Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatano, 10 Aprili 2013 17:45

Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain (7)

Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain (7)

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kusikilizi kipindi cha saba katika mfulullizo wa vipindi hivi vya Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain ambavyo hukujieni siku na wakati kama huu kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Tulisema katika kipindi kilichopita kwamba dunia ni moja kati ya neema kubwa na muhimu tulizotunukiwa na Mwenyezi Mungu. Tulifafanua kwamba dunia ni shamba ambalo mwanadamu anapasa kupanda na kuvuna mavuno ambayo yatamfaidi katika maisha yake ya baadaye huko Akhera kwa sababu dunia ni mahala pa kupitia tu na sio makao yetu ya kudumu milele bali makao hayo yako huko Akhera.

Bila shaka mngali mnakumbuka kwamba tulisema katika kipindi hicho kwamba dunia ni sehemu ya mwanadamu kukusanya na kujidhaminia masurufu yake kwa ajili ya maisha yake ya milele huko Akhera. Kwa kuzingatia umuhimu ambao umepewa dunia katika hatua hii muhimu ya maisha ya mwandamu, tuliuliza swali nyeti mwishoni mwa kipindi hicho kwamba je, kama ukweli ni huo basi ni kwa nini dunia imekemewa kiasi hiki katika aya za Qur'ani na hadithi za Mtume Muhammad (saw) panoja na Ahlul Beit wake (as)? Tuliahidi kujibu swali hilo katika kipindi chetu cha juma hili.

Hili ni Swali muhimu ambalo tutajaribu kulichunguza na kulipatia jibu kwa pamoja kwa kutegemea nguzo na minara miwili muhimu ya kidini ambayo ni Kitabu cha Mwenyezi Mungu Qur'ani Tukufu na Hadithi za Ahlul Beit wa Mtume Muhammad  al Mustafa (saw). Jumuikeni nasi hadi mwisho wa kipindi.

********

Ndugu wapenzi, tunaanza kutafuta jibu la swali la kipindi hiki kwa kuzingatia kwa makini aya zifuatazo: Aya ya kwanza ni ile ya 32 ya Suratul An'aam ambayo inasema: Na maisha ya dunia si chochote ila ni mchezo na upuzi tu. Na hakika nyumba ya Akhera ni bora zaidi kwa wenye takwa. Basi, je, hamtii akili?

Na Mwenyezi Mungu anasema anasema katika aya ya 64 ya Suratul Ankabut: Na haya maisha ya dunia si chochote ila ni pumbao na mchezo. Na nyumba ya Akhera ndiyo maisha khasa; laiti wangelikuwa wanajua!

Na tunasoma na kuzingatia kwa pamoja aya ya 20 ya Suratul Hadid inayosema: Jueni ya kwamba maisha ya dunia ni mchezo, na pumbao, na pambo, na kujifakhirisha baina yenu na kushindana kwa wingi wa mali na watoto. Ni kama mfano wa mvua ambayo huwafurahisha wakulima mimea yake, kisha hunyauka ukaiona ina rangi ya njano kisha ikawa makapi. Na Akhera kuna adhabu kali na maghufira kutoka kwa Mwenyezi Mungu na radhi. Na maisha ya dunia si chochote ila ni starehe ya udanganyifu.

Wapenzi wasikilizaji tunasoma aya nyingine za 37 hadi 39 za Surat anNaziat zinazosema: Basi ama yule aliyezidi ujeuri.Na akakhiari maisha ya dunia. Kwa hakika Jahannamu ndiyo makaazi yake!

Aya za 16 na 17 za Suratul A'laa zinasema: Lakini nyinyi mnakhiari maisha ya dunia!Na Akhera ni bora na yenye kudumu zaidi.

Na hatimaye tutafakari aya ya 86 ya Suratul Baqarah inayosema: Hao ndio walionunua uhai wa dunia kwa (uhai wa) Akhera; kwa hivyo hawatapunguziwa adhabu wala hawatanusuriwa.

*********

Naam mpenzi msikilizaji, tunajifunza kutokana na aya yulizosoma kwamba jambo linalokemewa na kulaaniwa hapa sio dunia kama dunia bali ni matendo maovu ya mwanadamu ambayo yananfanya asahau lengo la kuumbwa kwake humu duniani na kuanza kuabudu dunia na vilivyomo.

Ni wazi kuwa dunia kama neema kubwa aliyoumbiwa mwanadamu na Mwenyezi Mungu haipasi kulaumiwa bali ni mwanadamu mwenyewe ambaye hupoteza dira na kunza kufuata njia zo upotevu na giza ndiye anayepasa kulaumiwa kwa hilo. Jambo la kulaumiwa hapa si dunia bali ni matendo ya mwanadamu ambaye huamua kuuza Akhera yake kwa mambo ya kidunia yasiyokuwa na thamani yoyote.

Badala ya mwanadamu kutumia dunia kama njia na masurufu ya kujidhaminia Akhera kwa kufanya matendo mema na kumtii Mwenyezi Mungu Muumba, huibadilisha neema hii kubwa na yenye thamani kuwa sehemu ya mchezo, matendo ya upumbavu na kujifakharisha kwa mali na watoto. Kutokana na matendo hayo yasiyo na thamani hupoteza umri wake bure humu duniani badala ya kuutumia kwenye mambo yanayomjengea maisha yake ya kudumu milele huko Akhera, baada ya kuaga kuondoka humu duniani.

Ni wazi kuwa mtu mwenye busara baada ya kutambua kuwa kuna maisha ya milele huko Akhera, anapasa kuutumia umri wake mfupi humu duniani kufanya mambo mema na kujikamilisha kwa thamani za kiutu na kibinadamu ili apate kunufaika na maisha hayo ya milele pamoja na kuepuka adhabu kali ya Mwenyezi Mungu. Kwa maelezo hayo mafupi tunafahamu kwamba kitu kinachokemewa hapa ni kuzama kwenye anasa na starehe za dunia na kuichukulia kuwa shamba la shari badala ya kuwa shamba la Akhera.

Hebu sasa tuzingatie maneno ya Ahlul Beit  (as) ili tuone wanasema nini kuhusiana na suala hili.

Mtume (saw) anasema katika moja ya hotuba zake za kudumu milele kwamba: "Msikhiari kabisa dunia kwa Akhera kutokana na ladha na matamanio. Hii ni kwa sababu Mwenyezi Mungu anasema: (Basi ama yule aliyezidi ujeuri. Na akakhiari maisha ya dunia,) yaani dunia imelaaniwa na kilicholaaniwa hapa ni mambo yote yaliyomo isipokuwa yale ambayo ni ya Mwenyezi Mungu."

Mtume (saw) pia amesema: "Mtu anayepewa dunia na Akhera na akaamua kuchagua dunia badala ya Akhera, atakutana na Mwenyezi Mungu bila ya kuwa na jambo lolote jema litakalomkinga na moto."

Naye Imam Ali alMurtadha (as) amesema: "Mtu anayeabudu dunia na kuikhiari kwa Akhera huwa amedhuru mustakbali wake." Pia amesema: "Iwapo utajaalia dini yako kufuata dunia yako utakuwa umeihilikisha dini na dunia yako kwa pamoja na utakuwa miongoni mwa wahasirika huko Akhera, na iwapo utajaalia dunia yako kufuata dini yako utakuwa umeilinda dini na dunia yako na utakuwa miongoni mwa watu waliofuzu Akhera."

Pia amesema (as): "Enyi watu! Kwa hakika dunia ni makao ya majazi (makao bandia) na Akhera ni makao ya kudumu milele kwa hivyo chukueni kwenye njia yenu (masurufu humu duniani) kwa ajili ya makao yenu ya kudumu milele."

Wapenzi wasikilizaji kwa hivyo jambo linalokemewa na kulaaniwa hapa ni tabia ya mwanadamu ya kughiriki kwenye matamanio na anasa za dunia na kuichukulia kuwa makao yake ya kudumu milele. Huzama kwenye anasa hizo na kughafilika na ukweli kwamba dunia bila shaka ina kikomo na kupuuza mambo ya Akhera ambayo ni ya kudumu milele. Ni kwa msingi huo ndipo aya za Qur'ani  na hadithi tukufu zikakemea tabia ya kupenda dunia kuliko kiasi.

Imepokelewa kwamba Mwenyezi Mungu alimwambia Mtume wake Nabii Musa: "Jua kwamba kila mbegu ya fitina ni kupenda dunia."

Naye Mtume Mtukufu (saw) amesema: "Dhambi kubwa zaidi ni kupenda dunia." Pia amesema: "Kupenda dunia ni asili ya kila maasi na chanzo cha kila dhambi."

Imam Ali (as) amesema: "Bila shaka hautamwona Mwenyezi Mungu kwa amali iliyokudhuru kutokana na kupenda kwako dunia."

Na Imam Jaffar AsSwadiq (as) amesema: "Chanzo cha kila dhambi ni kupenda dunia."

*********

Wapenzi wasikilizaji, baada ya kusema tuliyoyasema katika kipindi hiki, swali jingine linajitokeza hapa ni hili kwamba, je, kila aina ya kupenda dunia inakemewa na je, humzuia mwanadamu kunufaika kwa njia sahihi na neema za Mwenyezi Mungu alizomjaalia humu duniani? Hili ndilo swali tutakalolitafutia jibu katika vipindi vyetu vijavyo inshallah. Basi hadi wakati huo hatuna budi kukuageni kwa kusema, kwaherini.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)