Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Alkhamisi, 07 Januari 2016 16:51

Madhara ya simu za mkononi kwa afya ya watoto

Madhara ya simu za mkononi kwa afya ya watoto

Katika makala hizi tunaangazia namna teknolojia hizo zinavoweza kuwa na faida na pia madhara kwa mwanadamu na yote yanategemea namna zinavyotumiwa. Katika makala yetu iliyopita tulisema kuwa wataalamu wanasema utumizi wa muda mrefu wa simu za mkononi ambao huambatana na kulengwa kwa muda mrefu na sumaku pamoja miale ya kielektroniki ni jambo lenye madhara makubwa kwa afya ya mwandamu. Kati ya madhara tunayoweza kuashiriki hapa ni kama vile kupungua uwezo wa ubongo kuhifadhi mambo, kuhisi uchovu, kukosa usingizi, saratani, uvimbe wa ubongo, utasa na ugumba. Tulisema wataalamu wanashauri kuwa usiweke simu karibu na moyo au eneo la kiuno. Inashauriwa pia kuwa simu ibebwe kwenye mfuko ule ambao hauko katika nguo ili athari zake mbaya zipungue. Katika makala hii tutaangazia baadhi ya madhara ya simu za mkononi kwa watoto.

Taathira hasi za utumizi wa simu za mkononi  huwa na madhara zaidi kwa watoto wadogo. Wataalamu katika nchi mbali mbali wametoa tahadahri kuhusu hatari ya utumizi wa simu za mkononi miongoni mwa watoto. Tahadhari hizo zimepewa uzito mkubwa kiashi kwamba katika baadhi ya nchi kama vile Uswisi, Austria na Canada huwa kunatolewa tahadhari kwa umma kuhusu hatari ya utumizi wa simu za mkononi miongoni mwa watoto na mabarobaro walio katika kundi la umri wa chini ya miaka 16. Wataalamu wanasema kundi hili huathiriwa vibaya  sana na miale ya kielektroniki na nguvu za sumaku au magnetism. Wataalamu wanasema watoto ambao wanatumia simu za mkononi hukabiliwa na hatari mara tano zaidi ya kupata aina mbali mbali za uvimbe wa ubongo.

Kwa mujibu wa ripoti iliyochapishwa na gazeti la Daily Telegraph, uchunguzi uliofanywa na wasomi wa Sweden wamebaini kuwa watoto walio chini ya umri wa miaka 16 huathirika mara tano zaidi na miale hatari ya simu za mkononi kutokana na kuwa mfumo wa ubongo wao huwa bado unastawi. Wataalamu hao wanasema uchunguzi wao umebaini kuwa watoto walio chini ya umri wa miaka 12 wanapaswa tu kutumia simu za mkononi iwapo kuna jambo la dharura sana. Chuo Kikuu cha Alabama huko Birmingham Uingereza kimefanya utafiti na kubaini kuwa asilimia 77 ya watoto walio na umri wa kati ya miaka 10 na 11 huwa na hatari ya kugongwa na gari wanapovuka barabra. Utafiti huo umebaini watoto wenye umri huo kawaida hawangalii pande zote mbili wanapovuka barabara. 

Kutokana na kuwa wanaadamu leo hawana budi ila kutumia vyombo vya kielektroniki kama vile simu za mkononi katika maisha yao ya kawaida, wataalamu hivi sasa wanafanya utafiti wa kina ili kutafuta njia za kukabiliana na kuangamiza taathira kwa mwili wa mwanadamu wakati anakumbwa na miale ya kielektroniki na nguvu za sumaku.

Kwa hivyo, kutokana na madhara mengi yaliyopo katika utumizi wa simu za mkononi, inashauriwa kuwa watoto wa umri wa chini ya miaka 16 wasitumia chombo hicho na watu wazima wanaotumia wakitumie kwa wastani.

Katika uhalisia wake, simu ya mkononi ni chombo cha mawasiliano wakati wa dharura na mazungumo kwa njia hiyo yanapaswa kuwa ni mafupi.

Badala ya kutumia simu ya mkononi katika mazungumzo ya muda mrefu inashauriwa kutumia simu ya mezani au kukutana ana kwa ana kwa kuzingatia madhara yapatikanayo ambayo huhatarisha maisha ya mwanadamu.

Hakuna shaka kuwa uvumbuzi wa kila siku katika uga wa teknolojia ya habari na mawasiliano au Tecnohama huwa ni kwa maslahi ya mwanadamu kwa lengo la kurahisisha na kuboresha maisha.

Bila shaka hakuna yeyote apendaye kuhatarisha afya yake kutokana na utumizi wa teknolojia za kisasa. Hivyo tunapaswa kujifunza utumizi sahihi wa teknolojia hizi ili ziwe na zenye kutuhdumia badala ya kutudhuru. Lakini la kusikitisha ni kuwa kuna uzingatiaji mdogo sana wa masuala ya afya katika utumizi wa vifaa vya kielektroniki hasa simu za mkononi au mobile. Hii ni kwa sababu aghalabu ya watu huhadaiwa na matangazo ya kibiashara ya kuvutia kutoka katika mashirika yenye kutengeneza simu za mkononi. Baadhi yetu tumetekwa na matangazo hayo ya biashara kiasi kwamba tunaghafilika na hatari mbaya za simu za mkononi kwa afya ya kimwili na kiroho ya watoto wetu. Ni kwa msingi huo ndio hata baadhi husonga mbele zaidi na kuwanunulia watoto wao simu za mkononi hata pasina kuwafundisha utamaduni sahihi wa kutumia chombo hicho.

Hii ni katika hali ambayo kutozingatia utumizi sahihi wa teknolojia ya simu ya mkononi husababisha matatizo na madhara makubwa kwa jamii na utamaduni miongoni mwa watoto na mabarobaro walio na umri wa chini ya miaka 16. Upuuzwaji wa madhara ya afya ya kimwili na kiroho katika utumizi wa  simu za mkononi huwa na taathira mbaya kwa wale wanaotumia teknolojia hiyo wakia na umri mdogo.

Kutokana na kubanwa na wakati makala yetu ya teknolojia za kisasa na taathira zake katika mtindo wa maisha  inafikia inafikia tamati hapa kwa leo.

Tek 29----B

Wataalamu katika uchunguzi wao wamebaini kuwa ni vigumu kwakataza na kuwazuia kikamilifu watoto na mabarobaro kutumia simu za mkono na kwa msingi huo kile kinachopaswa kufanyika ni  kuhakikisha utumizi wa chombo hicho unafanyika kwa njia ambayo hakutakuwa na natija hasi  au utumizi usio sahihi. Uchunguzi umebaini simu ya mkononi  na vitu mshabaha kama vile tablet huwa na tathira hasi na mbaya sana katika mkondo wa masomo ya wanafunzi. Watoto na mabarobaro wanaishi katika kipindi cha kuinukia ambapo wengi siku hizi wanamiliki simu ya mkononi yenye uwezo wa kupiga na kutuma picha, video na jumbe fupi. Simu ya mkononi huibua msisimko bandia ambapo kwa mfano wakati mwingi hutumiwa na vijana na mabarobaro wakisikiliza muziki au kutizama filamu. Kwa msingi huo wao huwa na wakati mdogo sana wa kushughulikia masomo hayo na natija yake huwa ni kudororo katika masomo. Baadhi ya wanafunzi huingia kwa siri na simu za mkononi darasani na kuanza kuzitumia pasina mwalimu kufahamu jambo ambalo hupelekea kutozingatiwa msomo.

Tatizo  sugu hivi sasa katika utumizi wa simu za mkononi miongoni mwa watoto na mabarobaro ni utumizi unaokiuka maadili hasa katika kutizama picha au video chafu ambapo mbali na hata kuzitamza wengine huzisambaza kwa wenzao. Hivi sasa imekuwa vigumu sana kwa wazazi na waalimu kudhibiti utumizi huo mbovu. Kwa msingi huo baadhi ya wazazi na walimu ili kuepuka tatizo hilo wameamua kupiga marufuku kabisa utumizi wa simu za mkononi miongoni mwa watoto na mabarobaro nyumbani na shuleni.

Tatizo jingine la utumizi wa simu za mkononi miongoni mwa wanafunzi shuleni ni kuwa watumizi huwa wanashindwa kuanzisha uhusiano bora na halisi wa kijamii na badala yake hujikita katika uhusiano kwa njia ya intaneti. Kwa msingi huo iwapo utumizi wa mitandao ya kijamii utafika kiwango cha uraibu mwenye kutegemea mawasiliano kwa njia hiyo, mtoto hukumbwa na matatizo anapoingia katika jamii ya kawaida na kukutuana na watu ana kwa ana. Hivi sasa  inashuhudiwa mara kadhaa namna vijana mabarobaro wanavotumia simu zao za mkononi na kuwapuuza hata marafiki walio karibu nao. Ifahamike kuwa mawasiliano kupitia jumbe fupi na mitandao ya kijamii kama whatsapp haipaswi kuchukua nafasi ya mazungumzo ya ana kwa ana baina ya wanadamu. Kadiri fursa inapopatikana wanadamu wanapaswa kuzungumza ana kwa ana.  Hii ni kwa sababu uhusiano usio wa mazungumzo huondoa zile hisia za ukuruba  na mahaba baina ya watu.

Baadhi ya familia huwanunulia watoto simu za mkononi ili wazitimue wakiwa nje ya nyumba na kwa njia hiyo kuondoa wasiwasi kuhusu waliko. Ni jambo linalotarajiwa kwa familia kufadhilisha kutumia simu kufuatilia kila lahadha ya waliko watoto.  Lakini ifahmike kuwa pasina kuwapa simu za mkononi , wazazi wenye uwezo bado wanaweza kudhibiti mwendo wa watoto wao kwa kuwapa chombo maalumu cha GPS chenye kuonyesha ramani ya mtoto aliko na kwa njia hiyo hakutakuwa na haja ya kutumia simu ya mkononi.

Hivi sasa aghalabu ya familia huwaruhusu watoto kuwa na simu za mkononi paisna kujali taathira zake hasi. Kwa vyovyote vile, kutumia simu za mkononi na teknolojia zinginezo zinazoshabihiana na chombo hicho ni jambo lenye hasara katika maisha ya ya mwanadamu.

Kama ambavyo katika kila jamii watu wanahitaji kutumia teknolojia za kisasa, utumizi   huo unapaswa kuandamana na nidhamu maalumu. Chombo cha mawasiliano kama mobile au simu ya mkononi kwa nafsi yake haiwezi kuwa na athari haribifu kwani madhara mabaya hutokana na utumizi usio sahihi wa chombo kama hicho. Kwa msingi huo tunapaswa kutafuta njia sahihi za kutumia teknolijia hii hasa miongoni mwa watoto na mabarobaro ambao wanatakiwa kufunza adabu na nidhamu ya kutumia  simu za mkononi, tablet, kompyuta, intaneti na teknolojia  zingine zote za habari na mawasiliano.

Kwa hivyo, kuna ulazima wa kujifunza kuhusu utamaduni wa utumizi sahihi wa teknolojia za sasa za habari na mawasiliano. Ni jukumu la wazazi, walimu na walezi kwa ujumla  kujifunza kuhusu teknolojia za kisasa za mawasiliano kama vile simu za mkononi n.k ili nao waweze kutoa mafunzo sahihi ya kutumia teknolojia hizo kwa watoto na mabarobaro.

Iwapo mitaala ya elimu katika kila nchi itazingatia umuhimu wa kutoa mafunzo kwa wanafunzi kuhusu utumizi wa teknoloijia za kisasa za mawasiliano, jambo hilo linaweza kuwa na nafasi muhimu sana. Watoto na mabarobaro wakifunzwa namna ya kuishi na kujiimarisha nafsi zao sambmba na kujiamini basi wataweza kusema kwa kauli moja, “la” kwa mambo yote yanayokiuka maadili kupitia simu za mkononi au intaneti kama vile picha na video chafu na za ufuska. Kunapaswa kutolewa mifano hai kuhusu madhara ya utumizi usio sahihi wa simu za mkononi. Kwa ujumla ni kuwa kujenga imani sahihi ya maadili bora ni jambo ambalo litawawezesha watoto na mabarobaro kutotumbukia katika mtego wa utumizi usio sahihi wa simu za mkononi.

Jukumu hili halipaswi kuachiwa upande moja tu bali walimu, wazazi na walezi wote wana nafasi yao katika kuwaongoza wanafunzi. Familia hasa zinakuwa na nafasi muhimu zaidi kwani simu za mkononi hununuliwa na wazazi au walwezi hivyo watoto wanaponunuliwa chombo hicho cha mawasiliano wanapaswa kufunzwa kuhusu utumizi sahihi na wafahamishwa hatari zinazoweza kuambatana na utumbizi mbovu wa simu za mkononi , tablet n.k.

Kuimarisha imani na itikadi za kidini miogoni mwa wanafunzi na kukita mizizi ya kutotazama na kuchukizwa na picha na filamu chafu kimaadili ni mambo yanayoweza kutoa mchango mkubwa katika kutatua tatizo hilo.

Kwa kumalizia hapa tunapaswa kusema kuwa, si watoto na mabarobaro pekee wanaopaswa kujifunza kuhusu utumizi sahihi wa simu za mkononi na teknolojia zinazoambatana na simu hizo kama vile intaneti, bali pia hata watu wazazi na wazima nao pia wanapaswa kujifunza kuhusu utumizi sahihi wa teknolojia hii ili wawe mfano bora kwa watoto na mbarobaro.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)