Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 22 Februari 2016 13:01

Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain (114)

Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain (114)

Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswaili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni moja kwa moja kutoka mjini Tehran. Tuna furaha kukutana tena katika sehemu hii ya 114 ya kipindi hiki cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain ambapo leo tutaanza kujadili maswali yanayohusiana na Uimamu baada ya kumaliza kujibu maswali yanayohusiana na Utume kwa ujumla na kadhalika Utume wa Mtume wa Mwisho al- Mustafa (saw). Swali linalojitokeza hapa ni kuhusu maana ya Uimamu uliotoka kwa Mwenyezi Mungu na tofauti iliyopo kati ya uimamu huu na Utume. Tunavirejea Vizito Viwili vya wongofu ili kupata jibu sahihi kuhusiana na swali hili muhimu, kwa hivyo kuweni nasi hadi mwisho wa kipindi ili tupate kunufaika na jibu la swali hili, karibuni.
*****
Wapenzi wasikilizaji tunaanza kujibu swali hili kwa kuashiria aya ambayo imetaja Utume na Uimamu kwa pamoja na ambayo inamzungumzia Sheikh wa Manabii, Nabii Ibrahim al-Khalil (as) nayo ni kauli ya Mwenyezi Mungu katika aya ya 124 ya Surat al-Baqarah inayosema: Na Mola wake alipomjaribu Ibrahim kwa matamko, naye akayazitimiza, akamwambia: Hakika Mimi nimekufanya Imam wa watu. Akasema: Na katika kizazi changu pia? Akasema: Ahadi yangu haiwafikii madhalimu.
Imam katika lugha ya Kiarabu wapenzi wasikilizaji, ina maana ya kufuatwa mtu katika maneno na vitendo vyake, na maana hii inajumuisha maimamu wa kufr na upotovu na vilevile maimamu wa haki na wongofu. Neno hili limetumika katika Qur'ani Tukufu na Hadithi kwa maana hii pana inayojumuisha makundi haya mawili ya maimamu.
Ni wazi kuwa Imam aliyekusudiwa katika aya tukufu tuliyotangulia kuisoma ni Imam wa haki aliyeteuliwa na Mwenyezi Mungu na Uimamu wake ni ule unaohesabiwa kuwa moja ya misingi ya dini ya haki.
Jambo la kwanza tunalojifunza kutokana na aya hii ni kuwa Uimamu ni ahadi ya Mwenyezi Mungu ambayo huijalia mtu anayemtaka kwa sharti kwamba asiwe miongoni mwa madhalimu. Kutokana na kuwa aya tukufu iliyotajwa imetumia neno madhalimu kwa upana wake na bila kuweka sharti lolote, tunafahamu kuwa Imam ambaye anateuliwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ahadi ya Uimamu anapasa kuwa maasumu moja kwa moja, yaani mtu asitenda dhambi kabisa.
*********
Wapenzi wasikilizaji, jambo tunalojifunza moja kwa moja kutokaa na aya hii ni kwamba Mwenyezi Mungu alimteua Nabii Ibrahim (as) kuwa Imam na kuhudumia nafasi hiyo baada ya utume. Nam, jambo hilo linabainika wazi mwanzo kutokana na ombi la Ibrahim al-Khalil kwa Mwenyezi Mungu ajaliye Uimamu kuwa katika kizazi chake. Imethibiti kupitia Qur'ani Tukufu kwamba Nabii Ibrahim (as) aliruzukiwa kizazi katika miaka ya mwisho ya umri wake na hili ni jambo ambalo linathibitishwa na aya kadhaa za kitabu hicho kitakatifu. Aya hizo zinasema kwamba kwanza Nabii Ibrahim (as) aliruzukiwa Ismail na kisha Is'haq akiwa katika umri huo mkubwa na kwa mujibu wa kanuni ya muujiza wa Mwenyezi Mungu kuhusiana na Is'haq kwa sababu mama yake, Sarah (as) alikuwa ajuza na mgumba kwa ibara ya Qur'ani Tukufu. Na Maimamu wa Ahlul Beit (as) wameashiria jambo hili katika Hadithi nyingi ikiwemo ile iliyopokelewa katika kitabu cha Uyun Akhbar ar-Ridha (as) ambayo inasema: 'Hakika Mwenyezi Mungu alimpa Ibrahim al-Khalil (as) Uimamu baada ya Unabii, na urafiki ni sehemu ya tatu na fadhila alizompa kama alama ya utukufu na kumsifu. Mwenyezi Mungu Mtukufu akasema: Hakika Mimi nimekufanya Imam wa watu. Naye Khalil (as) akasema: Na katika kizazi changu pia? Mwenyezi Mungu akasema: Ahadi yangu haiwafikii madhalimu. Kwa hivyo aya hii ilibatilisha uimamu wa kila dhalimu hadi Siku ya Kiama na hivyo kuwa kweye vitu bora na halisi.'
Imepokelwa katika kitabu cha Usuul al- Kafi kutoka kwa Imam wetu as-Swadiq (as) kwamba alisema: 'Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu alimfanya Ibrahim kuwa mja kabla ya kumpa Unabii, Nabii kabla ya kumfanya Mtume, Mtume kabla ya kumteua kuwa Rafiki na alimfanya kuwa Rafiki kabla ya kumteua kuwa Imam. Baada ya kumpa mambo hayo yote, yaani uchaji Mungu, Unabii, Utume na Urafiki – alisema: Hakika Mimi nimekufanya Imam wa watu. Kisha Imam Swadiq (as) akasema - na katika muhimu zaidi kati ya haya – yaani Uimamu – katika mtazamo wa Ibrahim (as), akasema: Na katika kizazi changu pia? Akasema Mwenyezi Mungu: Ahadi yangu haiwafikii madhalimu..... Alisema, mtu mjinga hawi Imam mcha Mungu.'
*************
Wapenzi wasikilizaji, tunarejea katika aya tukufu tuliyoisoma mwanzoni na kupata kuwa Mweyezi Mungu alimpa rafiki yake Ibrahim cheo cha Uimamu baada ya kumpa mtihani mgumu wa matamko na akafaulu katika mtihani huo. Je, nini maana ya suala hili? Bila kujali makusudio ya maneno yaliyotumika kwenye aya hii, la muhimu ni kuwa matamko hayo yalikuwa matamko ya Mwenyezi Mungu ambayo alimtahini kwayo rafiki Yake Ibrahim (as) ili apate kushinda na kufaa kupewa nafasi muhimu ya Uimamu na hivyo kufikia ahadi ya Mwenyezi Mungu. Matamko hayo ni njia ya kuthibiti hakika ya Tauhidi ambayo hutumika kwa ajili ya kumuwezesha mwanadamu kuwa na sifa na maadili yanayotakiwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu katika maneno na matendo yake yote kwa ajili ya kumfanya mtu kama huyo kuwa mfano mwema na usiotenda dhambi kwa akili ya kuwaongoza wanadamu wenzake kwenye njia sahihi na iliyonyooka.
Jambo la pili ni kuwa kufaulu katika kujua na kuchambua matamko hayo humuandaa mwanadamu mwema kwa ajili ya kutekeleza vyema ahadi maalumu ya Mwenyezi Mungu iliyoko kwenye Uimamu wa mbinguni. Tunaona kwamba aya hii inazungumzia mazungumzo yaliyojiri kati ya Mwenyezi Mungu na rafiki yake Ibrahim (as) na hii ni dalili nyingine inayothibitisha kupata kwake Wahyi wa Mwenyezi Mungu akiwa ni Mtume na Imam.
*************
Ndugu wasikilizaji, muhtasari wa mambo tuliyosoma kwenye kipindi hiki ni kuwa Qur'ani Tukufu inatwambia wazi kwamba Uimamu mwanzo ni ahadi ya Mwenyezi Mungu ambayo humpa mja wake mwema madamu awe ni maasumu mutlaki, yaani asiyetenda dhambi kwa njia yoyote ile.
Uimamu huu sio cheo cha Unabii wala Utume bali yumkini vyeo hivi vyote vikakusanyika sehemu moja au Uimamu huu ukakusanyika na moja ya vyeo hivi. Huenda pia usikutane na vyeo viwili hivi kwa sababu Nabii Ibrahim (as) aliomba kizazi chake kipewe cheo hiki nao si wote waliokuwa Manabii. Kwa hivyo Mwenyezi Mungu hakuufungamanisha na Manabii bali alijibu kwa kusema kuwa Madhalimu hawakipati cheo hiki.
Na kwa natija hii iliyo wazi ndio tunafikia mwisho wa kipindi cha juma hili cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain ambacho mmekisikiliza kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Tunakushukuruni nyote kwa kuwa pamoja nasi hadi mwisho wa kipindi....
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)