Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 08 Aprili 2013 17:48

Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain (6)

Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain (6)

Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji na karibuni kusikiliza kipindi kingine cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain. Swali la kipindi cha wiki hii linasema je, nini hakika ya sayari hii ya dunia tunayoishi? Katika kujibu swali hili kama kawaida tutategemea vitu viwili vizito ambavyo tumekuwa tukivitegemea katika vipi vilivyopita navyo ni Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Hadithi za Ahlul Beit (as). Hili ni swali muhimu ambalo jibu lake linamfungulia mwanadamu upeo mpana wa maisha mazuri na yaliyojaa saada humu duniani kwa ajili ya Akhera.

*********

Ili kufikia jibu la swali hili tunaanza kwa kuchunguza na kuzingatia kwa makini maana ya aya za 24 na 25 za Suratu Yunus ambapo Mwenyezi Mungu anasema: Hakika mfano wa maisha ya dunia ni kama maji tuliyoyateremsha kutoka mbinguni, kisha yakachanganyika na mimea ya ardhi wanayoila watu na wanyama. Mpaka ardhi ilipokamilika uzuri wake, na ikapambika, na wenyewe wakadhani wameshaiweza, iliifikia amri yetu usiku au mchana, tukaifanya kama iliyofyekwa - kama kwamba haikuwapo jana. Namna hivi tunazipambanua Ishara zetu kwa watu wanaofikiri. Na Mwenyezi Mungu anaita kwendea Nyumba ya Amani, na anamwongoa amtakaye kwenye njia iliyonyooka.

Tutafakari pia aya ya 70 ya Suratul Qaswas ambapo Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema anasema: Naye ni Mwenyezi Mungu ambaye hapana mungu isipokuwa Yeye. Sifa zote njema ni zake Yeye, mwanzo na mwisho. Na hukumu ni yake Yeye. Na kwake Yeye mtarejeshwa.

Kadhalika aya ya 77 ya sura hiyohiyo inasema: Na utafute, kwa aliyokupa Mwenyezi Mungu, makaazi ya Akhera. Wala usisahau fungu lako la dunia. Nawe fanya wema kama Mwenyezi Mungu alivyokufanyia wema wewe. Wala usitafute kufanya ufisadi katika ardhi. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi mafisadi.

Aya ya 39 ya Suratul Ghaafir inasema: Enyi watu wangu! Hakika haya maisha ya dunia ni starehe ipitayo tu, na hakika Akhera ndiyo nyumba ya daima.

Tuzingatie pia aya ya 30 ya Surat an-Nahl inayosema: Na wataambiwa waliomcha Mungu: Mola wenu Mlezi ameteremsha nini? Watasema: Kheri. Waliofanya wema katika dunia hii watapata wema. Na nyumba ya Akhera ni bora zaidi, na njema mno nyumba ya wacha-Mungu.

Imepokelewa kuwa Imam Muhammad al-Baqir aliulizwa maana ya maneno 'na njema mno nyumba ya wacha-Mungu' akasema ni dunia.

*********

Wapenzi wasikilizaji, nukta muhimu tunayoipata kutokana na aya tulizosoma mwanzoni ni kuwa maisha ya humu duniani ni kati ya neema za Mwenyezi Mungu ambazo amezijaaliwa waja wake ili wapate kunufaika nazo katika maisha yao ya humu duniani. Bila shaka kunufaika vyema na maisha hayo kunawapa fursa ya kuweza kufikia ufanisi mkubwa zaidi katika maisha yao ya baadaye yaani maisha ya Akhera. Maisha hayo ni mfano wa maji ya mvua inayonyesha kutoka mbinguni ambapo kila kitu kilicho hai hutokana na maji hayo. Kwa msingi huo hiyo ni neema kubwa ambayo Mwenyezi Mungu anastahiki kushukuriwa kwa kuwapa waja wake.

Licha ya neema na baraka zote hizi zinazopatikana duniani kwa maslahi ya mwanadamu lakini dunia si ya kudumu milele bali itafika siku ambapo itafikia kikomo na kutoweka. Kwa hivyo mwanadamu anapasa kufanya kila juhudi ili anufaike na kila neema aliyopewa na Mwenyezi Mungu humu duniani kwa ajili ya maisha yake ya kudumu milele huko Akhera. Anapokuwa hai humu duniani anapasa kujiweka mbali na ufisadi pamoja na kujiepusha na maovu yanayomsababishia madhambi ili aweze kufikia wema wa nyumba ya wacha-Mungu.

Na sasa tunakirejea kitu cha pili kwa uzito wa kimaanawi na utukufu nao ni Mtume Muhammad (saw) na Ahlu Beit wake watoharifu (as). Tunakuombeni muendelee kuwa nasi hadi mwisho wa kipindi.

******

Imam Ali (as) amesema: "Dunia hutumika kulinda Akhera." Imepokelewa pia kutoka kwa Imam Baqir (as) kwamba amesema: "Msaada bora zaidi wa dunia ni kutumiwa dunia kufikia Akhera."

Maimamu wetu pia wamemnukuu babu yao ambaye ni Mtume Mtukufu (saw) akisema: "Dunia ni shamba la Akhera." Naye Imam Ali (as) amenukuliwa akisema: "Dunia ni shamba la kheri na shari."

Amesema katika hadithi nyingine: "Hakika Mwenyezi Mungu ameumba dunia kwa ajili ya mambo yaliyo baada yake (dunia). Wanadamu wanatahiniwa humu duniani ili Mungu apate kujua ni nani kati yao anatenda mema. Na sisi hatukuumbwa kwa ajili ya dunia." Imam (as) amesema pia: "Dunia imeumbwa kwa ajili ya wengine na sio kwa ajili ya nafsi yake yenyewe." Pia amesema (as): "Ondoeni nyoyo zenu duniani kabla ya kuondoka humo miili yenu, kwani humo mnatahiniwa lakini mumeumbwa kwa ajili ya ulimwengu mwingine."

Imam Swadiq (as) amenukuliwa akisema: "Luqman alimwambia mwanaye: Chukua kwenye dunia mambo yanayotosha kukidhi haja zako na usiyakatae usije ukawa mzigo kwa watu, wala usiingie duniani muingio unaodhuru Akhera yako."

Imam Swadiq (as) alikuwa akisema katika dua ya kumzuru babu yake Imam Hussein (as): "Ewe Mwenyezi Mungu..... wala usijaalie nighafilike kukudhukuru na kukusabihi kwa kunikithirishia neema humu duniani. Dunia ambayo itanishughulisha kwa maajabu ya vivutio vyake wala kunifitini kwa mapambo ya uzuri wake. Wala usinipunguzie neema kiwango cha kudhuru ibada yangu kwako kwa kunifanya nifanye kazi kupita kiasi na kushughulishwa daima na kazi hiyo. Nijaalie duniani mambo yatakayonikinaisha na hivyo kunikinga na maovu ya viumbe wako, na vilevile nijaalie mahitaji yatakayoniwezesha kufikia ridhaa yako."

Na hatimaye tufungue nyoyo zetu ili tupate kunufaika na maneno ya Mtume wetu Muhammad al-Mustafa (saw) ambapo alivihusia vizazi vyote hadi siku ya Kiama kwa kusema: "Na achukue mja duniani masurufu kwa ajili ya Akhera yake, maishani kwa ajili ya mauti yake na ujanani kwa ajili ya uzee wake, kwa sababu dunia imeumbwa kwa ajili yenu na nyinyi mumeumbwa kwa ajili ya Akhera."

*******

Kwa maelezo hayo wapenzi wasikilizaji, tunafahamu kwamba dunia ni neema kubwa ambayo tulitunukiwa na Mwenyezi Mungu ili tupate kutayarisha masurufu yetu kupitia matendo mema ambayo yatatusaidia kujenga Akhera yetu ambayo ni maisha na makao yetu ya kudumu milele.

 Kwa kuzingatia yale yote tuliyoyasema katika kipindi hiki, swali linalojitokeza hapa ni hili kwamba, je, kama dunia ni shamba la kujikusanyia masurufu na mambo yatakayotufanikisha huko Akhera, basi ni kwa nini ikakemewa kwa kiwango hiki katika aya za Qur'ani na Hadithi Tukufu?

Hili ni swali ambalo tutalijibu katika kipindi chetu kijacho panapo majaaliwa yake Mola. Basi hadi wiki ijayo tunakuageni nyote wapenzi wasikilizaji kwa kusema, kwaherini.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)