Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumamosi, 16 Aprili 2016 07:09

Watoto na wanawake wa Yemen na Nyoyo zilizojaa machungu

Watoto na wanawake wa Yemen na Nyoyo zilizojaa machungu

Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika makala hii ya kila wiki ambayo kwa kawaida huwa inatupia jicho matukio mbalimbali muhimu yaliyojiri katika kipindi cha juma zima. Leo tumekuandalieni makala fupi chini ya kichwa cha maneno kisemacho: Watoto na Wanawake wa Yemen na Nyoyo Zilizojaa Machungu, tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa makala hii.
*******
Uvamizi wa kijeshi nchini Yemen ulianza tarehe 25 Machi 2015 kwa mashambulizi ya anga ya muungano wa nchi za eneo hili zikiongozwa na Saudi Arabia. Muungano huo uliupa jina la "Tufani Ngangari" uvamizi wake huo ingawa baada ya kupita kama mwezi mmoja hivi ulibadilisha jina hilo na kuuita opereseheni ya kuhuisha matumaini. Ukiitoa Oman, nchi nyingine za Kiarabu wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi yaani Imarati, Qatar, Kuwait na Bahrain zinashiriki katika uvamizi huo zikiongozwa na Saudia. Wahanga wakuu wa uvamizi huo unaozishirika pia nchi za Jordan, Misri, Morocco na Sudan, ni wananchi madhulumu wa Yemen.
Tangu mwanzoni mwa uvamizi huo, vyombo vya habari vya Yemen vilikuwa vinaripoti kwa kusisitiza juu ya namna utawala wa Kizayuni unavyoiunga mkono Saudia katika mashambulio hayo. Baada ya hapo baadhi ya vyombo vya habari vya Magharibi vilitangaza ripoti zilizothibitisha uungaji mkono wa kisilaha na hata kushiriki wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika uvamizi huo wa nchini Yemen.
Nchi za Marekani, Uingereza, Ufaransa na Uturuki ni miongoni mwa nchi ambazo zinawaunga mkono viongozi wa Saudia wanaouwa watoto wadogo huko Yemen kiasi kwamba Ikulu ya Marekani White House imefikia kutangaza kuwa, Rais Barack Obama wa nchi hiyo ameruhusu askari wa Marekani kuzisaidia kilojistiki pamoja na taarifa za kijasusi operesheni za kijeshi za Saudia nchini Yemen.
Hivi sasa zaidi ya mwaka mmoja umepita tangu ulipoanza uvamizi huo unaoongozwa na Saudia huko Yemen, lakini wavamizi hao licha ya kutumia uwezo wao wote wa kijeshi, wameshindwa kufikia malengo waliyodai - ya kuanzisha uvamizi huo. Miongoni mwa malengo yao hayo ni kuiangamiza harakati ya wananchi ya Ansarullah na kumrejesha madarakani Abdu Rabuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa Yemen aliyejiuzulu na kuitoroka nchi. Matokeo pekee ya uvamizi wa nchi hizo katika nchi hiyo ya Kiarabu na Kiislamu ni kuongezeka nguvu za kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh, kushadidi ukata na umaskini pamoja na ukosefu mkubwa wa amani na usalama, sambamba na uvunjaji wa haki za kimsingi na za chini kabisa za wananchi wa Yemen.
Kufanya mauaji dhidi ya raia wakiwemo wanawake na watoto wadogo, kushambulia mahospitali na vituo vya matibabu bali hata vituo vya Umoja wa Mataifa vya madaktari wasio na mipaka, kutumia baadhi ya silaha zilizopigwa marufuku kama vile mabomu ya vishada, kuyatumbukiza katika hatari maisha ya mamilioni ya wananchi wa Yemen kupitia kuwazingira kila upande na kutoruhusu kuwafikia shehena za misaada ya kibinadamu, kushambulia na kuangamiza miundo mbinu na asasi zote za kiuchumi za nchi hiyo, ni miongoni mwa uvunjaji mkubwa na wa wazi wa sheria za kimataifa za haki za binadamu unaofanywa na wavamizi wa Yemen wakiongozwa na Saudi Arabia.
*******
Takwimu zinaonesha kuwa, tangu mwaka jana hadi hivi sasa, zaidi ya watu 9,400 wa Yemen wameshauawa shahidi katika mashambulizi ya kivamizi yanayoongozwa na Saudia huko Yemen. Kati ya watu hao, wanawake ni 1519 na watoto wadogo ni 1996. Zaidi ya raia 16 elfu wa Yemen wameripotiwa kujeruhiwa katika mashambulizi hayo ya kinyama huku idadi ya wanawake na watoto wadogo waliojeruhiwa kwenye jinai hizo ikipindukia elfu tatu.
Amma shirika la kimataifa la haki za binadamu la Amnesty International limesema katika takwimu zake za hivi karibuni ilizozitoa tarehe 26 Februari kwamba raia 35 elfu wa Yemen wameshauawa kwa umati hadi hivi sasa. Shirika hilo limeongeza kuwa, lina ushahidi madhubuti unaothibitisha kwamba Saudia imeshambulia maeneo ya raia na miundo mbinu ya Yemen na katika kipindi cha chini ya mwaka mmoja, imeua kwa umati watu 35 elfu wa Yemen na kusababisha zaidi ya raia milioni mbili na nusu wa nchi hiyo kuwa wakimbizi ndani na nje ya mipaka ya Yemen.
Katika umwagaji huo mkubwa wa damu, Saudia imeshambulia na kuharibu viwanja vya ndege 14, bandari 10, madaraja na barabara kuu 512, vituo 125 vya umeme, matangi 164 makubwa ya maji, vituo 167 vya mawasiliano, nyumba laki tatu na 28,137 za makazi ya raia, misikiti 615, taasisi 569 za masomo na shule, vyuo vikuu 39, vituo vya habari 16, vituo 328 vya afya, taasisi 970 za serikali, masoko na vituo 353 vya biashara, malori 584 ya kubeba mafuta na vyakula, vituo 328 vya huduma za mafuta, maghala 546 ya chakula, maeneo 59 ya kihistoria, maeneo 119 ya utalii, karakana 190 na viwanja 42 vya michezo vya Yemen pamoja na kupelekea kufungwa shule 3750 za Yemen.
Kwa mujibu wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu milioni mbili na laki sita na 90 elfu wamekuwa wakimbizi ndani ya mipaka ya Yemen kutokana na mashambulizi hayo yanayoongozwa na Saudia. Hadi sasa wananchi laki moja na 70 elfu wamekimbilia katika nchi za Djibouti, Ethiopia, Somalia na Sudan. Wakati huo huo Umoja wa Mataifa umetabiri kuwa, hadi mwishoni mwa mwaka huu, watu laki moja na 67 elfu wataongezeka katika idadi ya wakimbizi hao, iwapo vita hivyo vitaendelea.
Kituo cha habari cha Kiarabu cha Akhbarus Sa'a kimeripoti kuwa, kila wiki kati ya raia 500 hadi 800 wa Yemen wanakimbilia Djibouti kutokana na mashambulizi ya ndege za kivita za Saudia. Huko Djibouti nako wanalazimika kuishi katika mazingira magumu sana ya ukosefu wa chakula, maji na madawa, tena katika mazingira ya joto kali lisilovumilika.
*******
Mgogoro angamizi wa kibinadamu nchini Yemen umewafanya zaidi ya asilimia 80 ya wananchi wa Yemen kukumbwa na ukosefu mkubwa wa chakula, na watoto milioni moja na laki nane kushindwa kwenda shuleni. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, khumusi nne (nne ya tano) ya wakazi wa Yemen, sawa na watu milioni 21.2 wa nchi hiyo wanahitajia misaada ya dharura ya kibinadamu. Kwa uchache watoto laki tatu na 20 elfu walio chini ya miaka mitano wanasumbuliwa na lishe duni huko Yemen kutokana na mashambulizi hayo ya Saudia na wenzake mashambulizi ambayo lengo lake linaonekana wazi kuwa ni kuangamiza kizazi cha Waislamu wa Yemen.
Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF hivi karibuni umetoa ripoti na kusema kuwa, kila siku watoto wasiopungua sita wanauawa na kujeruhiwa nchini Yemen. Katika ripoti yake hiyo iliyoipa jina la Watoto Walioko Hatarini, UNICEF imesema, tangu ulipoanza uvamizi wa Saudi Arabia nchini Yemen hadi hivi sasa, watoto 935 wa Yemen wameshauawa na 1356 wengine wamejeruhiwa katika mashambulizi ya moja kwa moja. Aidha karibu watoto elfu kumi wenye umri wa chini ya miaka mitano wamepoteza maisha yao kutokana na lishe duni na kukosa suhula nzuri za matibabu.
Ukiweka pembeni ukatili huo, taasisi za haki za binadamu za kimataifa zimeripoti kufanyika unyanyasaji mkubwa wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana wadogo wa Yemen. Saba Zawbah, mratibu wa kitaifa wa miradi ya haki za binadamu wa Shirika la Ustawi la Umoja wa Mataifa amesema kuwa, ndoa za wanaume vizee wa Saudia na wasichana wadogo wa Yemen zimeongezeka sana. Wengi wa wasichana hao wa Yemen wanaolewa na vikongwe hivyo vya Saudia licha ya kuwa na umri ulio chini ya rika la kuolewa. Kiujumla ni kuwa, madhara ya kimwili na kisaikolojia ya uvamizi huo angamizi wa Saudia nchini Yemen ni makubwa mno ambayo itapita miaka mingi bila ya kufutika.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)