ya vipindi hivyo.

Katika kipindi kilichopita tulitaja idadi ya makundi ya kigaidi na kitakfiri yanayoendesha harakati za kigaidi nchini Syria huku tukiishia kulitaja kundi la Jab’hatul-Islamiyyah Suriyyah ambalo limehusika na mashambulizi mengi dhidi ya wafuasi wa dini ya wachache nchini humo hususan Wakristo. Leo tutaendelea kufafanua kundi hilo, karibuni. Ndugu wasikilizaji kaulimbiu ya genge hilo ni ‘Mapambano dhidi ya Mashia, Wakristo na taasisi za serikali ya Kisuni za eneo la Sham.’ Hata hivyo wanachama wa kundi hilo wanajitambua kuwa sehemu ya mtandao wa kigaidi wa al-Qaidah huku wakiwa na uadui mkubwa na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh. Kadhalika kundi la Jayshul-Hurr 'yaani jeshi huru' ndilo kundi la mwanzo la wabeba silaha likiongozwa na Riad al-Asaad lililojitenga na jeshi la serikali ya Syria hapo mwaka 2011 kupitia  uungaji mkono kamili wa Saudia, Qatar, Uturuki, Imarat na baadhi ya nchi. Kile kinachoitwa mrengo wa wafanyamapinduzi nchini Syria, unayajumuisha makundi ya wabeba silaha ambayo Jeyshul-Hurr linashikilia nafasi kubwa ndani yake. Kati ya makundi hayo ni pamoja na al-Faruq, al-Faruqu Islami, Liwaaut-Tawhid, Liwaul-Fathi, Liwaul-Islami, Swaqurush-Shami na Majlisuth-Thuwwari Deir ez-Zor. Awali habari mbalimbali zilienea baada ya kujeruhiwa Riad al-Asaad huku nyingine zikielezea kuuawa kwake. Kufuatia hali hiyo, hatimaye kundi la Jeyshul-Hurr likamchagua Abdullah al-Bashir kuwa kinara wa genge hilo mwanzoni mwa mwaka 2014. Vyombo vya habari vya Saudia, Imarat, Qatar na waitifaki wao, wakaliita kundi hilo la kigaidi la Jayshul-Hurr kwa lakabu ya wanamapinduzi nchini Syria. Ngome za kundi hilo, zilikuwa katika miji ya Idlib, viunga vya Damascus, Hama na Deir ez-Zor. Kwa kadri siku zilivyokuwa zikisonga mbele, kundi hilo lilikuwa likizidi kupanua wigo wake nchini Syria. Hata hivyo kuingia makundi ya kigaidi na yenye misimamo ya kufurutu ada kama vile Daesh na mfano wa hilo huko nchini humo na kadhalika mapigano ya kila mara baina ya wapiganaji wa magenge hayo, kulipunguza nafasi ya wanamgambo wa Jayshul-Hurr katika ulingo wa kisiasa. Itakumbukwa kuwa, tangu awali wanamgambo wa kundi la hilo la Jeshi Huru, walifanya jinai mbalimbali dhidi ya raia na askari wa serikali ya Syria. Aidha magaidi hao walitoa adhabu kali sanjari na kuwalazimisha wakazi wa maeneo waliyokuwa wakiyadhibiti kuishi kwa misingi ya ukabila, ubaguzi utekaji nyara watu na uporaji mali. Mabadiliko yanayojiri nchini humo yameyafanya mara zote makundi ya kigaidi kutengana na kutofautiana au kuungana baina yao ili kwa njia hiyo makundi hayo yaweze kuendeleza uepo wao zaidi. Miongoni mwa makundi hayo ambalo sasa linaelekea kutimiza kipindi cha mwaka mmoja tangu kuasisiwa kwake, ni genge la Jayshul-Fathi tawi la mtandao wa kigaidi wa Al-Qaidah nchini Syria. Kwa mujibu wa duru za habari, kundi hilo linaundwa na wanachama wa kigaidi wanaokadiriwa kufikia elfu nne. Genge hilo liliundwa na muungano wa makundi saba hapo tarehe 24 Machi mwaka jana 2015, na kuzaliwa kundi hilo la Jayshul-Fathi.

***************************************************

Kundi la kigaidi na kitakfiri la Jab'hatu Nusra ni kati ya makundi muhimu ya kigaidi yanayounda genge la Jayshul-Fathi. Mbali na Jab'hatu Nusra kuna makundi ya Ahrarush-Sham, Jundul-Aqsa, Jayshus-Sunnah, Faylaq-Sham, Liwaul-Haqq na Ajnadush-Sham. Hivi sasa magaidi wa Jayshul-Fathi wanajaribu kujionyesha kuwa wenye misimamo ya wastani, ingawa hahata hivyo hawawezi kukanusha uhalisia wa itikadi na fikra zao za kigaidi kutoka genge la al-Qaidah. Mwaka 2013 Abu Mohammad al-Julani, kinara wa kundi la Jab'hatu Nusra nchini Syria alitangaza utiifu wake kwa Ayman al-Zawahiri, kiongozi wa genge la al-Qaidah. Uundwaji wa kundi la kigaidi la Jayshul-Fathi, ulifanyika kwa uungaji mkono mkubwa wa kigeni wa Saudia, Qatar na Uturuki.

Jayshul-Mujahidina wal-Wanswar ni kundi lingine la kigaidi na kitakfiri nchini Syria. Kundi hilo liliundwa na wanachama kutoka mataifa tofauti hapo mwezi Machi mwaka 2013. Wengi wa wanachama wake wanatoka kaskazini mwa Caucasus. Kundi la Jayshul-Mujahidina wal-Answar linaendesha harakati zake kwa uwazi mjini Aleppo na baadhi ya maeneo ya mji wa Hama na Lattakia. Kiongozi wa genge hilo hatari la kitakfiri ni raia wa Chechnya maarufu kwa jina la Abu Omar al-Shishani, ambaye ndiye muhusika mkuu wa upangaji mashambulizi ya kigaidi na ya kujitoa muhanga nchini Syria. Hata hivyo tarehe 13 Novemba mwaka 2014, kiongozi wa wapiganaji wa kitakfiri kutoka Chechnya, Ramadhan Qadir-of alitangaza habari ya kuuawa Abu Omar al-Shishani, kupitia moja ya shambulizi la la jeshi la Syria. Harakat Ahrarush-Sham ni kundi lingine la kitakfiri na kigaidi nchini Syria. Genge hilo ni muungano wa makundi manne ya kigaidi ambayo ni Jama'atu al-Twaliatul-Islamiyyah, Harakatul-Fajril-Islamiyyah, Kataibul-Iman na Kataibu Ahrarush-Sham. Kundi hilo linaendesha harakati zake katika mipaka ya miji ya Idlib na Hama. Kundi la Harakat Ahrarush-Sham linashirikiana sana kifikra na kistratijia na kundi la Jab'hatu Nusra. Mbali na genge hilo kuna kundi lingine kwa jina la Jab'hatul-Islami Litahrir Suriyyah ambalo ni kati ya makundi ya kigaidi yanayoendesha harakati zake nchini humo. Genge hilo liliundwa mwezi Septemba mwaka 2012 kwa kuyaunganisha pamoja makundi ya kigaidi yapatayo 20. Genge hilo linayajumuisha pamoja makundi ya upinzani na yenye mitazamo na harakati ya  Ikhwanul Muslimin na kundi la kigaidi la 'at-Tawhid' lenye makao yake mjini Aleppo. Kadhalika yapo makundi la ugaidi na yenye kujitegemea kama vile kundi la al-Faruq linaloendesha harakati zake katika mji wa Homs na maeneo ya karibu yanayopakana na Uturuki. Kwa mujibu wa Aron Lund, mtaalamu wa makundi ya kigaidi na kitakfiri nchini Syria, genge la Jab'hatul-Islami Litahrir Suriyyah ndilo kundi kubwa la utakfiri ndani ya taifa hilo la Kiarabu.

*****************************************************

Kundi la Jab'hatul-Islami al-Suriyyah, pia ni miongoni mwa makundi ya kigaidi na kitakfiri nchini Syria. Kundi hilo liliundwa mwezi Disemba mwaka 2012. Hatakama linaonekana kuwa kundi dogo la utakfiri nchini Syria, lakini ni kundi lenye nguvu ambalo limeenea katika maeneo tofauti ya nchi hiyo huku uongozi wake ukisimamiwa pia na kundi lingine la Ahrarul-Islami ash-Shami. Jab'hatul-Islami al-Suriyyah linahusika pakubwa katika kuratibu mashambulizi dhidi ya uwanja wa ndege wa kijeshi wa Taftanaz wa mjini Idlib, kaskazini mwa nchi hiyo. Licha ya kundi hilo kutangaza malengo yake kuwa ni kwa ajili ya raia pekee wa Syria, lakini asilimia kubwa ya wanachama wake ni raia wa kigeni kutoka nchi za Kirabu na Magharibi. Kadhalika vinara wa genge hilo ni sharti wawe raia wa Syria, huku likipiga marufuku kwa mwenye uraia wa kigeni kuweza kuliongoza. Kundi la Ahrarul-Islami ni ambalo liliundwa mwishoni mwa mwaka 2011 katika mkoa wa Idlib na katika mpaka wa Iraq na Syria chini ya uongozi wa Hassan Abboud na kwa idadi ya wapiganaji elfu 15 hadi 20. Awali wanachama wake walianza kuvamia maghala ya silaha ya jeshi la Syria na kujizatiti, ambapo kutokana na kuwa na mawasiliano ya karibu na makundi ya kigaidi ya nchini Iraq, lilianza kuyauzia silaha makundi hayo ya kigaidi nchini humo Iraq. Kundi hilo tunaweza kulitaja kama muhusika wa mashambulizi ya kujiripua na utegaji mabomu ndani ya magari katika miji tofauti ya Syria, hususan, Damascus, Aleppo na Homs ambapo linatumia uzoefu wa makundi ya kigaidi ya Iraq, katika kutekeleza hujuma hizo. Kwa sasa wanachama wa genge hilo wapo katika maeneo ya mkoa wa Al-Raqqah na viunga vya mashariki vya mji wa Aleppo wakishirikiana na wanachama wa Daesh. Kutokana na Ahrarul-Islami ash-Shami kuwepo katika maeneo ya mpakani na Uturuki, ndipo likahusika katika kuwapokea na kuwapa mafunzo magaidi wapya wanaoingia nchini Syria kwa lengo la kujiunga na magenge ya kigaidi. Kama tulivyosema, nchini Syria kuna idadi kubwa sana ya makundi ya kigaidi na kitakfiri yanayotenda jinai kila uchao dhidi ya raia. Kwa hakika mgogoro wa kubuniwa na madola ya Magharibi kwa kushirikiana na Saudia, Qatar na Uturuki huko Syria, umelifanya taifa hilo kuwa ngome ya makundi ya kigaidi duniani.

Wapenzi wasikilizaji kipindi cha makala ya utakfiri sehemu ya 37 kinaishia hapa kwa leo. Msikose kusikiliza sehemu ya 39 ya makala haya wiki ijayo. Mimi ni Sudi Jafar Shaban, kwaherini.

 

Sauti na Video

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)