Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Alkhamisi, 24 Disemba 2015 12:04

Simu za mkononi ni hatari kwa afya ya watoto

Simu za mkononi ni hatari kwa afya ya watoto

Katika makala yetu iliyotangulia tulisema kuwa wataalamu wanasema utumizi wa muda mrefu wa simu za mkononi ambao huambatana na kulengwa kwa muda mrefu na sumaku pamoja na miale ya kielektroniki ni jambo lenye madhara makubwa kwa afya ya mwandamu. Kati ya madhara tunayoweza kuashiriki hapa ni kama vile kupungua uwezo wa ubongo kuhifadhi mambo, kuhisi uchovu, kukosa usingizi, saratani, uvimbe wa ubongo, utasa na ugumba. Tulisema wataalamu wanashauri kuwa usiweke simu karibu na moyo au eneo la kiuno. Inashauriwa pia kuwa simu ibebwe kwenye mfuko ambao hauko katika nguo ili athari zake mbaya zipungue. Katika makala hii tutaangazia baadhi ya madhara ya simu za mkononi kwa watoto. Karibuni kujiunga nasi hadi mwisho wa kipindi.

Taathira hasi za utumizi wa simu za mkononi huwa na madhara zaidi kwa watoto wadogo. Wataalamu katika nchi mbali mbali wametoa tahadahri kuhusu hatari ya utumizi wa simu za mkononi miongoni mwa watoto. Tahadhari hizo zimepewa uzito mkubwa kiasi kwamba katika baadhi ya nchi kama vile Uswisi, Austria na Canada huwa kunatolewa tahadhari kwa umma kuhusu hatari ya utumizi wa simu za mkononi miongoni mwa watoto na mabarobaro walio katika kundi la umri wa chini ya miaka 16. Wataalamu wanasema kundi hili huathiriwa vibaya sana na miale ya kielektroniki na nguvu za sumaku au magnetism. Wataalamu wanasema watoto ambao wanatumia simu za mkononi hukabiliwa na hatari mara tano zaidi ya kupata aina mbali mbali za uvimbe wa ubongo.

Kwa mujibu wa ripoti iliyochapishwa na gazeti la Daily Telegraph, uchunguzi uliofanywa na wasomi wa Sweden umebaini kuwa watoto walio chini ya umri wa miaka 16 huathirika mara tano zaidi na miale hatari ya simu za mkononi kutokana na kuwa mfumo wa ubongo wao huwa bado unastawi. Wataalamu hao wanasema uchunguzi wao umebaini kuwa watoto walio chini ya umri wa miaka 12 wanapaswa tu kutumia simu za mkononi iwapo kuna jambo la dharura. Chuo Kikuu cha Alabama huko Birmingham Uingereza kimefanya utafiti na kubaini kuwa asilimia 77 ya watoto walio na umri wa kati ya miaka 10 na 11 huwa na hatari ya kugongwa na gari wanapovuka barabra. Utafiti huo umebaini watoto wenye umri huo kawaida hawaangalii pande zote mbili wanapovuka barabara. 

Kutokana na kuwa wanaadamu leo hawana budi ila kutumia vyombo vya kielektroniki kama vile simu za mkononi katika maisha yao ya kawaida, wataalamu hivi sasa wanafanya utafiti wa kina ili kutafuta njia za kukabiliana na kuangamiza taathira kwa mwili wa mwanadamu wakati anakumbwa na miale ya kielektroniki na nguvu za sumaku.

Kwa hivyo, kutokana na madhara mengi yaliyopo katika utumizi wa simu za mkononi, inashauriwa kuwa watoto wa umri wa chini ya miaka 16 wasitumie chombo hicho na watu wazima wanaotumia wakitumie kwa wastani.

Katika uhalisia wake, simu ya mkononi ni chombo cha mawasiliano wakati wa dharura na mazungumo kwa njia hiyo yanapaswa kuwa ni mafupi.

Badala ya kutumia simu ya mkononi katika mazungumzo ya muda mrefu inashauriwa kutumia simu ya mezani au kukutana ana kwa ana kwa kuzingatia madhara yanayopatikana katika mawasiliano ya aina hiyo ambayo huhatarisha maisha ya mwanadamu.

Hakuna shaka kuwa uvumbuzi wa kila siku katika uga wa teknolojia ya habari na mawasiliano au tecnohama huwa ni kwa maslahi ya mwanadamu kwa lengo la kurahisisha na kuboresha maisha.

Bila shaka hakuna yeyote anayependa kuhatarisha afya yake kutokana na utumizi wa teknolojia za kisasa. Hivyo tunapaswa kujifunza utumizi sahihi wa teknolojia hizi ili ziwe ni zenye kutuhdumia badala ya kutudhuru. Lakini la kusikitisha ni kuwa kuna uzingatiaji mdogo sana wa masuala ya afya katika utumizi wa vifaa vya kielektroniki hasa simu za mkononi au mobile. Hii ni kwa sababu aghalabu ya watu huhadaiwa na matangazo ya kibiashara ya kuvutia kutoka katika mashirika yenye kutengeneza simu za mkononi. Baadhi yetu tumetekwa na matangazo hayo ya biashara kiasi kwamba tunaghafilika na hatari mbaya za simu za mkononi kwa afya ya kimwili na kiroho ya watoto wetu. Ni kwa msingi huo ndio hata baadhi husonga mbele zaidi na kuwanunulia watoto wao simu za mkononi hata pasina kuwafundisha utamaduni sahihi wa kutumia chombo hicho.

Hii ni katika hali ambayo kutozingatia utumizi sahihi wa teknolojia ya simu ya mkononi husababisha matatizo na madhara makubwa kwa jamii na utamaduni miongoni mwa watoto na mabarobaro walio na umri wa chini ya miaka 16. Upuuzwaji wa madhara ya afya ya kimwili na kiroho katika utumizi wa simu za mkononi huwa na taathira mbaya kwa wale wanaotumia teknolojia hiyo wakiwa na umri mdogo.

Wapenzi wasikilizaji kutokana na kubanwa na wakati makala yetu ya teknolojia za kisasa na taathira zake katika mtindo wa maisha inafikia tamati hapa kwa leo.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)