Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatano, 20 Aprili 2016 10:33

Malengo na mbinu za Wamagharibi katika kueneza chuki dhidi ya Iran na Uislamu

Malengo na mbinu za Wamagharibi katika kueneza chuki dhidi ya Iran na Uislamu

Baada ya kusambaratika mfumo wa ncha mbili wa kambi za Magharibi na Mashariki, jumuiya ya kimataifa ingali katika kipindi cha mpito. Katika kipindi hiki cha mpito, nchi za Magharibi zinazodai kuwa na utamaduni bora zinadai kuwa kufuatia kusambaratika mfumo wa Kikomunisti, hakuna tena chaguo jngine isipokuwa Demokrasia ya Kiliberali katika dunia.

Makala itaangazia malengo na mbinu za Wamagharibi katika kueneza chuki dhidi ya Iran na Uislamu. Kwa msingi wa fikra hizo potofu za kisiasa, baadhi ya wananadharia wanaofuata mtazamo huo waliibua fikra kuwa baada ya Ukomunisti, hivi sasa ni Uislamu unaotoa changamoto kwa Demokrasia ya Uliberali.

Hapa tunaweza kutaja nadharia ya Samuel Huntington ambaye aliwasilisha nadharia ya 'Makabiliano ya Staarabu.' Fikra hii ilikuwa mwanzo wa mkondo wa chuki dhidi ya Uislamu na chuki dhidi ya Iran nchi ambayo ni chimbuko la Mapinduzi ya Kiislamu. Fikra ya Chuki Dhidi ya Uislamu ilishika kasi kufuatia mashambulizi ya kigaidi yenye kutiliwa shaka huko Marekani Septemba mwaka 2001.

Baada ya mashambulizi hayo, adui wa Wamagharibi sasa hakuwa tena kambi ya Mashariki iliyosambaratika bali Uislamu na Waislamu walitambuliwa kama maadui.

Pamoja na hayo tunaweza kusema kuwa chuki dhidi ya Uislamu ni fikra ambayo ilikuwepo katika karne za nyuma hasa wakati wa makabiliano baina ya Waislamu na Wakristo maarufu kama Vita vya Msalaba. Katika zama zetu tulianza kushuhudia kiwango kikubwa cha chuki dhidi ya Uislamu katika muongo wa 1980. Fikra hiyo ilishika kasi baada ya hujuma za Septemba 11 2001 nchini Marekani.

Taasisi ya Runnymede Trust ya Uingereza katika kubainisha maana ya istilahi ya Islamophobia au chuki dhidi ya Uislamu ilisema itikadi hiyo ina maana ya kuwa na hofu, wahka na woga kuhusu Uislamu na Waislamu na kwa msingi huo kuwabagua Waislamu kisiasa, kiuchumi na kijamii. Wenye itikadi hiyo huwatazama Waislamu kama tishio kwa ustaarabu wa Magharibi na pia huutazama Uislamu kama dini yenye kupenda vita na yenye kubakisha watu nyuma. Aidha huutazama Uislamu zaidi kama idiolojia ya kisiasa na wala si kama dini tukufu na kwamba Uislamu si ustaarabu. Kwa msingi wa fikra hiyo potovu, Wamagharibi huwatazama Waislamu kama tishio kwa thamani zao za kitaifa na kiutamaduni.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika barua yake ya pili kwa vijana wa Magharibi aliashiria maudhui hii ya Wamagharibi kujaribu kuuonyesha Uislamu kama adui na kusema: "Katika muda wa miongo miwili sasa, yaani takribani muda wa baada ya kusambaratika Shirikisho la Sovieti, kumekuwepo na mikakati ya kuuonyesha Uislamu kama adui wa kutisha."

Mbali na kuwepo chuki dhidi ya Uislamu pia kuna chuki dhidi ya nchi muhimu ya Kiislamu yaani Iran. Chuki dhidi ya Iran au Iranophobia, ni fikra ambayo iliibuka sehemu moja na ile ya chuki dhidi ya Uislamu katika nchi za Magharibi. Fikra hii ilijitokeza katika nchi za Magharibi baada ya Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979 na kufuatia kuongezeka nguvu na uwezo wa Iran katika eneo katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni hasa baada ya uvamizi wa nchi za Magharibi Afghanistan mwaka 2001 na Iraq mwaka 2003 na matukio ya mwamko katika Ulimwengu wa Kiislamu kuanzia Desemba mwaka 2010.

Fikra ya chuki dhidi ya Iran inaandamana na fikra nyingine potovu ya chuki dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia yaani Shiaphobia. Fikra hii ya chuki dhidi ya Mashia imekuwa ikienezwa na nchi za Magharibi na pia baadhi ya nchi za Kiarabu zinazopinga maendeleo ya kimapinduzi katika eneo. Kwa miaka kadhaa sasa baadhi ya waandishi na watawala wa tawala hizo za Kiarabu wamekuwa wakitumia istilahi ya 'Hilali ya Kishia'. Lengo la istilahi hiyo likiwa ni kuonyesha kuwa hatari harakati za Mashia katika uga wa kisiasa na kijamii katika ulimwengu wa Kiislamu.

Kuna historia ndefu ya makabiliano ya Uislamu na Magharibi. Lakini kustawi kwa kasi Uislamu duniani sambamba na kujiri Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran ni nukta mbili ambazo zilihuisha upya tahamani za Kiislamu na kupelekea Utambulisho wa Kiislamu kupata nguvu mpya duniani. Kwa msingi huo dunia ikashuhudia mwamko mkubwa wa Kiislamu hasa katika nchi za Kiislamu. Kutokana na hali hiyo nchi za Magharibi zilihisi kuwa maslahi yao yatakuwa hatarini kutokana na kuwa Waislamu wameamka. Kwa msingi huo nchi za Magharibi zilianza kutumia nguvu za kijeshi, kipropaganda, kiutamaduni na kiuchumi kukabiliana na Uislamu ambapo Iran imekuwa mlengwa mkuu wa njama hizo. Iran inalengwa kwa sababu ni nchi ya Kiislamu, na pia kwa ajili ya kuwa wananchi wake wengi ni wafuasi wa madhehebu ya Shia. Kwa hivyo nchi hii inakumbwa na aina tatu ya chuki za Wamagharibi yaani chuki dhidi ya Uislamu, chuki dhidi ya Iran na chuki dhidi ya Ushia. Lengo la aina hizo tatu za chuki ni kuifanya nchi hii itengwe na kuwafanya walimwengu wawe na hofu nayo.

Ukweli ni kuwa mfumo wa kibeberu wa nchi za Magharibi unatumia vyombo vya habari kukabiliana kwa njia mbali mbali na Uislamu pamoja na Waislamu.

Nchi za Magharibi zinataka zidhibiti na kuwa na satwa katika eneo la Magharibi mwa Asia lenye umuhimu mkubwa kwa mtazamo wa jiografia ya kisiasa, kistratijia na kiuchumi. Lengo la satwa hiyo ni pamoja na kudhamini maslahi ya nchi za Magharibi na pia kulinda usalama wa baadhi ya waitifaki wao katika eneo hasa utawala wa Kizayuni wa Israel. Katika kufikia lengo lao la chuki dhidi ya Uislamu, Wamagharibi sasa wanatumia ugaidi na vitendo vya kigaidi.

Marekani inachochea pia mazingira ya 'chuki dhidi ya Iran' katika eneo na inataka maudhui ya Iran iwe maudhui muhimu zaidi katika sera zake za kigeni sambamba na kuunda muungano mkubwa wa kieneo na kimataifa dhidi ya ustawi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nyanya za sayansi kama vile mpango wa nyuklia wenye malengo ya amani. Kwa kueneza habari potovu kuhusu Iran Marekani inataka Jamhuri ya Kiislamu itengwa kimataifa.

Katika sehemu nyingi tunashuhudia kuendeshwa kwa pamoja kampeni ya chuki dhidi ya Uislamu, chuki dhidi ya Iran na chuki dhidi ya Ushia. Aidha tunaona pia chuki dhidi ya Uislamu usio wa Kishia kama vile kutumia vitendo vilivyo dhidi ya ubinadamu na dhidi ya Uislamu vya magaidi wa Daesh au ISIS kueneza chuki dhidi ya Uislamu.

Tunaweza kusema kuwa Wamagharibi wanafuatilia malengo kadhaa katika kueneza chuki dhidi ya Uislamu, Iran na Ushia.

Moja ya sababu za kueneza chuki dhidi ya Uislamu ni kuzuia kuenea dini hii tukufu duniani hasa miongoni mwa watu wa ulimwengu wa Magharibi hususana vijana. Wakati vijana wengi wanapoukumbatia Uislamu, dini hii na ustaarabu wake unakuwa ni changamoto kubwa kwa ile fikra inayotawala Magharibi ya Demokrasia ya Kiliberali. Kwa kueneza chuki dhidi ya Iran na Ushia, Marekani na waitifaki wake wanapata mwanya wa kuleta majeshi yao vamizi katika eneo sambamba na kuvuruga mshikamano wa nchi za Kiislamu.

Baadhi ya malengo ya chuki dhidi ya Iran na Ushia ni kuzuia Iran ya Kiislamu kuwa kigezo kwa nchi zingine katika eneo na ulimwengu mzima wa Kiislamu. Kwa hivyo Wamgharibi wanafanya kila wawezalo kuona Iran haipati ushawishi katika eneo sambamba na kujaribu kubadilisha muundo na mwenendo wa Jamhuri ya Kiislamu na pia kuzuia nchi hii kuwa mhusika katika mchakato wa kudhamini usalama wa eneo. Wamagharibi wanatumia kila fursa ya hujuma ya ugaidi kueneza chuki dhidi ya Uislamu sambamba na kushadidisha chuki dhidi ya Iran na Ushia. Magaidi wa Daesh na makundi mengine ya Waislamu wenye misimamo mikali husaidia kueneza chuki dhidi ya Uislamu hata kuliko Wamagharibi na maadui wengine wa Uislamu.

Wananadharia wa kisiasa wa nchi za Magharibi wanaamini kuwa katika kila kipindi kunapaswa kuwepo nchi au staarabu yenye kuhesabiwa kama adui ili kufanikisha malengo ya Magharibi.

Aidha kama tulivosema, hofu ya kuwa vijana wa nchi za Magharibi wanavutiwa na Uislamu na hivyo kuongeza idadi ya Waislamu nchi za Magharibi ni sababu nyingine ya kueneza chuki dhidi ya Uislamu. Kwa hivyo ili kufikia malengo yao Wamagharibi wanatekeleza sera ya kuonyesha Uislamu kuwa dini hatari na iliyo duni ikilinganishwa na dini zingine. Aidha katika kufikia malengo yao Wamagharibi wanahujumu kijeshi nchi za Kiislamu sambamba na kueneza hitilafu na mifarakano baina ya mataifa ya Waislamu.

Wamagharibi wanataka kuwepo na hofu endelevu na isiyo na mantiki kuhusu Uislamu na Waislamu ili kuarifisha mitazamo ya kisiasa ya Uislamu na itikadi za Waislamu kuwa tishio kwa dunia. Pamoja na njama hizo za Wamagharibi lakini walimwengu nao wanazinduka hatua kwa hatua na wengi wanatambua hadaa zilizopo katika propaganda za nchi za Magharibi.

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)