Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 19 Januari 2016 12:09

Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain (113)

Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain (113)

Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji na karibuni kusikiliza sehemu ya 113 ya kipindi hiki cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain ambacho kinakujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutoka hapa mjini Tehran. Kama mnavyojua kipindi hiki hujibu maswali mbalimbali yanayohusiana na itikadi ya Kiislamu kuhusu masuala tofauti. Katika vipindi kadhaa ambavyo tumekuwa tukivizungumzia katika wiki chache zilizopita tumekuwa tukijadili haki za Mtukufu Mtume (saw) kwa Waislamu na tayari tumekwishazungumzia haki 12 kati ya haki hizo na majukumu tuliyonayo kuhusiana na mtukufu huyo (saw). Kutokana na umuhimu wa suala hili katika kipindi cha leo tutatoa muhtasari wa haki hizo kumi na mbili pamoja na kubainisha yanayokusudiwa kwenye haki hizo, hivyo kuweni nasi hadi mwisho wa kipindi hiki, karibuni.
************
Haki ya kwanza ya Nabii Muhammad (saw) ambayo tunaifahamu kutokana na maandiko matakatifu ni haki ya kutiiwa na kufuatwa katika kila jambo analotuamuru kulifanya au kutolifanya kwa sababu kutiiwa Mwenyezi Mungu kunafungamana moja kwa moja na kutiiwa Mtume Mtukufu (saw). Kufuatwa Mtume (saw) ni njia ya kufuzu na kufaulu na vilevile kupendwa wafauasi wake na Mwenyezi Mungu, katika hali ambayo kutotekeleza haki hii ya Mtume (saw) ni chanzo cha kubughudhiwa na kukasirikiwa walioasi na Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu anasema katika aya mbili za 31 na 32 za Surat Aal Imran: Sema: Ikiwa nyinyi mnampenda Mwenyezi Mungu basi nifuateni mimi, Mwenyezi Mungu atakupendeni na atakufutieni madhambi yenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kufuta madhambi na Mwenye kurehemu. Sema: Mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume. Na wakikataa basi hakika Mwenyezi Mungu hawapendi makafiri. Na haki hii ya Mtume hutekelezwa kwa kutekelezwa wasia wake (saw) kupitia hadithi sahihi zilizopokelewa kutoka kwake na pia kutiiwa wale watu ambao Mwenyezi Mungu ameamuru watiiwe katika Maimamu na Itra ya Mtukufu Mtume (saw) ambayo ni maasumu na wala haitendi dhambi (as), kama inavyoashiria wazi jambo hilo aya ya 59 katika Surat an-Nisaa inayosema: Enyi mlioamini! Mt'iini Mwenyezi Mungu, na mt'iini Mtume na wenye mamlaka katika nyinyi. Na mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, ikiwa mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Hilo ni bora zaidi na mwisho mzuri.
Ama haki ya pili ya Mtume Mtukufu (saw) ni haki ya kurejea kwake na kuhukumiwa naye wakati hitilafu zinapotokea kati ya Waislamu au kwenye jamii ya Kiislamu na kuridhia hukumu inayotolewa naye kama inavyosema sehemu ya aya hiyohiyo ya 59 ya Surat an-Nisaa: ......Na mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, ikiwa mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Hilo ni bora zaidi na mwisho mzuri.
Haki hii ya Mtume (saw) huthibiti kwa kurejea kwenye hadithi na sunna sahihi za Mtume ili kujua ukweli wa mambo, na vilevile kurejea kwa walio na mamlaka katika jamii na Umma wa Kiislamu ambao ni Maimamu maasumu (as) kama inavyoashiria hilo kauli ya Mwenyezi Mungu katika aya ya 83 ya Surat an-Nisaa: Na linapowafikia jambo lolote linalohusu amani au la hofu wao hulitangaza. Na lau wangelirejesha kwa Mtume na kwa wenye mamlaka katika wao, wangejua wale wenye kuchunguza katika wao. Na lau si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema yake mngemfuata shetani isipokuwa wachache wenu tu.
Ni wazi kuwa utekelezaji wa haki hii humuwezesha mja kukwepa mitego ya shetani na hivyo kufaulu kwa kile kilicho cha heri na mwisho mzuri.
************
Wapenzi wasikilizaji haki ya tatu ya Mtume Muhammad (saw) kwa Umma wa Kiislamu ni haki ya kumuonyesha mahaba na mapenzi na kuyatanguliza mahaba hayo juu ya mahaba mengine yote. Mapenzi haya kwa Mtume hutimia kwa kumpenda kwanza Mwenyezi Mungu kwa sababu Yeye ndiye kipimo cha mapenzi yote halisi. Utekelezaji wa haki hii ya kumpenda Mtume huthibiti kwa kujiweka mbali pamoja na kuwachukia kwa moyo maadui wote wanaomchukia Mtume wa Mwenyezi Mungu na Watu wa Karibu na Mtume (saw), tokea watu wa mwanzoni hadi wa mwisho. Na haki ya nne ya Mtume Muhammad (saw) ambayo inasisitizwa na maandiko matakatifu ni haki ya kuswaliwa wakati jina lake (saw) linapotajwa. Utekelezwaji wa haki hii husisitizwa zaidi jina la Mtume (saw) linapotajwa, na ni wajibu kumswalia wakati wa kutoa tashahhud kwenye swala kwa namna na matamshi ambayo yamepokelewa kwenye hadithi za Mtume Mwenyewe (saw). Kumswalia huko ni kule kunakojumuisha kuswaliwa yeye pamoja na Watu wa Nyumba yake na kujiepusha kutoa swala ambayo haiandamani na swala ya Ahlul Beit wake (as). Mtume amekataza kuswaliwa bila kujumuishwa Ahlul Beit wake kwenye swala hiyo kama ilivyopokelewa kwa njia sahihi na madhehebu zote za Kiislamu.
Wapenzi wasikilizaji ama haki ya tano ya Mtume Mtukufu (saw) ni haki ya kuheshimu, kutukuza na kumuadhimisha kama alivyoadhimishwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu mwenyewe kwa kusema: 'Na hakika wewe una tabia tukufu,' na kuamuru kutekelezwa jambo hilo katika aya nyingi za Qur'ani Tukufu zikiwemo za mwanzoni katika Surat al-Hujuraat. Kutekelezwa haki hii hutimia kama zinavyotuamuru aya hizi tukufu kuwa tunapaswa kumtaja Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) kwa majina na sifa za heshima kama alivyofanya Allah mwenyewe, kwa mfano kwa kumtaja kuwa ni Mtume wa Mwisho na Mtume wa Mwenyezi Mungu na kuepuka kutaja jina lake au kumwita kama tunavyoitana sisi kwa sisi. Vilevile tunatakiwa kuepuka kupaza sauti zetu wakati tunapomzuru Mtume (saw) kwenye kaburi lake tukufu, na kuingia msikitini kwake baada ya kumuomba idhini na kumtaja kwa heshima kwenye vitabu na sehemu nyinginezo.
Ama haki ya sita ni haki ya kumpa beia Mtume Mtukufu (saw) ambayo ina maana kwamba tuko tayari kumpa msaada na kumnusuru katika maisha yake na baada ya kuaga dunia kwa kutetea kwa moyo na nguvu zetu zote njia yake takatifu na kupiga vita kila jambo linalomdhihaki na kumvunjia heshima (saw).
************
Ndugu wasikilizaji na haki ya saba kati ya haki za Mtume Mtukufu (saw) ni haki ya kumzuru na kumuomba Allah maghfira kupitia kwake (saw) katika zama za uhai wake na baada ya kuaga kwake dunia, iwe ni kwa karibu au kutokea mbali kama yanavyosisitiza hilo maandiko mengi matakatifu.
Kati ya haki zake pia ni haki ya kutoa khumsi kwa ajili yake, yaani khumsi inayozidi matumizi yetu ya mwaka. Haki hii hutimia baada ya kuaga kwake dunia kwa kupewa makhalifa wake maasumeena kama inavyosisitizwa kwenye vitabu vya fiqhi. Na maandiko matakatifu yanatuarifu kwamba Mtume Mtukufu (saw) ana haki ya kuwa bababa wa kimaanawi kwetu waumini wa Kiislamu na Umma mzima wa Kiislamu hadi Siku ya Kiama. Kwa msingi huo inatupasa sisi Waislamu kuamiliana na Mtume kama watoto wanavyoamiliana kwa heshima na wazazi wao tena kwa kiwango cha juu kabisa. Kwa mfano tunapasa kufanya kila jambo ili kupata ridhaa yake na kumshukuru pamoja na kumuombea dua na mambo mengine kama hayo ambayo ni miongoni mwa haki alizonazo mzazi kwa wanawe kama inavyosisitizwa kwenye Qurani na hadithi tukufu.
Ama haki ya kumi ya Mtume Mtukufu (saw) wapenzi wasikilizaji ni haki ya kuwapenda watu wa karibu na Ahlu Beit wake watoharifu (as) kama zinavyotambia hilo aya za Surat as-Shuraa na pia hadithi tukufu. Maandiko haya matakatifu yanatwambia kwamba haki hii inatulazimu sisi Waislamu kuheshimu na kukipenda kizazi cha Mtukufu Mtume (saw) na kukifanyia hisani.
Kujiepusha kumuudhi Mtume (saw) katika uhai wake na baada ya kuaga kwake dunia ni haki yake nyingine ambayo tunatakiwa kuizingatia na kuiheshimu. Haki hii kama zilivyo haki zake nyingine, imesisitizwa sana katika Qur'ani na hadithi tukufu. Mfano wa wazi zaidi kuhusiana na jambo hili, ni kutowaudhi Watu wa Nyumba na Ahlul Beit wake (as) na pia kutomuudhi kwa kutenda maovu na dhambi.
Nam, suala hili limezungumziwa kwa urefu na aya takatifu na kubainishwa kwa kina na hadithi nyingi zilizo sahihi ambazo zinasisitiza kwamba Mwenyezi Mungu humfahamisha Mtume wake (saw) akiwa kwenye Barzakh matendo ya wafuasi na Umma wake, ambapo humuudhi matendo yao mabaya na kumfurahisha matendo yao mema.
Na haki ya kumi na mbili ya Mtume Mtukufu (saw) na ambayo ni haki muhimu na kubwa zaidi kuliko haki zote tulizozitaja na utekelezaji wake ni wajibu mkubwa zaidi kuhusiana na Mtume Mtukufu (saw) ni haki ya kulinda na kuhifadhi amana zake mbili alizotuachia humu duniani ambazo ni Kitabu Kitakatifu cha Mwenyezi Mungu (Qur'ani Tukufu na Itra pamoja na Watu wa Nyumba yake (as). Alituachia amana mbili hizi ili zipate kuwa minara miwili ya kutuongoza kwenye njia nyoofu na kutuepusha na upotovu. Kutekeleza haki hii ya kulinda amana mbili hizi ambazo mara nyingine hutajwa kuwa Vizito Viwili kwa hakika huthibiti kwa kushikamana navyo kikamilifu na kutovipuuza kwa sababu Mtume ametuahidi kwamba viwili hivi havitaachana hadi vitakaporejea kwake (saw) kwenye Hodhi Takatifu.
Tunamwomba Mwenyezi Mungu atupe sote wapenzi wasikilizaji taufiki ya kuweza kutekeleza haki hizi za Mtume Mtukufu (saw) kwa baraka za kushikamana na amana mbili hizi takatifu za al-Mustafa (saw).... Allahumma Ameen.
Na kufkia hapa ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain ambacho kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu kutoka hapa mjini Tehran. Basi hadi tutakapopata fursa nyingine ya kukutana nanyi tena wapenzi wasikilizaji katika kipindi kingine cha Maswali yetu na Majibu ya Thaqalain, tunakuageni nyote kwa kusema Wassalaam Aleikum Wararahmatullahi Wabarakatuh.

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)