Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Ijumaa, 18 Machi 2016 09:44

Historia fupi ya Nairuzi

Historia fupi ya Nairuzi

Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Jumapili ya tarehe 20 Machi mwaka huu inasadifiana na kuanza mwaka mpya wa Kiirani wa Hijria Shamsia. Ni sherehe za kale na za muda mrefu ambao matawi yake yameenea katika kona mbalimbali za dunia hadi Afrika Mashariki. Asili ya sherehe za Mwakakongwa huko Makunduchi visiwani Zanzibar, ni sherehe hizo za Nairuzi za nchini Iran. Mbali na Iran sherehe za Nairuzi hufanyika pia katika Jamhuri ya Azerbaijan, Albania, Kirghizstan, Turkmenistan, Macedonia, India, Uturuki, Jamhuri ya Tatarstan nchini Russia, Sudan na Zanzibar huko Tanzania. Leo tumeamua katika makala yetu ya wiki tuzungumze kwa muhtasari kuhusu historia ya sherehe za mwaka huu mkongwe ambao hivi sasa unafuata Hijra ya Bwana Mtume Muhammad SAW kutoka Makka kwenda Madina lakini kwa kutegemea jua na si mwezi na ndio maana ukaitwa mwaka wa Hijria Shamsia. Karibuni.


*********

Nairuzi ni sherehe ambayo imedumu toka zama za kale na ingali inaadhimishwa. Kwa mujibu wa aghalabu ya ngano za kale na riwaya za kihistoria kuhusu Nairuzi, sikuukuu hii ilianzishwa na mfalme Jamshid katika silisila ya tawala za Pishdadi. Jamshid alikuwa mfalme wa nne katika silisila ya watawala wa Pishdadi na anatambuliwa kama muasisi wa siku kuu ya Nairuzi. Jamshid alikuwa mfalme aliyependwa sana na wananchi. Inasimuliwa kuwa katika siku zake, nchi ilifika katika kilele cha utajiri wa mali. Ferdowsi malenga wa tungo za hamasa wa Iran katika simulizi yake kuhusu kuibuka Nairuzi anasema wakati neema zilipokuwa nyingi katika nchi, aliwakusanya maafisa wote wa serikali na kuwashukuru. Jamshid aliwashukuru na kuwaenzi waliofanya kazi vizuri tarehe Mosi Farvardin ambayo ilikuwa siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza wa mwaka wa Hijria Shamsia. Aliitaja siku hiyo kuwa ni siku ya Nairuzi yaani siku mpya ya sherehe.
Pamoja na kuwa hakuna nyaraka kamili kuhusu historia ya Nairuzi, lakini ni jambo lisilo na shaka kuwa Nairuzi ni sherehe ya kale na ilikuwa ikisherehekewa katika ardhi ya Iran hata kabla ya kuwasili kaumu ya Arya. Kwa mujibu wa mtafiti Muirani Mehrdad Bahar, Nairuzi ni mila na desturi ya kale ambayo ilikuwepo millennia ya tatu kabla ya Miladia (Kuzaliwa Nabii Issa AS). Anaandika hivi: 'Sherehe hizo zilikuwa zikiadhimishwa na makabila ya asili ya wenye kuhamahama Iran.' Baadhi ya riwaya za kihistoria zinasema Nairuzi iliingia Iran mwaka 538 kabla ya kuzaliwa Masih Isa AS baada ya Kourosh kuliteka eneo la Babel. Riwaya hizo zinasema kuwa katika kukaribisha Nairuzi, Kourosh wa Pili alikuwa na mpango maalumu wa kuboresha maisha ya askari wake, kusafisha na kudumisha usafi katika maeneo ya umma na nyumba binafsi sambamba na kuwaachilia huru wafungwa.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa katika maandishi yaliyokuwa kwenye majabali katika zama za Wakhamaneshi kwenye karne ya 6 kabla ya kuzaliwa Nabii Isa AS, watu wa zama hizo walikuwa wakifahamu vyema mila na desturi za Nairuzi. Wafalme wa silisila ya Wakhamaneshi walikuwa wakifanya makaribisho maalumu ya kuipokea Nairuzi katika eneo maalumu la ibada lililojulikana kama Takht-e Jamshid yaani Persepolis huko Shiraz, Iran. Kwenye sherehe hizo maalumu wafalme walikuwa wakiwakaribisha watu kutoka kaumu na mataifa mbali mbali. Kila mwaka wawakilishi wa mataifa mbali mbali ya dunia, wakiwa wamevalia nguo zao za kienyeji na kitaifa walikuwa wakifika huko Takht-e Jamshid na kusherehekea sikukuu ya Nairuzi. Katika maadhimisho hayo, walikuwa wakimletea mfalme wa Iran zawadi zenye thamani kubwa.
Nyaraka za historia zinaonyesha kuwa, Mfalme Dariush wa Kwanza, katika mwaka wa 416 kabla ya kuzaliwa Masih Isa AS, alitengeneza sarafu za dhahabu kwa mnasaba wa Nairuzi. Sehemu moja ya sarafu hiyo ina taswira ya askari akirusha mshale. Katika zama za watalwa wa Washkani na Wassasani kuanzia karne ya 247 BC hadi karne ya 650 Miladia kuliendelea kufanyika sherehe za Nairuzi ambazo ziliadhimishwa kwa siku kadhaa mfululizo. Katika zama za Washkani siku kuu hii ilikuwa na duru mbili yaani Nairuzi ndogo na Nairuzi Kubwa. Katika zama za Wasassani, Nairuzi ilikuwa na duru ya Nairuzi ya Umma na Nairuzi Maalumu. Nairuzi ya umma ilidumu kwa muda wa siku tano kuanzia tarehe Mosi Farvardin na Nairuzi Maalumu ilikuwa siku ya sita ya Farvardin ambapo kulifanyika sherehe kubwa. Katika siku tano za kwanza za Nairuzi kulikuwa na karamu kwa ajili ya umma ambapo pia wananchi walipata fursa ya kutoa maombi yao. Katika siku ya sita ambayo ilikuwa ndio Nairuzi kubwa kulifanyika sherehe maalumu ya mfalme na watu wa karibu naye. Tunaweza kusema kwamba sherehe hiyo ilikuwa maalumu katika kasri la utawala.


*********


Baada ya kuingia Uislamu katika ardhi ya Iran, Wairani Waislamu waliendelea kuadhimisha sikukuu ya Nairuzi lakini kwa kuzingatia mafundisho, mila na desturi za Kiislamu. Katika zama za utawala wa Waseljuki walioanza kutawala Iran katika karne ya 10 Miladia kulifanyika mabadiliko katika kalenda kuhusu mwaka unaofuata jua yaani mwaka wa Shamsia. Mnamo mwaka 467 Hijria Qamaria sawa na mwaka 1,074 Miladia, Jalaluddin Malik Shah Seljuki aliwataka wanahisabati na wataalamu wa falaki yaani elimu ya nyota akiwemo Omar Khayyam Nishaburi wafanye utafiti juu ya namna ya kuifanyia marekebisho kalenda iliyokuwepo wakati huo. Wataalamu hao waliamua siku ya kwanza ya Nairuzi isadifiane na siku ya kwanza ya msimu wa machipuo na ndio maana kalenda ya Iran ikapewa pia jina la 'Kalenda ya Jalali' au 'Maliki'. Kimsingi ni kuwa kalenda hii ilienda sambamba na kalenda ya kimaumbile kikamilifu. Kwa hivyo si tu kuwa Nairuzi iko katika siku ya awali ya msimu wa machipuo, bali pia kalenda ya Jalali au Hijria Shamsia inaenda sambamba na misimu yote ya kimaumbile katika eneo hili. Mwaka wa kalenda ya Jalali haurudi nyuma hata siku moja na hii ni kinyume na Kalenda ya Miladia (Gregorian) ambayo baada ya kila miaka elfu 10 huwa na hitilafu ya takribani siku tatu.
Baada ya kudhihiri Uislamu nchini Iran hasa katika zama za utawala wa Wassafavi yaani karne za 10 na 11 Hijria Qamaria au karne ya 16 Miladia, sherehe za Nairuzi zilichanganywa na mila na desturi za Kiislamu na hivyo kupata uhai na ufahamu mpya. Hali kadhalika kuna riwaya za Kiislamu kuhusu umuhimu wa Siku Kuu ya Nairuzi jambo ambalo limefanya sherehe hizo zipate umuhimu zaidi hasa miongoni mwa Waislamu wa madhehebu ya Kishia. Kwa mujibu wa riwaya za Maulamaa wa Kishia, Nairuzi ni siku tukufu. Imam Ja'afar Sadiq AS amenukuliwa akisema kuwa Nairuzi ni siku ya furaha na iliyobarikiwa na kwamba Nabii Adam AS aliumbwa katika siku kama hii. Aidha kwa mujibu wa riwaya nyingine, tunasoma kuwa katika siku inayosadifiana na hii yaani mwaka wa 10 Hijria, Mtume Muhammad SAW, akiwa katika eneo lijulikanalo kama Ghadir Khum, alimtangaza Imam Ali AS kuwa mtu atakayechukua uongozi baada yake kama Khalifa wa Waislamu.
Kwa msingi huo Waislamu wa Iran wanaitambua Nairuzi kama siku yenye furaha na baraka na wameiambatanisha na utamaduni wa Kiislamu.
Mwaka 2009 Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi na Utamaduni UNESCO lilitangaza na kuisajili Nairuzi kama turathi ya kimaanawi duniani. Aidha Mwaka 2010 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilitangaza rasmi tarehe Mosi Farvardin yaani Machi 21 kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Nairuzi. Umoja wa Mataifa umeitambua Siku ya Nairuzi kama siku kuu ya kale ambayo huadhimishwa wakati wa kuwadia msimu wa machipuo na kuhuishwa tena maumbile. Kwa mujibu wa tovuti ya Umoja wa Mataifa, sikukuu ya Nairuzi hueneza thamani za amani na mshikamano wa vizazi katika familia sambamba na kuleta maelewano na ujirani mwema na hivyo kuwa na mchango mkubwa katika kudumisha urafiki baina ya watu wa jamii mbali mbali. Katika matini ya kuidhinishwa Nairuzi katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa imeandikwa kuwa: "Sherehe za Nairuzi zina mizizi ya Kiirani ya zaidi ya miaka 3,000 iliyopita na leo zaidi ya watu milioni 300 huadhimisha siku hii."
Mpenzi msikilizaji, kwa hayo machache ndio tunatamatisha dakika hizi chache za kukuleteeni makala hii maalumu. Ni matumaini yangu umefaidika vya kutosha.

 

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)