Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 29 Machi 2016 13:04

Tatizo la ndoa za watoto

Tatizo la ndoa za watoto
Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni katika makala hii ambayo itaangazia ndoa za watoto au za utotoni duniani.

Tutazungmza kuhusu kundi la jamii ambalo hufikishwa katika hafla ya harusi si kwa kutaka bali kwa matakwa ya watu wengine. Huwa wanaingia katika ulimwengu wa ndoa mapema na pasina wao kuchagua na pia kwa kutojua hali ya mustakabali wao. Baadhi hufungishwa ndoa pasina wao kujua au hufungishwa ndoa kwa nguvu na mabavu na yote hayo huwa na matokeo mabaya.

Kuwaozesha watoto wadogo huwa na madahara kadhaa ya kimwili kama vile kutokuwa tayari kushika mimba katika umri mdogo na vile vile matatizo ya kisaikolojia kutokana na kulazimishwa kufunga ndoa n.k.

Kwa mujibu wa ripoti iliyochapishwa hivi karibuni na Tume Kuu ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, kila siku duniani mabanati 39 huozwa bila kuridhia wala pasina haki ya kuchagua mume. Iwapo hali kama hii itaendelea, inatabiriwa kuwa ifikapo mwaka 2020, kutakuwa na wasichana milioni 142 walioozeshwa kabla ya kufika umri wa miaka 18.

Elina ni binti kutoka nchi ya Malawi ambaye alilazimishwa kufunga ndoa akiwa na umri wa miaka 15. Anasema hivi kuhusu suala hilo: "Nilipata matatizo mengi baada ya kuolewa. Nilikuwa mtoto mdogo na sikujua ni vipi niwe mke. Kipindi kibaya zaidi kilikuwa wakati nilipopata ujauzito. Hii ni kwa sababu mbali na kumshughulikia mume nililazimika kufanya kazi zote za ndani ya nyumba na pia shambani."

Kuna sababu mbali mbali za ndoa za mapema na hilo hutegemea aina ya jamii. Ukimbizi, umasikini, mila na desturi, na kutafuta usalama mabanati ni kati ya sababu za ndoa za mapema. Kuna familia nyingi ambazo huwa zimetumbukia katika dimbwi la umasikini na hivyo ili kukidhi gharama za maisha huamua kuwaoza mabainti zao wakiwa wangali watoto. Katika baadhi ya jamii, wazazi huwa na dhana kuwa iwapo hawataafiki kuwaoza mabanati zao wakiwa watoto basi hawatapata fursa ya kuolewa katika siku za baadaye.

Katika baadhi ya jamii, hata kama kuna shule za watoto wa kike, lakini kiwango duni cha masomo na ukosefu wa waalimu hupelekea wazizi kuona masomo kuwa yanachukua gharama za bure na kuwapotezea watoto wakati. Katika upande mwingine baadhi ya familia hupinga watoto wao kuenda shuleni. Hii ni kwa sababu huwa wanawatumia mabanati zao kama wafanyakazi ndani ya nyumba za watu matajiri ili wakidhi pato lao kwa njia hiyo.

Katika baadhi ya jamii za nchi kama vile Sudan Kusini, mchumba hufahamisha familia ya binti kuhusu utajiri wake ambapo hujumuisha pesa, dhahabu na mifugo kama vile ng'ombe. Ayen, binti Msudani Kusini anasema hivi: "Mume wangu alimlipa baba yangu mahari ya ng'ombe 75 ili anioe. Hatukuwa tunajuana hata kidogo kabla ya kufungishwa ndoa wala hatukujadili suala hilo wala sikuwa nikijua lolote kuhusu ndoa. Wakati nilipomfahamisha baba yangu kuwa sitaki kuolewa , alisema lazima niolewe kwani anahitajia ng'ombe."

Uchunguzi wa shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch umebaini kuwa, katika nchi za Afghanistan, Bangladesh, Malawi, Nepal, Sudan Kusini, Tanzania, Yemen na Zimbabwe kuna kesi nyingi za ndoa za watoto ambapo watoto waathirika hupata matatizo ya muda mrefu. Uchunguzi huo umebaini kuwa ndoa hizo za mapema hupelekea watoto wengi kupokonywa haki zao kama wanadamu.

Ndoa za watoto ni tatizo sugu kote duniani. Kati ya madhara ya kuozwa mapema mabanati ni kuhatarisha afya, kupata mimba mapema, kuteswa na kupigwa katika ndoa n.k.

Uchunguzi kote duniani umebaini kuwa, kuna hatari kubwa ya kupoteza maisha watoto ambao huzaa wakiwa na umri wa kati ya miaka 10-14. Aidha madhara mengine ya kuozwa mabanati mapema ni kunyimwa haki ya kuendelea na masomo. Katika nchi kama vile Bangladesh, imebainika kuwa wasichana ambao wanapata fursa za kusoma huwa hawana hamu ya kuolewa wakiwa watoto.

Shirika la Kutetea Haki za Binadamu, Human Rights Watch limetangaza kuwa, pamoja na kuwa kumepatikana maendeleo katika hali ya wanawake duniani katika siku za hivi karibuni, lakini tatizo la wasichana wadogo kuolewa mapema lingalipo.

Bangladesh ni nchi ya bara Asia ambayo ni ya nne duniani kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya wasichana wanaoolewa wakiwa wangali watoto wadogo. Kabla ya Bangladesh, nchi zilizo na idadi kubwa zaidi ya watoto wa kike wanaoolewa wakiwa watoto duniani ni Niger, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Chad. Kwa mujibu wa takwimu za Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF, katika muda wa mwaka 2005-2013, asilimia 29 ya mabanati wa Bangladesh waliolewa kabla hawajafikia umri wa miaka 15 huku wengine asilimia 65 wakiozwa kabla ya kufikia umri wa miaka 18.

Kumetajwa sababu kadhaa za kuolewa watoto wa kike Wabangladeshi. Kati ya sababu hizo ni ubaguzi wa kijnsia, wasiwasi wa kijamii pamoja na mila na desturi za nchi hiyo ya kusini mwa Asia. Aidha sababu nyingine imetajwa kuwa mahari ya juu wanayotozwa wanaume wanaooa wasichana wadogo.

Hali kadhalika umasikini mkubwa katika familia nyingi huwalazimu wazazi wawaoze mabanati zao kama njia ya kuwaokoa kwani huwa hawawezi kujimudu kuwapa chakula na kuwaelimisha.

Bangladesh pia ni kati ya nchi ambazo hukumbwa na mabalaa mengi ya kimaumbile kutokana na mabadiliko ya tabia nchi. Ukweli huu hupelekea wananchi wa nchi hiyo kukabiliana na hali ngumu sana ya kimaisha hasa katika mitaa ya mabanda nchini humo.

Human Rights Watch inasema imezihoji familia za Wabangladeshi ambao wamewalazimu watoto wao wa kike waolewe. Aghalabu ya familia hizo zimetaja umasikini kuwa sababu kuu ya kuwaoza wasichana wakiwa na umri mdogo sana. Mmoja kati ya wazazi hao amenukulwa akisema hivi: "Mimi nilimuoza binti yangu akiwa yungali mtoto kwa sababu nilikuwa na njaa."

Mwezi Novemba mwaka 2014, Umoja wa Mataifa ulipitisha azimio kuzishurutisha nchi wanachama kupiga marufuku ndoa za watoto wadogo katika nchi zao.

Tatizo la ndoa za watoto wadogo ni gumu sana na limeenea kote duniani. Ni kwa sababu hiyo ndio nchi zote duniani zikaahidi kuangamiza tatizo hilo ifikapo mwaka 2030. Bila shaka ili kufikia lengo hilo, serikali zinapaswa kuchukua hatua imara kwa kuzingatia hali ya kila nchi.

Ingawa katika baadhi ya maeneo duniani kumeshuhdiwa kupungua idadi ya ndoa za watoto wadogo, lakini kuna baadhi ya nchi ambapo tatizo hilo limeongezeka.

Kwa hivyo kuchukuliwa hatua za pamoja na kwa msingi wa sheria za kitaifa na kimataifa, bila shaka kutasaidia kutafutiwa ufumbuzi wa kimsingi tatizo la ndoa za watoto wadogo duniani.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)