Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 11 Septemba 2016 12:15

Chanzo cha utakfiri katika ulimwengu wa Kiislamu sehemu ya (37) na sauti

Chanzo cha utakfiri katika ulimwengu wa Kiislamu sehemu ya (37) na sauti

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni tena katika mfululizo wa vipindi hivi vinavyoangazia macho chimbuko la makundi yenye kuwakufurisha Waislamu wengine na kutekeleza jinai na mauaji ya kutisha dhidi yao hii leo ikiwa ni sehemu ya 37 ya vipindi hivyo.

Katika kipindi kilichopita tulizungumzia nafasi ya moja kwa moja ya Saudi Arabia katika kuasisi makundi ya kigaidi na kitakfiri ya al-Qaidah na Taleban yanayofanya jinai nchini Pakistan, Afghanistan, Iraq, Syria na kwingineko duniani. Ama katika kipindi hiki tutazungumzia kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh na namna kundi hilo lilivyoundwa kupitia mafundisho na itikadi za Uwahabi wa Saudia. Ndugu wasikilizaji, kundi la kitakfiri la Daesh kama yalivyo makundi mengine ya kigaidi ya al-Qaidah na Taleban, liliundwa nchini Iraq kwa ajili ya kudhamini malengo na siasa za Marekani na waitifaki wake wa Ulaya na Saudia ndani ya taifa hilo. Inafaa kuashiria kuwa, kabla ya kuvamiwa na Marekani hapo mwaka 2003, Iraq ilikuwa ikikabiliwa na matatizo chungu nzima ya kiutamaduni, kikaumu, kiuchumi na kisiasa. Utawala wa kiditeta wa Baathi chini ya Saddam Hussein, ulikuwa ukitumia mwanya huo ili kujitanua zaidi nchini humo. Hivyo uvamizi wa Marekani nchini Iraq, ulipigilia msumari wa matatizo hayo ndani ya taifa hilo la Kiarabu, kiasi cha kuyafanya kuwa mgogoro mkubwa. Mbali na hayo ni kwamba asilimia kubwa ya raia wa Iraq, ni Waislamu wa Kishia, huku Waislamu wa Kisuni na Wakurdi wakishika nafasi ya pili ya jamii ya Wairaq wote. Hata hivyo isisahaulike kuwa, mbali na Mashia, Masuni na Wakurdi, zipo jamii nyingine za watu wachache kama vile Waturkmen na Mayazidi. Tangu nchi hiyo ilipopata uhuru, jamii ya Waislamu wa Kishia iliendelea kutengwa mbali na ulingo wa kisiasa, huku utawala ukishikiliwa na wafuasi wa dhehebu la Kisuni pekee. Mbali na hayo, katika utawala wa Baathi wa dikteta Saddam Hussein, maulama wengi wa Kishia waliuliwa shahidi au kuwekwa jela na utawala huo. Katika hali hiyo, malengo ya Marekani katika kuivamia nchi hiyo hapo mwaka 2003, yalishindwa kufikia lengo lake. Aidha uchaguzi uliofanyika na kadhalika serikali iliyoundwa baada ya hapo, iliutia wasi wasi mkubwa utawala wa kifalme wa Aal-Saudi, nchini Saudia. Kuundwa serikali ya kidemokrasia na yenye uhusiano mzuri na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kulikuwa na maana ya kupungua ushawishi wa Aal Saud nchini Iraq. Ni baada ya hapo ndipo Saudia ikatumia uwezo wake wote kwa ajili ya kuvuruga usalama na amani nchini humo. Ni katika fremu hiyo ndipo kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh lenye misimamo ya Kiwahabi likaundwa ndani ya taifa hilo la Kiarabu.
***********************************************
Kundi la ‘Dola la Kiislamu nchini Iraq na Sham’ kwa kifupi, Daesh au (ISIS), liliundwa mnamo mwaka 2003 sanjari na kujiri mashambulizi ya Marekani mwaka huo na kuhamia nchini humo likiwa na baadhi ya viongozi wa genge la al-Qaidah wakiongozwa na Abu Musab al-Zarqawi mwenye uraia wa Jordan. Baada ya al-Zarqawi kuwasili nchini Iraq, aliunda kundi lililoitwa ‘Jama'at al-Tawhid wal-Jihad’ sanjari na kutangaza utiifu wake kwa kinara wa kundi la al-Qaidah, yaani Osama bin Laden. Aidha gaidi huyo aliunda baraza la ushauri la mujahidina nchini Iraq na kuyataka makabila tofauti ya nchi hiyo kuliunga mkono baraza hilo, huku watu walioungana naye akiwataka kula kiapo alichokiita ‘Halaful-Mutwayyibin’ yaani ‘Kiapo cha watu wema.’ Hatimaye Abu Musab al-Zarqawi aliuawa mwaka 2006 mjini Diyala huku uongozi wa harakati hiyo ukichukuliwa na Abu Omar al-Baghdadi. Naye Abu Omar al-Baghdadi akauawa na askari wa Iraq hapo mwaka 2010 ambapo Abubakar al-Baghdadi alichaguliwa kurithi mikoba ya mtangulizi wake, yaani Abu Omar al-Baghdadi. Baada ya kuibuka mgogoro wa Syria uliobuniwa na tawala za nchi za Ulaya, Marekani na waitifaki wao katika eneo kama vile Uturuki, Saudia na Qatar hapo mwaka 2011 ndipo kundi la kigaidi na kitakfiri la Jab’hatu Nusra likaundwa chini ya uongozi wa Abu Muhammad al-Julani. Ni kwa kuzingatia kuwa, misimamo ya kundi la Jab’hatu Nusra na lile ya Daesh yote ni ya Kiwahabi na yenye kufanana, ndipo kinara wa Daesh (Abubakar al-Baghdadi) akatoa mkanda wa sauti na kulitaja kundi la Jab’hatu Nusra kuwa ni sehemu ya ‘Dola la Kiislamu nchini Iraq na Sham.’ Aidha mwaka 2013 kinara wa kundi hilo la ukufurishaji alitangaza rasmi jina la harakati yake kuwa ‘Dola la Kiislamu nchini Iraq na Sham’ Yaani Daesh, ili kwa ajili hiyo kundi hilo liweze kuanza kutekeleza jinai katika nchi mbili hizo jirani za Iraq na Syria. Kadhalika Abubakar al-Baghdadi aliendelea kusisitiza kuwa, wanachama wa kundi la Jab’hatu Nusra walitakiwa kuwa chini ya bendera ya Daesh, sisitizo ambalo hata hivyo lilikataliwa na vinara wa al-Nusra. Hii ni katika hali ambayo kabla ya kuibuliwa mgogoro wa Syria, Abu Muhammad al-Julani alikuwa nchini Iraq na chini ya uongozi wa al-Baghdadi. Ni kwa utaratibu huo ndipo sanjari na kuendelea vita dhidi ya serikali halali ya Rais Bashar al-Assad, kukaibuka pia mapigano makali baina ya wanachama wa Daesh na Jab’hatu Nusra, mapigano ambayo yalipelekea maelfu ya wanachama wa makundi hayo kuuawa. Kufuatia kushadidi tofauti baina ya magenge hayo ya Kiwahabi, aliibuka Ayman al-Zawahiri, kiongozi wa mtandao wa kigaidi wa al-Qaidah kwa minajili ya kuhitimisha mvutano huo na kutangaza kuunga mkono fikra za Abu Mohammad al-Julani za kutaka kujitenga makundi hayo mawili, kama ambavyo pia alipendekeza kundi la Daesh liendeleze shughuli zake nchini Iraq pekee, huku lile la al-Nusra akilitaka liendeleshe shughuli zake nchini Syria pekee bila kuwepo maingiliano yoyote baina yao. Tangazo la al-Zawahiri lilimkasirisha sana Abubakar al-Baghdadi, na hivyo akaamua kutoa radiamali yake kwa kumtaja kinara huyo wa al-Qaidah kuwa ni kafiri sanjari na kuhalalisha damu yake. Hata hivyo na licha ya makundi ya kigaidi na kitakfiri ya Daesh, Jab’hatu Nusra na makundi mengine kama hayo kuwa na tofauti kubwa baina yao, lakini yanaendelea kufanya jinai za kutisha nchini Syria hadi leo chini ya uungaji mkono wa nchi za Magharibi na za eneo hususan Uturuki, Qatar na Saudia.
****************************************************************
Ndugu wasikilizaji tulisema kuwa, makundi ya Daesh na Jab’hatu Nusra ni makundi ya kigaidi na ya kitakfiri ambayo yanapata himaya kamili kutoka kwa baadhi ya nchi za Kiarabu na Magharibi kwa ajili ya kuvuruga amani ya baadhi ya nchi maalumu zisizofuata siasa za madola hayo hususan katika eneo la Mashariki ya Kati. Mbali na makundi hayo mawili, kadhalika yapo makumi ya makundi mengine ya kigaidi kama hayo yanayofanya jinai na mauaji ya kutisha. Kwa hakika mgogoro ulioibuliwa na madola ya Magharibi kwa kusaidiana na baadhi ya nchi za eneo, za Saudia, Uturuki na Qatar huko nchini Syria, umeifanya nchi hiyo ya Kiarabu kugeuka na kuwa ngome ya makundi ya kitakfiri duaniani. Hii ni kusema kuwa, mbali na makundi ya Daesh na al-Nusra, kuna kundi la ‘Jaishul-Islami’ ambalo ni moja ya makundi makubwa ya kitakfiri yanayoungwa mkono moja kwa moja na Saudia huko nchini Syria. Kundi hilo lilikuwa likiongozwa na Zahran Alloush aliyetangaza kuundwa genge hilo mnamo mwaka 2013. Ni vyema kuashiria hapa kwamba, baba yake na Alloush ni mmoja wa mamufti wakubwa wa Kiwahabi nchini Saudia. Kundi la kigaidi la Jaishul-Islami linaundwa na karibu makundi madogomadogo yapatayo 50 yenye fikra na mitazamo ya Usalafi wa Kiwahabi wa nchini Saudia, huku likiendesha harakati zake mjini Damascus na viunga vyake. Aidha kundi la Jaishul-Islamu ni maarufu kwa jina la jeshi la Saudia nchini Syria. Jina hilo lilitokana na kwamba, tofauti kubwa zilizopo baina ya viongozi wa muungano wa wapinzani wa Syria, zilipelekea kuibuka tofauti na mgawanyiko wa makundi ya wabeba silaha ndani ya nchi hiyo ya Kiarabu, suala ambalo liliifanya Saudia kutuma misaada ya fedha na silaha kwa makundi ya kigaidi yanayoendesha harakati zao katika viunga vya mji wa Damascus. Ni katika fremu hiyo, ndipo makumi ya maelfu ya magaidi yakakusanywa na kuunda genge hilo la Jaishul-Islami. Hatimaye Zahran Alloush aliuawa mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka jana 2015 katika moja ya mashambulizi ya anga akiwa yeye na baadhi ya makamanda wa genge hilo la Jaishul-Islami. Kuuawa kwa kinara huyo wa kitakfiri, kulilisababishia kundi hilo pigo kubwa. Jab’hatul- Islamiyyah Suriyyah ni kundi lingine kubwa la kigaidi na kitakfiri lenye kutekeleza mauaji na jinai za kutisha nchini Syria. Kundi hilo liliundwa mwezi Disemba mwaka 2012 kwa kuyaunganisha pamoja makundi yapatayo 11 ya Kiwahabi. Muhusika mkuu katika kuundwa genge hilo alikuwa ni Hassan Aboud, maarufu kwa jina la ‘Abdullah al-Hamawi’ aliyekuwa kinara wa kundi la kigaidi la ‘Harakat Ahrar ash-Shami al-Islamiyya.’ Ni vyema kuashiria kuwa, katika miaka ya mwanzoni mwa kuvamiwa kijeshi na Marekani taifa la Iraq, Abdullah al-Hamawi alifanya safari nchini humo na kushirikiana bega kwa bega na makundi ya kigaidi enzi hizo, ambapo baada ya kurejea nchini Syria, serikali ya Damascus ilimtia mbaroni na kumuweka jela. Hata hivyo takfiri huyo alitoroka jela kupitia hujuma iliyofanywa na makundi ya kigaidi yenye kubeba silaha hapo mwaka 2011. Jab’hatul- Islamiyyah Suriyyah linayajumuisha makundi ya kigaidi ya ‘Katibatul-Haqqi’ la mjini Homs, ‘Answarush-Sham’ la Idlib, ‘Jaishut-Tawhid’ la mjini Deir ez-Zor na ‘Katibatul-Mujahidina ash-Shami’ la mjini Hama. Kundi hilo la Jab’hatul- Islamiyyah Suriyyah, linafuata idiolojia ya utakfiri ambapo pia limehusika na mashambulizi mengi dhidi ya wafuasi wa dini ya wachache nchini humo hususan Wakristo. Kaulimbiu ya genge hilo ni ‘Mapambano dhidi ya Mashia, Wakristo na taasisi za serikali ya Kisuni za eneo la Sham.’ Hata hivyo wanachama wa genge hilo wanajitambua kuwa sehemu ya mtandao wa kigaidi wa al-Qaidah huku wakiwa na uadui mkubwa na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh. 
Wapenzi wasikilizaji kipindi cha makala ya utakfiri sehemu ya 37 kinaishia hapa kwa leo. Msikose kusikiliza sehemu ya 38 ya makala haya wiki ijayo. Mimi ni Sudi Jafar Shaban, kwaherini.

 

Sauti na Video

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)